28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli kubeba ajenda tatu SADC

NORA DAMIAN NA ANDREW MSECHU

RAIS Dk. John Magufuli leo anatarajiwa kukabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) huku akitazamiwa kusimamia programu tatu za jumuiya hiyo.

Programu hizo zinalenga kuhamasisha utekelezaji wa kaulimbiu ya mkutano huo inayosema; ‘Mazingira Mazuri ya Maendeleo ya Pamoja na Endelevu ya Viwanda, Kuongezeka kwa Biashara ya Kanda na Uzalishaji wa Fursa za Ajira.

Programu hizo ambazo zitasimamiwa na SADC kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU) zitatiwa saini kupitia kwa Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Stergomena Tax na Balozi wa EU kwa Botswana na SADC, Jan Sadek.

Programu hizo zinahusu Uwezeshaji wa Kuboresha Uwekezaji na Mazingira ya Biashara (SIBE), Uwezeshaji kwa Viwanda na Sekta za Uzalishaji (SIP) na Programu ya Uwezeshaji (TFP).

Leo, agenda za mkutano huo zitahusu utoaji tuzo kwa washindi wa kikanda wa mashindano ya insha kwa shule za sekondari za nchi za SADC na tuzo za wanahabari zitakazotolewa leo na mwenyekiti anayemaliza muda wake, Rais Hage Geingob wa Jamhuri ya Namibia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati Maalumu ya Maandalizi ya mkutano huo, baada ya kukabidhi tuzo hizo, Rais Geingob atatoa hotuba rasmi ya kumaliza muda wake wa uenyekiti wa SADC kisha kukabidhi rasmi uenyekiti huo kwa kumvisha beji ya uenyekiti wa SADC Mwenyekiti anayeingia, Rais Magufuli.

“Baada ya kukabidhiwa rasmi uenyekiti wa SADC, Rais Magufuli atatoa hotuba yake ya kupokea wadhifa huo na akiwa mwenyeji wa mkutano huo wa 39 wa Wakuu wa SADC wa Wakuu wa Nchi na Serikali, ataufungua rasmi mkutano wa mwaka huu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika mkutano wa leo viongozi hao pia watajadili utekelezwaji wa maazimio ya mkutano mkuu wa 38 wa Sadc uliofanyika mwaka jana nchini Namibia sambamba na mwelekeo wa mwaka ujao.

Mkutano huo utahitimishwa rasmi na Rais Magufuli kesho baada ya mkutano wa ndani wa marais hao, ambapo Katibu Mtendaji, Dk. Tax atawasilisha makubaliano yaliyofikiwa na marais hao.

Marais wawasili

Tayari marais na viongozi mbalimbali wa nchi wanachama wa SADC wamewasili nchini kuhudhuria mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo unaoanza leo.

Viongozi wengi waliwasili jana kwa nyakati tofauti katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakitanguliwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye aliwasili nchini tangu juzi.

Mpaka tunaenda mitamboni jana viongozi waliowasili jana ni Rais wa Shelisheli, Danny Faure, Rais wa Zambia, Edgar Lungu, Rais wa Angola, Joao Lorenco,  Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) , Felix Tshisekedi na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.

Mbali ya marais hao, nchi nyingine zimewakilishwa na mawaziri ambapo Rais wa Lesotho amewakilishwa na Waziri Mkuu wake, Dk. Motsoahae Thabane huku Rais wa Mauritius akiwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Nandi Botha.

Viongozi wengine wanaotarajiwa kuwasili ni Rais wa Comoro, Azali Assoumani, Rais wa Msumbiji (Filipe Nyusi), Rais wa Namibia (Dk. Hage Geingob), Rais wa Madagascar (Andry Rajoelina).

Kwa mujibu wa taarifa nchi 10 zilithibitisha kuwakilishwa na marais ambazo ni Afrika Kusini, Comoro, Shelisheli, Angola, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Madagascar, Zimbabwe, Msumbiji na Namibia.

Nchi zilizothibitisha kuwakilishwa na mawaziri wakuu ni eSwatini, Lesotho, na Malawi itawakilishwa na Makamu wa Rais, ambapo Botswana na Mauritius zitawakilishwa na mawaziri wa Mambo ya Nje.

Katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wageni hao walipokelewa na viongozi mbalimbali wa Tanzania wakiwemo mawaziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Japhet Hasunga (Waziri wa Kilimo), Jenister Mhagama (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), William Lukuvi (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi).

Wakiwa uwanjani hapo viongozi hao pia walikagua gwaride maalumu na kulakiwa na vikundi mbalimbali vya burudani ikiwemo ngoma maarufu ya kabila la Wangoni.

Pia katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam hasa kuanzia eneo hilo la uwanja wa ndege hadi katikati ya Jiji, kulikuwa na vikundi vya hamasa na burudani kwa ajili ya kuwalaki viongozi hao.

Tanzania itakavyochukua uenyekiti

Katika mkutano huo wa kilele unaofanyika leo na kesho, mojawapo ya tukio muhimu linalosubiriwa kwa hamu ni la Rais Dk. John Magufuli kukabidhiwa rasmi uenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka kwa Rais wa Namibia, Hage Geingob, nafasi atakayodumu nayo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Hatua hiyo inafuatia baada ya Rais Dk. Magufuli kushikilia nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu Agosti mwaka jana.

Uenyekiti wa SADC ni wa mzunguko na kwa mara ya mwisho mkutano huo ulifanyika nchini mwaka 2003 ambapo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alichaguliwa kuwa mwenyekiti.

Nafasi ya Tanzania katika kanda hiyo inaangaliwa kwa jicho pana hasa wakati huu ambapo jumuiya hiyo ina mkakati wa kukuza uchumi wa viwanda hivyo, Rais Magufuli anatarajiwa kuchochea mkakati huo na kuhakikisha anatimiza majukumu yake kikamilifu yanayohusu jumuiya hiyo kwa mwaka mzima ambao atakuwa mwenyekiti.

Nchi wanachama wa SADC wana mategemeo makubwa na uenyekiti wa Tanzania kwamba itasukuma ajenda ya maendeleo hivyo, dhamana kubwa ambayo Tanzania tunayo ni kukidhi matarajio hayo ya nchi wanachama.

Miongoni mwa mambo muhimu ambayo Tanzania imeahidi kuyasimamia inapochukua uenyekiti wa mkutano huo wa 39, ni utekelezaji wa zaidi ya maazimio 107 yaliyofikiwa kupitia Kamati ya Mawaziri wa Sadc, ikiwemo kuidhinisha lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC na kuendesha kampeni maalumu ya kuhakikisha Zimbabwe inaondolewa vikwazo vya kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles