25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli awafuta machozi wafanyakazi

1* Ashusha PAYE hadi asilimia 9 kima cha chini

* Kada ya kati na juu waendelea kuumia

Elizabeth Hombo na Ramadhan Hassan, Dodoma

RAIS Dk. John Magufuli jana aliwafuta machozi wafanyakazi kwa kutangaza kupunguza kiwango cha kodi katika mishahara (PAYE) kutoka asilimia 11 ya sasa hadi tisa kitakachoanza mwaka wa fedha wa 2016/17.

Mkuu huyo wa nchi alifanya hivyo wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi na wafanyakazi waliohudhuria katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa viwango vya kodi vilivyopo sasa, punguzo hilo litawabeba zaidi wafanyakazi wa kada ya chini wanaolipwa mshahara kuanzia Sh 170,000 hadi Sh 360,000.

Kwa mujibu wa viwango hivyo, wafanyakazi wanaolipwa kuanzia Sh 361,000 hadi Sh 540,000 wanakatwa kodi ya asilimia 20, huku wanaopata kuanzia Sh 541,000 hadi Sh 720,000 na kuendelea wanakatwa asilimia 25-30.

Hatua hiyo ya Rais Magufuli ni kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni kusaidia watu wa kada ya chini kuboresha maisha yao.

Hata hivyo, Rais Magufuli alishindwa kukata kiu ya wafanyakazi hao kwa kutotangaza nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kama walivyotarajia.

“Nimesikiliza kero zenu na sitaweza kuzijibu hoja zote zilizotolewa kwenye risala zenu na Mgaya (Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicolas Mgaya), Serikali tumezipokea kero zenu na tutazifanyia kazi.

“Lakini nitagusia machache, kikubwa napenda kuwaarifu kwamba Serikali yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu, nimeamua kupunguza kodi ya makato ya mishahara, yaani PAYE, kutoka asilimia 11 hadi tisa kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/17 nikiwa na mategemeo makubwa wabunge watapitisha katika bajeti, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewapunguzia wafanyakazi mzigo mkubwa,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa na maelfu ya wafanyakazi waliohudhuria maadhimisho hayo.

Alisema ameanza na hilo la PAYE, na kwamba baada ya changamoto zote za uchumi kukaa sawa, atawapandishia wafanyakazi mishahara.

“Nimeanza na hili kwanza ili changamoto zote za uchumi tuweze kuzikabili, na baadaye mambo yakiwa mazuri tutapandisha mishahara na siku zote msema kweli ni mpenzi wa Mungu ndugu zangu. Tukipunguza hili la PAYE tutakuwa na pengo kubwa la makusanyo ya kodi.

“Watu pekee ambao hawakwepi kodi ni wafanyakazi, wengine wote wanakwepa, kwa mfano wafanyabiashara. Lakini wafanyakazi hawana njia ya kukwepa mshahara, ukishaingia tayari wameshakatwa. Baada ya ku-‘save’ hizi fedha nyingi kwenye mishahara hewa, tutakaa na viongozi wenu wa TUCTA na tutaangalia ni namna gani tutaongeza mishahara yenu,” alisema.

 

FAINI YA PAPO KWA HAPO

Aidha katika hotuba yake, Rais Magufuli alisema Serikali yake haitawavumilia waajiri ambao hawatoi mikataba kwa wafanyakazi wao.

Alisema Serikali yake iko mbioni kurekebisha sheria ya kazi ambayo adhabu itakuwa ni ya papo kwa hapo.

“Wapo waajiri wengi hawatekelezi mikataba ya sheria ya ajira, na yapo malalamiko mengi ya wafanyakazi ya kutokuwa na mikataba ya kazi, michango ya pensheni au kutowasilishwa kwenye mifuko ya jamii.

“Serikali haitawavumilia na tutaanzisha adhabu ya hapo kwa papo… tutarekebisha sheria ya ajira, na waajiri ambao hawatatekeleza watapigwa faini.

“Katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya kuajiri maofisa kazi 21, na ninawaomba hao watakaojiriwa na wale waliopo wasije waka-‘compromise’ na waajiri… wakasimamie maadili ya kazi yao,” alisema Rais Magufuli.

 

WAAJIRI KUKIONA

Kuhusu wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi, Rais Magufuli alisema waajiri ambao watakuwa wanawazuia wafanyakazi wao kujiunga na vyama hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.

“Waajiri waruhusu wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi, na suala hili si la hiyari bali ni wajibu, wawaruhusu bila kushurutishwa au kuchaguliwa chama cha kujiunga, waajiri wote wanaovunja sheria hii watachukuliwa hatua.

“Lakini naomba niwaambie vyama hivyo visitumike kuchochea migogoro kazini, visitumike vikawa vya kisiasa, vilete utulivu sehemu za kazi,” alisema.

 

WAGENI WASIO NA VIBALI

Akizungumzia wageni walioajiriwa nchini, Rais Magufuli alitoa agizo kwa wizara zote kuwafichua wote wanaofanya kazi bila vibali.

“Kushugulikia ajira za wageni wakati wazawa wapo… naagiza wizara zote zisimamie hili suala kwa nguvu zote, hata kwenye hoteli mtu anatoka nje, hili haliwezekani. Tumekuwa watu wa kushinikizwa na hawa watu,” alisema.

 

MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII

Akizungumzia mifuko ya hifadhi ya jamii, Rais Magufuli alisema Serikali yake itaipunguza.

“Serikali itapunguza idadi ya mifuko ya hifadhi za jamii na hili tutalikamilisha ndani ya mwaka 2016/17. Kwa sababu hifadhi hizi zimekuwa zikiingia kwenye miradi ya ajabu ajabu. Wawekeze kwenye viwanda ili kupanua wigo wa ajira na kujipatia wanachama zaidi.

Ukiwekeza kwenye kiwanda cha nguo utapata wanachama wengi na tutakuwa tumejenga uchumi imara.

“Lakini ukiwekeza kwenye daraja au karavati, hiyo karavati ikajengwa kwa mwezi mmoja wale wafanyakazi watakuwa ‘temporary’, wala hawatakuwa kwenye mkataba kwa sababu yule mkandarasi akishamaliza anaondoka, hao ni wa muda huku wewe unataka upate hela, hao ni wa ‘short term’.

“Wanavyuo wanamaliza vyuo lakini hawapati ajira. Lakini hawa watu ni wanyama kweli, ni wabinafsi kweli kweli,” alisema.

 

MAOMBI YA TUCTA

 

SHIRIKISHO la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limeiomba Serikali kushughulikia kero za wafanyakazi ambazo zimekuwa sugu kwa kipindi kirefu.

Akisoma risala ya wafanyakazi, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Nicolaus Mgaya alisema mwaka 2006 TUCTA ilifanya uchambuzi wa gharama za maisha na kubaini kuwa familia ya mfanyakazi yenye watu sita ilihitaji kima cha chini cha mshahara wa Sh 315,000 kwa mwezi.

“Kutokana na kuendelea kupanda kwa gharama za bei za bidhaa na kushuka kwa shilingi ya Tanzania, ni wazi kwamba Sh 315,000 ni ndogo na ni mateso makubwa kwa wafanyakazi kwani haijapanda kwa zaidi ya miaka kumi sasa,” alisema.

Mgaya pia alimweleza rais Magufuli kuwa Wizara ya Kazi inashindwa kusimamia sheria za kazi ipasavyo kwa kuwa inapewa bajeti ndogo.

“Tungependa kuona wizara hii ikipewa bajeti toshelezi, wataalamu toshelezi na vitendea kazi toshelezi ili iweze kusimamia haki za wafanykazi, ili waweze kufanya kazi vizuri,” alisema Mgaya.

Kutokana na hilo, alisema kwa sasa wanahitaji kima cha chini cha Sh 750,000 ambayo itakuwa haijakatwa kodi ili kuweza kukabiliana na ugumu wa maisha.

Pia aliomba ibaki mifuko miwili ya hifadhi ya jamii, mmoja wa sekta ya umma na mwingine wa binafsi ili kupunguza gharama za uendeshaji.

“Licha ya kwamba wafanyakazi tumekuwa na kilio cha muda mrefu cha kulipwa kima cha chini kisichotosheleza kumudu kupanda kwa gharama za maisha, mshahara huo mdogo pia unatozwa kodi, kodi hii inawaumiza sana wafanyakazi,” alisema.

Pamoja na mambo mengine aliitaka Serikali ya awamu ya tano kuhamia Dodoma ili kupunguza gharama katika utendaji huku akitolea mfano wa nchi za Nigeria ambayo imehamia Abuja na Malawi kuhamia Lilongwe.

 

MABANGO YA WALIMU

Yalipoanza kuingia maandamano ya walimu, uwanja mzima ulilipuka kwa shangwe, huku wakiwa wamebeba mabango mbalimbali mengine yakisomeka; “Shemeji bila mimi mwalimu usingekalia kiti hicho”, “Awamu ya tano walimu ofisini hadi nyumbani”, “Bila kuongeza bajeti ya elimu, elimu bure ni ndoto”.

Rais Magufuli aliwasili katika uwanjani saa 07:15 ambapo baadaye alipokea maandamano ya wafanyakazi mbalimbali.

Viongozi wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, mawaziri, wabunge na viongozi wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles