23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI KUISUKA UPYA CCM YAKE

 Rais Dk. John Magufuli
Rais Dk. John Magufuli

Na WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), inatarajia kukutana Desemba 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam, imefahamika.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Msemaji wa chama hicho, Seleman Mwenda, ilisema mkutano huo utatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu (CC), kitakachofanyika Desemba 11 hadi 12, jijini Dar es Salaam.

Ingawa hadi sasa ajenda za vikao hivyo hazijajulikana, lakini wachambuzi wa masuala ya  siasa wanasema, kufanyika kwa vikao hivyo kunatajwa kuwa ni mkakati wa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli  kutaka kuisuka upya CCM.

Baadhi ya wachambuzi hao wanasema uteuzi wa wajumbe watatu wa sekretarieti ya chama hicho kuwa mabalozi ni mwendelezo wa mkakati huo kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho mwakani.

Mbali na hao mjumbe mwingine wa sekretarieti, Dk Asha -Rose Migiro aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na nafasi yake ndani ya chama kuchukuliwa na Pindi Chana ambaye naye ameteuliwa kuwa balozi.

Katika Serikali ya awamu ya nne, Pindi Chana alikuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na baadae mwaka huu aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.

Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Dk. Emmanuel Nchimbi, kuteuliwa kuwa balozi kunathibitisha kuhusu uwapo wa mkakati wa Rais Magufuli kusuka upya chama hicho kwa kuweka sura mpya.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye pia ni Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa chama hatarajiwi kuwapo katika safu hiyo mpya, kwani tayari yupo serikalini.

Mwingini ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Rajabu Luhwavi ambaye ameteuliwa kuwa balozi anazidi kutoa taswira kuhusu mkakati wa Rais Magufuli kusuka upya chama hicho.

Wachambuzi mbalimbali wa siasa waliiambia MTANZANIA jana kuwa Februari 5 mwakani, CCM kitatimiza miaka 40 tangu kuzaliwa kwake huku kikiwa hakijafanya marekebisho makubwa ya muundo wake ili kuendana na hali ya sasa.

Baadhi ya wasomi waliozungumzia muundo huo mkongwe wa CCM ni pamoja na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO),Profesa Gaudence Mpangala ambaye alimshauri mwenyekiti wa chama hicho Rais Dk. Magufuli kuifumua safu nzima ya uongozi kwa sababu kilikua chama cha wala rushwa.

“Chama hicho kilisababisha kujitokeza kwa matabaka baina ya walionacho na wasio nacho na kusababisha chama hicho kupoteza mvuto, baadhi ya viongozi wake walijigeuza Mungu watu huku wakishindwa kuwatumikia wananchiipasavyo.

Profesa Mpangala alisema mpaka sasa wananchi hawakipendi chama hicho kutokana na viongozi hao ambao wanafanya kazi kwa ajili ya kulindana na kuangalia maslahi yao binafsi kuliko wanaowatumikia.

“CCM ilipoteza mwelekeo kutokana na baadhi ya watendaji kushindwa kutumia majukumu yao ipasavyo,wengi wao ni wala rushwa, mafisadi na miungu watu ambao wanashindwa kushughulikia matatizo ya wananchi kutokana na ubinafsi.

“Kutokana na hali hiyo, Rais Dk Magufuli anapaswa kuifumua CCM kwa sababu ni chanzo cha matatizo na malalamiko yaliyosababisha wananchi kutokuwa na imani nayo.

Rais Magufuli anapaswa kuondoa kokoro zote na kupanga safu mpya ambayo itafanya kazi ya kuwatumikia wananchi.

“Viongozi wa CCM lazima wajitafakari wamefanya nini katiba kipindi cha miaka 40 kinachotarajiwa kutimizwa Februari mwakani, kwa sababu malalamiko ni mengi kuliko sifa,”alisema mhadhiri huyo wa RUCO.

Mwingine aliyezungumzia uhitaji wa mabadiliko ndani ya CCM ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana.

Yeye alisema vikao vinavyotarajiwa kufanyika licha ya kuwepo kwenye kalenda ya vikao vya chama lakini pia kunaweza kuwepo mabadiliko ya uongozi yatakayofanywa na Mwenyekiti wake.

Alisema, hali hiyo imedhihirika  baada ya baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu na sekretarieti ya chama hicho kuteuliwa kuwa mabalozi wa nchi mbalimbali, jambo linaloonyesha wazi kuwa, nafasi zao zitajazwa na watu wengine.

“Kitendo cha kuwaondoa baadhi ya wajumbe wa kamati kuu na kuwapa ubalozi kinaonyesha wazi kuwa, kuna mabadiliko ya uongozi yanakuja, lakini mabadiliko hayo yaendane na kuwatumikia wananchi,”alisema Dk. Bana.

Hata hivyo,Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu alisema kuwa, mabadiliko hayo ni ya kawaida kama yaliyofanywa serikalini na kwamba sasa hivi yamehamia kwenye chama.

Alisema anachotaka kufanya mwenyekiti wa chama hicho ni kupanga safu yake ya uongozi ndani ya chama ili aweze kufanya nayo kazi katika kipindi cha miaka mitano ijayo”alisema Profesa Baregu.

Hata hivyo Profesa Baregu haoni jambo jipya kwenye mabadiliko hayo kwa sababu wanachama wa CCM ni wale wale.

CCM aitakayo Dk. Magufuli

Katika hotuba ya Rais Dk. Magufuli baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa chama hicho alisema miongoni mwa mambo atakayoyatekeleza ni kuimarisha utendaji kazi wa chama, huku akimnukuu hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kusema kuwa chama legelege huzaa serikali legelege.

“Nitashirikiana nanyi kujenga chama madhubuti chenye uwezo wa kuisimamia vizuri Serikali ili itekeleze ipasavyo majukumu yake, ikiwezekana tutapitia upya katiba na kanuni zetu ili kukidhi mazingira ya sasa na kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo.

“Tutahakikisha pia tunakuwa na safu bora ya uongozi katika ngazi zote kuanzia shina hadi taifa. Tutaangalia muundo (structure) wa chama chetu katika ngazi mbalimbali na kuondoa vyeo visivyokuwa na tija katika chama na hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi” alisema Dk. Magufuli.

Dk. Magufuli alihoji kuhusu uhalali wa kuendelea kuwapo vijana wa chipukizi ndani ya chama hicho pamoja na baadhi ya safu za uongozi ndani ya chama hicho.

“WanaCCM ni lazima tujiulize je ni kweli katika zama hizi bado tunahitaji mtoto wa miaka 8 hadi 15 kuwa chipukizi kwa ajili ya kumtumia kwenye siasa badala ya kumwacha asome?  Kama akiwepo chipukizi wa CCM, chipukizi wa NCCR au Chadema ama TLP tutakuwa tunajenga nchi ya namna gani?

“Je bado kuna umuhimu wa kuwa na makamanda wa vijana ambao mara nyingi wenye kupewa vyeo hivyo ni wale wenye uwezo wa kifedha pekee?  Je walezi kwenye Umoja wa Wanawake (UWT) bado wanahitajika? Je washauri ndani ya Jumuiya ya Wazazi wanahitajika? Alihoji Dk. Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles