>> Awaambia wasipolipa kodi ndani ya muda huo wataisoma namba
>> Afichua serikali kutopeleka fedha za maendeleo Wizarani
>> Amuonya mfanyabiashara anayetaka kumili ufukwe wa Coco
Na Kulwa Mzee , Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli, ametoa siku saba kwa wafanyabiashara waliopitish makontena yao bandarini bila kulipa kodi, kujisalimisha wenyewe na kulipa fedha hizo za serikali na watakaokamatwa baada ya muda huo watachukuliwa hatua zaidi za kisheria.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli, imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam, Novemba 27, mwaka huu ambapo alibaini makontena 349 yalitolewa bila kulipiwa kodi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh. bilioni 80.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Dk. Magufuli, alipokutana na Wafanyabiashara wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), aliwataka wafanyabiashara hao kulipa kodi, kwani licha ya Serikali kuhitaji fedha lakini inataka mahusiano mazuri na wafanyabiashara.
“Kwa wale ambao kwa bahati mbaya walikwepa kulipa ushuru wasihangaike kuyaficha makontena yao, natoa siku 7 wakalipe kodi yao ili wakaishi kwa raha wala wasiwe na wasiwasi, utahangaika kuyakimbiza kule, unajua kontena haliko kama sindano, ukilibeba huko mwishowe litakuponda bure.
“Nenda ukalipe kwa muda huu wa siku saba kwa wale wafanyabiashara mbao walikwepa ushuru wa Serikali waende wakalipe hakuna atakayewashtaki kwa sabbu sisi tunachotaka ni kodi yetu.
“Pia tunataka mahusiano mazuri na wafanyabiashara lakini baada ya siku 7 kuanzia leo (jana), tukiwakamata itabidi sheria itumike, nenda ukalipe tupate kodi tuendeshe nchi, kama unataka mradi mwingine omba utapewa.
“Nataka niwahakikishie kama kuna mfanyabiashara yeyote anataka kufanya uwekezaji na akacheleweshwa na mtu yeyote ambaye yupo chini ya mamlaka ya uteuzi wangu, nasema hatabaki kwenye serikali huyo mtu kwa sababu atakuwa anatuchelewesha tunapotaka kwenda,” alisema Dk Magufuli.
Dk. Magufuli pia aliwaahidi wafanyabiashara hao ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuachana na kodi ambazo zimekuwa kero kwao.
Alisema kuliko kuwa na utitiri wa kodi ni bora kuwe na kodi inayoeleweka na inayolipika na watu wote.
Alisema kukiwa na kodi hizo, watu wengi watalipa kodi kuliko sasa ambavyo wanalipa wachache huku wengi wakijaribu kuikwepa.
Coco beach
Kuhusu eneo la Coco beach lililopo ufukweni mwa bahari jijini Dar es Salaam lenye mgogoro baada ya kununuliwa na mfanyabiashara mmoja, Dk. Magufuli alisema Serikali haipo tayari kuona wanyonge wakionewa kwa kunyimwa haki yao na wachache wanaotumia fedha zao kununua maeneo ya wazi.
“Unaona eneo la wazi unataka uling’ang’anie kwa kuwa una uwezo wa kurubuni watu wa serikali na ukazuia watu wa Manzese ambao ndio eneo lao la kwenda kufurahi, saa nyingine unaweza kimbilia mahakamni, lakini kumbuka Serikali ipo na ni ya John Pombe Magufuli, kama unataka kuendeleza eneo mbona maeneo yapo mengi tu.
“Kachukue eneo ambalo halina matumizi yenye maslahi na umma, watu wataenda huko na itasaidia hata kupunguza faleni mjini sasa wewe umeng’ang’ania hapo hapo tu, najua mmepaelewa, haiwezekani siyo kwa utawala wangu, na bahati nzuri nimekaa wizara ya ardhi nafahamu lile eneo lote, unaweza kujenga kwa nguvu lakini wakazi wa Dar es Salaam wapo zaidi ya milioni tano wanaweza wakaja kulibomoa,” alisema Dk Magufuli.
Hakuna fedha za maendeleo
Alisema tangu bajeti ya 2015/16, awamu ya kwanza ya fedha za maendelo zimeanza kutolewa hivi karibuni ikiwa ni miezi sita imepita.
“Ninavyozungumza hapa tangu bajeti ya 2015/16 ipitishwe ilikuwa haijatolewa hela yoyote ya maendeleo, katibu mkuu yupo hapa, hata senti tano, nafikiri tumetoa mwezi huu ikiwa ni karibu miezi sita imepita, hakuna fedha yoyote ya maendeleo iliyoenda kwenye wizara yoyote, fedha yote tulikuwa tunaitumia kwa ajili ya mishahara na vitu vingine,” alisema.
Alisema wakati mwingine Serikali inapojaribu kuchukua hatua haifanyi kwa ajili ya ujeuri ila inafanya kwa nia njema, ili malengo ya Watanzania wa chini wapate kile wanachopaswa kukipata.
“Mwezi huu ndiyo tumetoa hizo fedha za maendeleo bilioni 120, lakini kwa miezi yote tangu bajeti ipitishwe ilikuwa haijatoka hata senti tano hata OC (matumizi mengine), ilikuwa ni tatizo, kwa hiyo niwaombe sana mimi nitatoa ushirikiano mkubwa na serikali yangu, nataka mfanye kazi kwelikweli.
“Ndiyo maana nilijiepusha sana na mchango wowote kutoka kwa wafanyabiashara yoyote, kama yupo mfanyabiashara aliyenichangia hata Sh mbili asimame anyooshe mkono, nilikwepa kwa sababu nilitaka iwe kazi tu,” alisema Dk Magufuli.
Tunategemea sekta binafsi
Alisema Serikali inategemea sana sekta binafsi na upande mwingine sekta binafsi zinaitegemea serikali, hivyo wakiungana pamoja na kuweka maslahi ya taifa mbele nchi hii ni tajiri sana.
“Haiingii akilini mfano sekta ya madini, nchi ya kwanza kuuza Tanzanite ni India, ikifuatiwa na Kenya, wakati madini hayo yanatoka Tanzania. Nilitarajia sekta binafsi mtakaa na kusema inatosha inatosha. Kwa nini tusichonge Tanzanite wenyewe wale wa nje waje kununua hapa?,” alihoji Dk. Magufuli.
“Mchanga unaohesabika kama ‘west product’, unasafirishwa inaharibu barabara zetu, inaenda hadi bandarini kupakiwa na kusafirishwa nje ya nchi, wakati wanapochimba mchanga ndani kuna madini mengine kama shaba ambayo yangeweza kutoka hapa hapa iwapo kungekuwa na kiwanda,” alisema.
Dk. Magufuli, alisema hayo yanafanyika wakati sekta binafsi ipo na kuongeza kwamba angejitokeza tajiri wa kujenga kiwanda cha kutenganisha mchanga huo angempongeza sana.
Aliomba wafanyabiashara wa sekta binafsi kufanya kazi zao vizuri kwani wakifanya hivyo, nchi haiwezi kuhitaji misaada kwa kuomba omba huku akitolea mfano sekta ya mabenki ambayo imekuwa ikifanya kazi na serikal.
Mashine za EFD
Akizungumzia mashine za EFD, Dk. Magufuli, alihoji kwa nini wafanyabiashara wasipewe mashine hizo bure wakati hazifiki hata Sh milioni 12, halafu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikawa inaangalia mapato kutoka kwao.
Awali, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais Dk. Magufuli ni rafiki mkubwa wa sekta binafsi na hilo limekuwa kundi la kwanza kukutana nalo hata kabla hajaunda Baraza la Mawaziri.
Alisema wafanyabiashara na wawekezaji ni wabia wakubwa wa Serikali na wana mchango mkubwa na kuwaambia wafanyabiashara hao watafaidika sana chini ya uongozi wa Rais Dk. Magufuli.
Mwenyekiti wa TPSF
Mwenyekiti wa Taasisi za Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi alimpongeza Dk. Magufuli kwa kuchaguliwa na kusema kwamba sekta binafsi inaamini Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wana nia ya dhati ya kupunguza au kuondoa changamoto zinazowakabili Watanzania.
Alisema TPSF ipo tayari kushirikiana na serikali yake kuhakikisha kodi stahiki zinalipwa na wapo pamoja katika vita ya ufisadi.
Dk. Mengi aliomba katika mapambano ya rushwa izingatiwe misingi ya utawala bora, Sheria ya Kupambana na Kuzuia Rushwa ya 2007, ifanyiwe marekebisho ili kuipa TAKUKURU, mamlaka ya kuchunguza na kuzitolea uamuzi.