25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mjadala kuongeza muda wa urais unamkera JPM-Polepole

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amewataka wanachama wa chama hicho kutoendelea na mjadala wa kuongezwa kwa muda wa uongozi Rais John Magufuli kwa kuwa unamkwaza.

Alisema hayo jana jijini hapa wakati  akifungua kikao cha Baraza la Jumuiya ya Wanawake wa Chama hicho (UWT).

Polepole alisema aliitwa na Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho na kumtaka awatangazie Watanzania kwamba nchi inaongozwa kwa Katiba na sheria hivyo amesikia watu wakizungumza kuhusu kuongezewa muda baada ya kumaliza ukomo wa muda wa uongozi wake jambo ambalo linamkwaza.

Alisema muda wake wa kumaliza uongozi ukifika atang’atuka mara moja na hata ongeza hata dakika tano kwa kuwa uongozi ni mgumu.

“Wale wanachama wenzangu ambao mnaendeleza huu mjadala wa kuongezwa muda wa uongozi naomba muuache maana mwenyekiti anasema anakwazwa nao,”alisema.

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Polepole alisema katika mchakato wa kuteua wagombe, wajiepushe kuteua watu ambao ni walaghai na wasio kubalika na jamii kwa kuwa inawavunja moyo wanawake.

“Wapiga kura waaminifu ni wanawake lakini tungesema wanaume wakapige kura tungeshaliwa kitambo. Tusiwavunje moyo wanawake kwa kuwateulia wagombea wasio na uwezo,”alisema.

Alisema kuendelea kuwatumia wanawake kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuwa wanaweza kulisaidia Taifa kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

Alisema wanawake hawaibi na wala hawachukui rushwa na pia uwepo wao kwenye maeneo muhimu ndio salama ya Taifa kwa kuwa wanajua mengi yanayogusa watu wote.

Aliwataka wanawake kuyaweka maarifa yao mezani na kuendelea kupigania kuwepo kwa 50 kwa 50 kwenye nafasi za uongozi kama ambavyo Ilani ya CCM ya mwaka 2015 inavyoelekeza.

Aliagiza UWT kutengeneza kanzi data ambayo itaonyesha wanawake na elimu zao ili waweze kupata nafasi mbalimbali za uteuzi.

“Chama kinatambua ushindi wake, ukubalifu wake kwa umma na mafanikio ndani na nje ya chama, yamekuja kwasababu ya umoja wa wanawake wa watanzania na wanawake wa chama,”alisema Polepole.

Alisema kuwa awamu zote za uongozi kulikuwa hakuna mama lakini awamu ya tano katika viongozi wakuu wa nchi yupo mama ambaye ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na kwa kipindi cha miaka miwili mambo mengi yamefanyika kuwagusa wanawake ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya.

Naye, Katibu wa UWT Taifa, Queen Mlozi, alisema mabaraza hayo yamekuwa yakilenga kuwainua wanawake kiuchumi na kisiasa huku akisisitiza kuwa wataendelea kumlinda na kumtetea Rais Magufuli kwa mshikamano wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles