23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Anguko tena kidato cha nne

matokeo ya kidato cha nne*Robo tatu ya watahiniwa wafeli

*Shule za binafsi zang’ara,

*Mkoa wa Morogoro washika mkia

JONAS MUSHI NA BETHSHEBA WAMBURA (RCT), DAR

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2015 yakiwa katika mfumo wa divisheni, ambako ufaulu umeporomoka huku shule za serikali zikianguka vibaya kwa kushika nafasi za mwisho.

Itakumbukwa kwamba mfumo wa upangaji matokeo ulibadilika mwaka 2013  kutoka ule wa divisheni na kuwa wa GPA na tangu kubadilishwa kwa mfumo huo ufaulu ulikuwa ukiongezeka kila mwaka.

Madaraja katika mfumo wa divisheni hupatikana kwa jumla ya alama huku madaraja ya GPA hukipatikana kwa wastani wa alama.

Akitangaza matokeo hayo kwa waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alisema ufaulu umeshuka kwa asilimia 0.8 ikilinganishwa na mwaka 2014.

Alisema takwimu  za matokeo hayo zinaonyesha   bado ufaulu wa masomo  mengi upo chini ya asilimia 50 huku idadi ya watahiniwa waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ikiwa ni robo tu ya watahiniwa wote.

Msonde alisema: “Baraza limefanya tathmini ya awali ya matokeo haya na imeonyesha kuwa ufaulu umeshuka kwa asilimia 0.8 ikilinganishwa na mwaka 2014”.

Kushuka kwa ufaulu hakuchangiwi na kubadilika kwa mfumo, alisema.

Akizungumzia ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule (school candidates), alisema   watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa madaraja ya I-III ni 94,941 (asilimia 24.73).

Msonde alisema watahiniwa waliopata daraja la nne ni 151,067 (asilimia 42.57) huku waliofeli wakiwa ni 113,489 (asilimia 32.09).

Alisema kati ya watahiniwa 433,633 waliofanya mtihani huo, 272,947 (asilimia 67.53) wamefaulu ikilinganishwa na watahiniwa 196,805 (asilimia 68.33) waliofaulu mwaka 2014.

Alisema wasichana waliofaulu ni 131,913 (asilimia 64.84) wakati wavulana waliofaulu ni 141,034 (asilimia 71.09).

Mwaka 2013 watahiniwa 235,227 (asilimia 58.25) ya watahiniwa wote walifaulu mtihani tofauti na mwaka 2012 ambako waliofaulu walikuwa  185,940.

Mwaka 2014 ufaulu uliongezeka kwa wasilimia 10.08 ambako  watahiniwa 196,805 (asilimia 68.33) ya watahiniwa wote waliofanya mtihani kidato cha nne, walifaulu ikilinganishwa na mwaka 2013.

UBORA WA UFAULU

Alisema ufaulu kwa watahiniwa wa kujitegemea (Private Candidates)umepanda ambako watahiniwa waliofaulu ni 31,951 (asilimia 64.80) ikilinganishwa na 29,162 (asilimia 61.12) waliofaulu mwaka jana.

Mtihani wa maarifa ufaulu umepungua na  waliofaulu ni 7,536 (asilimia 46.59) ikilinganishwa na watahiniwa 6,810 (asilimia 55.29) waliofaulu mwaka 2014.

KISWAHILI JUU, HISABATI CHINI

Dk. Msonde alisema somo la Kiswahili ndilo lililoongoza kwa ufaulu wa juu ambako asilimia 7.63 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hilo wamefaulu huku ufaulu wa chini   ukiwa wa somo la Hisabati ambako asilimia 16.76 ya watahiniwa waliofanya somo hilo wamefaulu.

WASICHANA WAONGOZA KATIKA TAIFA

Kuhusu wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri, alisema nafasi ya kwanza imeshikwa na msichana Butogwa Shija wa Shule ya Canossa  akifuatiwa na Congcong Wang, Feza Girls, zote za  Dar es Salaam.

Wanaofuata ni Innocent Lawrence (Feza Boys);  Dominic Aidano (Msolwa); Sang’udi Sang’udi (Ilboru); Asteria Chilambo (Canossa); Belinda Magere (Canossa); Humphrey Kimanya  (Msolwa); Bright Mwang’onda (Marian Boys) na Erick Mwang’ingo pia wa Marian Boys.

SHULE BINAFSI ZAONGOZA

Alizitaja shule 10 bora zilizoongoza  kuwa ni Kaizirege ya Kagera, Alliance Girls Mwanza, St. Francis Girls Mbeya, Alliance Boys Mwanza, Canossa Dar es Salaam, Marian Boys Pwani, Alliance Rock Army Mwanza, Feza Girls, Feza Boys za Dar es Salaam na Uru Seminari ya Kilimanjaro.

Shule 10 za mwisho zilishika mkia zote ni za serikali, alisema.

Hizo ni   Pande ya Lindi ikifuatiwa na Igawa Morogoro, Korona Arusha, Sofi Morogoro, Kurui Pwani na Patema ya Tanga.

Nyingine ni Salviak ya Dar es Salaam, Gubali Dodoma, Kichangani Morogoro na Malinyi Morogoro.

MATOKEO YALIYOZUILIWA, KUFUTWA

Dk. Msonde alisema watahiniwa 23 walipata matatizo ya afya na kushindwa kufanya baadhi ya mitihani na   wamepewa fursa ya kufanya mitihani hiyo katika mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.

Alisema watahiniwa 98 walishindwa kufanya mitihani yao yote kutokana na matatizo ya  afya hivyo wamepewa fursa ya kufanya mtihani mwaka huu.

NECTA imefuta matokeo yote ya watahiniwa 87 waliobainika kufanya udanganyifu na kati yao watahiniwa 25 ni wa kujitegemea, 52 wakuwa  shuleni na 10 ni wa mtihani wa maarifa (QT), alisema.

Katika mfumo wa divisheni kwa kidato cha kwanza hadi cha nne, Dk. Msonde alisema kutakuwa na grade A,B ,C, D na F huku kidato cha sita   ni A, B+, B, C, D, S na F.

Alisema hatua hiyo ya kurudi katika divisheni haibadilishi ubora wa ufaulu kwa vile  thamani ya matokeo haitabadilika.

“Ukiangalia alama za ufaulu kwenye mfumo wa GPA ni sawa na za sasa kwani kiwango cha chini cha ufaulu (D) kilikua 30 na cha juu (A) kilikua ni 75 na imebaki hivyo,” alisema Dk. Msonde.

Kidato cha nne   A alama ni 75-100, B (65-74), C (45-64), D (30-44) na F ni alama 0-29.

Kwa kidato cha sita A ni alama 80-100, B+ (70-79), B (60-69), C (50-59), D (40-49), S (35-39) na F ni alama 0-34.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles