Na Bakari Kimwanga, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli, amewataka Watanzania wazidi kuiombea Serikali yake kwa sababu kuna majipu mengi na mengine yanahitaji tiba mbadala kupasuliwa.
Amesema kwa miaka mingi, wapo baadhi ya watu serikalini wamekuwa wakifanya vitendo vya ajabu ikiwamo kutoa vibali kwa rushwa, jambo ambalo limekuwa likiwaumiza Watanzania wengi.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, alipozungumza na makundi maalumu ya wasanii, wanahabari na watalaamu wa mfumo ya kompyuta ambao walishiriki kampeni zake za uchaguzi mwaka jana.
Rais Dk. Magufuli, alimshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye amemjengea daraja zuri la kufanya kazi na makundi hayo ambayo yalifanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanampigania yeye na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kampeni na hatimaye kueleweka na Watanzania.
“Nina deni kwa Watanzania kuhakikisha yale niliyoahidi wakati wa kampeni nayatekeleza, ningewaita siku za mwanzo hata kazi ya kutumbua majipu pengine isingewezekana. Lakini tumefanikiwa na tunaendelea nayo maana yapo mengi (majipu) na mengine yanahitaji tiba mbadala.
“Ninachotaka kuwaambia urais si wangu, bali ni wa Watanzania sisi tumeshika dhamana kwa niaba yenu,” alisema Rais Magufuli
Viwanda vya sukari
Pamoja na hali hiyo, Rais Magufuli alisema lengo la Serikali ya awamu ya tano, ni kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kwa kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
Alisema pamoja na changamoto kadhaa zilizopo, watahakikisha wanazishinda ingawa bado kuna baadhi ya watendaji wamekuwa wakitoa vibali vya sukari kuingia nchini.
“Kuna watu wanatoa vibali vya kuleta sukari nchini, wakati kuna viwanda vya ndani. Kama ukifanya hivyo unataka kuwaambia wenye viwanda waache uzalishaji.
“… kwa maana wakifanya hivyo (kufunga viwanda), watu watakosa ajira na Serikali itakosa kodi, wapo watu wanapewa rushwa ili watoe vibali vya sukari kutoka nje.
“Tumejipanga Serikali kuanzia sasa hakuna vibali vya sukari kutoka bila idhini yetu, tunataka viwanda vya hapa nchini vizalishe sana watu wapate ajira na wakulima wa miwa wapate soko la uhakika,” alisema.
Ufisadi wa nchi
Alisema Tanzania ina utajiri wa rasilimali nyingi na ikiwa itatumika vizuri zitawakomboa Watanzania.
Alisema kutokana na kukosekana kwa usimamizi madhubuti watu walitanguliza zaidi ufisadi na hata kufikia kutamani kujijenga zaidi kuliko watu.
“Watu walitanguliza ufisadi zaidi kuliko kumwogopa Mungu walitamani kujenga wao. Kila mahali ni majipu si kama tunapenda kuyatumbua, lakini hakuna namna.
“Kila aliyepata nafasi ya uongozi ni lazima ajue yupo kwa niaba ya wananchi si kwa ajili yake na familia yake. Tufanye kazi zote na tukaongeze spidi zaidi,” alisema
Walalamikaji
Alisema inashangaza kuona watu hao wanaojilimbikizia mali, ndiyo wamekuwa walalamikaji zaidi huku wananchi wakiendelea kuumia.
“Wanalalamika sasa nao ni zamu yao ni vema wakalalamika watu 1000 lakini si Watanzania milioni 50. Ikiwa tutaacha hivi tutashindwa kujibu kwa Mungu Watanzania endeleeni kutuombea,” alisema.
Akumbuka maisha ya kampeni
Katika mkutano wake huo, Rais Magufuli, alisema anakumbuka maisha ya kampeni ambayo kila wakati huyakumbuka ikiwemo baadhi ya nyimbo za kampeni katika Uchaguzi Mkuu.
“Huwa nakaa nakumbuka wakati wa kampeni na hata kukumbuka baadhi ya nyimbo ikiwemo ule unaosema ‘ nyota na ing’are…., najua kuimba ingawa sauti yangu ndio hivyo.
“Hata ule wimbo wa yule mama aliimbaga Magufuli enheee nilikuwa nikisikia CD yake kwenye gari ingawa nilikuwa nachoka lakini nikisikia nyimbo najikuta niko imara na kufanya mikutano zaidi.
“Yote hii kwa sababu waandishi wa habari, wasanii na watu wa IT mlikuwa mkitujenga kupitia vyombo vyenu vya habari pamoja na nyimbo mwanana za wasanii wetu.
“Narudia kuwaambia tulianza wote na tutamaliza wote kikubwa tuzidi kuombeana kwa Mungu ili tuweze kutimiza majukumu tuliyokabidhiwa na Watanzania,” alisema.
Akumbuka pushapu
Alisema anakumbuka katika kipindi cha kampeni akiwa wilayani Karagwe mkoani Kagera, alipiga pushapu jambo ambalo alihisi wagombea wenzake wangefanya lakini baada ya kuona hakuna aliyemwiga aliona tayari ameshawazidi kete kwa kujiongezea matumaini ya ushindi.
Samia na Katiba Mpya
Awali akizunguma katika hafla hiyo Makumu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema hivi sasa kazi iliyobaki kwa Watanzania baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ni kupatikana kwa Katiba Mpya.
“Shughuli inayotukabili mbele yetu ni Katiba Inayopendekezwa, tulifanya kazi pale Dodoma ninawaomba mjitayarishe kwa jambo hilo.
“Nimesoma kwenye vyombo vya habari Mwenyekiti wa NEC anazungumzia Katiba Mpya nami nasema tuhakikishe tunaikamilisha kazi hiyo,” alisema Samia
Wasanii na Cosota
Akizungumzia kilio cha wasanii juu ya Chama cha Haki Miliki Tanzania (Cosota), Rais Dk. Magufuli, alisema naye anashangazwa na hatua ya chama hicho kuwa chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, hali ya kuwa wahusika wanasimamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Alimtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kuhakikisha anaandika barua kwenda kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili achukue hatua zinazohitajika.
Rais alitoa uamuzi huo, baada ya msanii wa kizazi kipya Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, kuwasilisha kilio dhidi ya haki miliki kuhusu Cosota.
Alisema kutokana na Cosota kuwa chini ya wizara nyingine, wasanii bado wananyonywa haki zao za ubunifu huku wanaofaidika ni watu wengine, huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikishindwa kukusanya kodi.
Kutokana na kilio hicho, Rais Dk. Magufuli, aliitaka TRA kuhakikisha wanakusanya mapato kwa kufanya msako kama wanavyofanya kwenye makontena yaliyofichwa.
“Hili la Cosota nimelisikia na nilipokuwa kwenye kampeni, nilisema kwangu ni kazi tu, sasa Waziri Nape kesho (leo), wasilisha barua kwa Waziri Mkuu afadhali naye yupo hapa, kama ni jambo ambalo halihitaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri au kwenda bungeni kwa ajili ya kubadili sheria nitaagiza mara moja Cosota, ikasokotee kwenye wizara yako.
“Huwezi kusimamia watu ambao ndio wahusika ukiwa wizara nyingine na hili tutachukua hatua za haraka,” alisema.
Alisema anataka kuona wasanii wa Tanzania wananufaika na kazi zao pamoja na ubunifu wao ambao vipaji wamepewa na Mwenyezi Mungu.
“Haiwezekani mtu ambaye hahusiki akafaidika na kazi yako, nitoe wito kwa TRA kama wanaweza kushika makontena yaliyofichwa pia wafanye hivyo kwa kazi za wasanii. Kikubwa niwahakikishie tena ndugu zangu tulianza wote na tutamaliza wote.
“Taifa letu tukiwa wamoja tutasonga mbele tusitegemee kuna mjomba wala shangazi atakayekuja kutusaidia, Watanzania wanahitaji Serikali iliyo imara,” alisema Rais Magufuli.