24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA: MIKUTANO YA NDANI MITAMU

Edward Lowassa
Edward Lowassa

Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema anamshukuru  Rais Dk. John Magufuli kwa kuruhusu vikao vya ndani.

Amesema vikao hivo,  “ni vitamu zaidi kuliko vile ya nje.”

Hayo aliyasema   Dar es Salaam alipofungua mafunzo ya siku mbili kwa madiwani, wabunge na viongozi wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam yanayoendelea kutolewa na Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) la   Ujerumani.

Akizungumzia   ziara za kanda zilizofanywa na viongozi wa chama hicho  hivi karibuni, Lowassa alisema vikao vya ndani vimewapa nafasi na muda mwingi wa kuzungumza na wanachama  kwa karibu zaidi.

“Tumefanya ziara, tumeona hali ya barabara ni nzuri lakini hali ni nzuri zaidi tulivyozungumza na wanachama wetu na tunamshukuru Rais.

“Aliona hakuna haja ya mikutano ya nje akatupatia vikao vya ndani, Loh! Ni vizuri, ni vitamu zaidi kuliko vile vya nje.

“Tunapata nafasi nzuri ya kuzungumza na wanachama ana kwa ana, kwa muda mrefu kwa mapenzi na mahaba.

“Nataka niwaambie Chadema ipo imara sana. Watu walidhani wamekata tamaa lakini wapo imara katika kuhakikisha chama kinapata ushindi  mwaka 2020,”alisema Lowassa.

Alisema yapo malalamiko madogo madogo likiwamo watu wengi kutaka uongozi wa chama.

Alipendekeza yawepo mabadiliko katika katiba ya nchi kuongeza nafasi za uongozi.

“Wana malalamiko madogo madogo lakini mengi ni ya uongozi, kila mtu anataka kuwa kiongozi hadi nikakumbuka kule Kenya walipobadilisha  Katiba wakaongeza nafasi za uongozi, magavana, mameya na nyingine ili zipatikane nafasi za siasa za kuongoza  na mimi nadhani tungepata muda tufafanue katiba ili ziongezwe nafasi za uteuzi.

“Au mnaonaje?” Lowassa aliwauliza wajumbe ambao kwa pamoja waliitikia: “Ndiyoo”

Alisema kuna kila dalili ya Chadema kushinda uchaguzi wa 2020.

Aliwataka  viongozi wa chama hicho kushikamana na kuepuka maneno ya kuwagawa akisisitiza kuwa  bila mshikamano hawataweza kushinda uchaguzi ujao.

“Dalili zote zinaonyesha tutashinda lakini kama tutakuwa wamoja.

“Bila umoja hatuwezi kushinda na CCM wanajua maana ya umoja ndiyo maana wanasema umoja ni ushindi, hivyo maneno ya kutugawa tusiyakubali, viongozi tushikamane,” alisema Lowassa.

Alitaja mbinu nyingine ya ushindi kuwa ni kwenda vijijini kutoa elimu kwa sababu utafiti unaonyesha kuwa CCM imekuwa ikishinda maeneo yaliyo nyuma katika elimu.

“Wakati tukiwa Dodoma kwenye ziara kuna vijiji mtu anakuambia mimi nampigia kura Nyerere (Hayati Baba wa Taifa Mwalimu  Nyerere), na akiona polisi anakimbia.

“Sasa kama mtu anakimbia akimwona polisi anawezaje kulinda kura?  Hivyo bila kwenda kutoa elimu vijijini hatuwezi kushinda,” alisisitiza Lowassa na kuongeza:

“ ‘There is no time left’ (Hatuna muda wa kupoteza),  muda uliobaki ni mdogo sana hatuna budi kuutumia vizuri kwa kuangalia wapi tulikosea na turekebishe vipi na tuongee kutoka moyoni tusiogopane.

“Tukosoane bila kusingiziana na tuone muda uliobaki tunafanya nini ili tushinde,” alisema Lowassa.

AINGILIA SUALA LA MAEGESHO

Lowassa pia alionya kuhusu suala la kupandisha gharama za maegesho ya magari   Dar es Salaam na akawataka viongozi wa chama hicho kukaa na kujadiliana suala hilo.

Alisema yapo maneno mengi yameanza kusemwa ikiwa ni mwaka mmoja tangu Chadema ichukue uongozi wa jiji la Dar es Salaam, likiwamo suala la maegesho na kupeana mikataba kienyeji.

Lowassa alisema ni vizuri kuanza kuyachambua kuona ukweli na kuyasema yale waliyoyafanya na ambayo hayajafanywa, ikiwa wanatimiza mwaka mmoja tangu wachukue uongozi wa jiji.

“Yemekuwapo  maneno mengi kuhusu ‘parking systems’ (maegesho) zilikuwa shilingi ngapi na sasa ni ngapi. Contract’ (mikataba) mnapeana kienyeji.

“Wamarekani wana msemo wao ‘job for the boys’(kazi kwa vijana)  ukishaenda kupigana vita mnaporudi mnapewa  kazi mnaambiwa ‘asante kwa kazi’.  Je?  ninyi mnatoa asante kwa kazi au mnatoa kwa watu waliokomaa vizuri?

“Tuzungumze vizuri hii habari ya ‘Great Dar es Salaam’ (Dar es Salaam Kubwa) ‘how we do that job’ (tunafanyaje hii kazi). Tusifike mahali watu wa Dar es Salaam wakaanza kusema afadhali CCM kwa sababu  wakianza kusema hivyo tumekwisha.

“Sasa tunafanyaje tusifikie hapo? Inabidi tukae na nasikitika mameya hawapo lakini naambiwa wapo njiani wanakuja, tuzungumze tujue tunafanyaje,” alisema Lowassa.

MEYA  WA JIJI

MTANZANIA ilimtafuta kwa   simu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema kilichohojiwa kwenye kikao cha jana ni kuhusu mkataba wa kukusanya tozo za maegesho kupewa Mkenya   na kupanda kwa gharama.

Hata hivyo alisema aliweza kueleza kuwa kampuni ya Kenya ilipatikana kwa uwazi baada ya kutangaza tenda ya kimataifa ambako walijitokeza waombaji 37.

Alisema kampuni hiyo ilishinda kwa vile ilikubali kulipa kiasi kikubwa cha fedha na kwa mwezi inalipa Sh  bilioni 2.5 hadi Sh bilioni 4.5 ikilinganishwa na milioni Sh milioni 117 za awali.

Kuhusu kupandisha gharama, alisema tozo zilizokuwa zikitozwa kwa ajili ya maegesho zimepitwa na wakati.

Alisema  tayari kulikuwa na sheria ya mwaka 2014 ambayo ilikuwa inaelekeza kupandisha gharama za tozo, hivyo wananchi hawana budi kuunga mkono suala hilo kwa maendeleo ya jiji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles