29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Matusi ya mke wa waziri yampandisha cheo trafiki  

dr-augustine-mahigaNA VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM

LUGHA ya matusi anayodaiwa kutoa mke wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani imegeuka neema kwa askari huyo.

Rais Dk. John Magufuli amemuagiza Kamishina wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu kumpandisha cheo askari huyo ikiwa ni tuzo ya kutukanwa akiwa kazini.

Alitoa agizo hilo juzi wakati alipokuwa akifungua kikao cha makamanda wa polisi wa mikoa, ambapo alisema tayari ameshamuonya waziri ambaye mke wake alimtukana askari huyo.

“Hakuna kiongozi au familia ya kiongozi iliyoko juu ya sheria,” alisema Rais Magufuli.

Katika sakata hilo, mke wa Mahiga anadaiwa kumtukana askari huyo ambaye alikuwa katika kituo chake cha kazi akitekeleza majukumu yake.

Mapema jana asubuhi, kwenye mitandao ya kijamii ilisambazwa sauti ya mahojiano baina ya askari huyo, mkuu wake wa kazi pamoja na mke wa Mahiga.

Katika sauti hiyo, alisikika askari huyo akilalamikia kitendo cha mke wa Mahiga kumtusi pale alipotaka kumwandikia faini dereva wake kwa kosa la kukanyaga alama ya pundamilia.

 

MAHOJIANO YALIVYOKUWA

Askari: Haloo afande… Lango 115 nimemkamata akiwa amevuka ‘zebra cross’ wakati namtaka ‘assign’ kwa kosa alilofanya akaanza kunitukana… anasema yeye ni mke wa waziri… nikamwambia hili ni kosa la dereva, nikamuuliza anatukana kwa sababu gani.

“Nikamwambia gari siiruhusu naipeleka kituoni. Wakati namuamuru dereva apeleke gari kituoni alitaka kuondoka, nikamnyang’anya funguo,” alisema.

Upande wa pili: Kwa hiyo alikutukanaje?

Askari: Amenitukana kuwa mimi ni mshenzi, sina akili… Anasema yeye ni mke wa Waziri Mahiga.

Upande wa pili: Sasa Mahiga ni waziri yupo juu ya sheria?

Askari: Sijui afande kama yupo juu ya sheria, mimi nimeamua kuizuia gari kituoni taratibu zingine ziendelee.

Upande wa pili: Ok, huyo mama yupo hapo?

Askari: Ndio.

Upande wa pili: Nipe niongee naye. (kinapita kitambo kidogo) Habari yako.

Mke wa Mahiga: Salama… huyu baba ni hivi… mimi naitwa mama Mahiga, sikumtukana wala sikusema hayo maneno ‘anayoni-cot’ ameamkaje mimi sielewi, kitu nilichomwambia kwamba huyu kijana alikuwa anakwenda moja kwa moja, mimi nilikuwa na visenti kidogo.

Kijana akachepuka na sehemu anayotakiwa kuchepuka ni hapa Namanga, akatusimamisha na kusema eti alisimama kwenye ‘zebra cross’, nikamwambia sawa hilo ni kosa la kuelimishwa, lakini sasa anamuandikia kwa kosa kama hilo… ni dogo, ‘very minor’ (dogo sana), si la kumwandikia lakini kama unaandika, andika hiyo Sh 30,000 sijui wanalipia wapi. Akatuelekeza, nikasema mngeheshimika zaidi kama mngeweza ku-‘negotiate’ kosa ‘sub scouting’ na nimeona mapolisi wengi wanakosea hapo, kitu kidogo mnakikuza kinakuwa kikubwa.

Upande wa pili: Unasema hilo ni ‘very minor’, unafahamu adhabu yake?

Mke wa Mahiga: Hapana… Basi nimekosa.

Upande wa pili: Hilo ni kosa kubwa na kama dereva akimgonga mtu na kufikishwa mahakamani ni kifungo jela, hakuna hata faini. Huyo dereva anajua maana yake na anapokaribia anatakiwa a-‘slow down’.

Mke wa Mahiga: Hakuna ubishi lakini, nilitaka aelewe (askari) mimi nimeendesha nchi nyingi, naelewa sheria na nikamwomba amfundishe huyu dereva.

Upande wa pili: Tufikie mahali tusifuge uovu, huyo dereva afundishwe kwani hakwenda darasani? Suala hilo tunategemea mtu yeyote aliyepita chuo ni ‘mandatory’, awe anafahamu. Huko nje ulikotembelea naamini unajua jinsi wanavyoheshimu na hasa hawa madereva wetu huwa wanaheshimu, sasa ile kuchekeana inaleta mazoea.

Nilitegemea kwamba amekosea na anachoagizwa na askari afuate, vinginevyo kama (askari) angekuwa ameomba rushwa ingekuwa kosa lingine.

Hivyo naagiza dereva aadhibiwe, hatuko kutazama nani ni nani. (Askari) huyo dereva muandikie faini, hakuna aliye juu ya sheria.

Askari: Sawa mkuu, lakini nilitaka nimfungulie mashtaka mahakamani.

Upande wa pili: Hayo sasa ni yako, lakini muandikie hiyo faini kwa mujibu wa sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles