29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli atoa maagizo mazito

NORA DAMIAN Na ELIYA MBONEA

-DAR/CHATO

RAIS Dk. John Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza idadi ya watalii nchini ili kutimiza lengo la kupokea watalii milioni 2 kwa mwaka ifikapo 2020.

Sekta hiyo inaipatia nchi asilimia 25 ya fedha za kigeni na kushika nafasi ya kwanza, inachangia asilimia 17 katika  pato la Taifa, ajira za moja kwa moja 600,000 na zisizo za moja kwa moja milioni 2.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa Hifadhi ya Burigi – Chato katika Kijiji cha Mkolani wilayani Chato mkoani Geita, Rais Magufuli alisema idadi ya watalii  imeongezeka kutoka milioni 1.1 mwaka 2015 hadi  milioni 1.5 mwaka 2018.

Alisema Aprili 2019, Serikali ilipokea watalii 1,000 kutoka Israel na kwamba wanatarajia kupokea watalii 10,000 kutoka China ambapo tayari kundi la watalii 300 kwanza liliwasili Mei.

“Ni lazima tuwasake watalii mahali popote, Misri na Morocco watalii wanaotembelea ni zaidi ya milioni 10 sisi milioni 1.5 wakati ni wa pili duniani kwa kuwa na vivutio vizuri, lazima tubadilike.

“Wahamasisheni Watanzania kwa kuweka gharama nafuu, tujijengee utamaduni wa kutembelea vivutio vyetu vya utalii na kuanzisha hifadhi ndogondogo za kufuga wanyama pori… na mimi nafikiria hilo ila nitafuga wale wanyama wapole nisije nikajikuta nimekuwa kitoweo humo ndani,” alisema Rais Magufuli.

Hata hivyo alisema baadhi ya watalii wamekuwa wakilalamika gharama za utalii kuwa juu, usafi kwenye hoteli na kuitaka wizara iangalie gaharama za wazawa zinakuwa chache.

Kulingana na Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa mwaka 2018 watalii bilioni 1.4 walitembelea maeneo mbalimbali na kuingiza Sh trilioni 1.4 na kwenye kila ajira 10 duniani moja inahusiana na masuala ya utalii.

SIKU YA MAVUNO

Rais Magufuli pia alipendekeza kutengwa kwa siku maalumu ya mavuno na ikibidi yafanyike mabadiliko ya sheria. 

“Hamtoagi ofa hata siku moja, angalau hawa vijana nao wale hata mnyama anayemtunza, kama kuna suala la kubadilisha sheria mbadilishe. Huwezi ukawa unachunga tu, unawalinda, unamuona swala halafu uruhusiwi kula hata siku moja, huo nao ni ufugaji mbaya, ni lazima tujiwekee mikakati.

“Kenya kuna hoteli moja ambayo inauza wanyama pori ni kibali kimetolewa sasa kwanini waziri msiangalie katika ‘regulation’ zako angalau hata baada ya miezi miwili au hata mitatu ili msiwashambulie wanyama mkawamaliza kule kule, mnapanga angalau siku moja ya kula mavano yenu.

“Ndio maana kuna siku za mavuno ninyi hamjawahi kuwa na siku za mavuno kila siku mnawavunia wengine kwenda kula,” alisema.

UJANGILI

Rais Magufuli alisema vitendo vya ujangili vilikuwa vinatishia uwepo wa wanyama katika hifadhi hususani tembo na faru, lakini tangu kuanzishwa kwa kikosi kazi cha kupambana na ujangili mwaka 2016 kimesaidia kuongezeka kwa idadi ya wanyama katika hifadhi.

Alisema miaka ya 1990, idadi ya tembo ilifikia 130,000, lakini walipungua na kufikia 43,330 mwaka 2014, wakati faru miaka ya 1970 walikuwa kati ya 7,000 hadi 8,000, lakini walipungua.

Alisema hivi sasa tembo wameongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 na kufikia zaidi ya 60,000 na faru wamefikia 163.

“Hakuna budi kupongeza kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na faru Rajabu (mtoto wa Faru John) ambaye amezalisha watoto 40. Nadhani yule wajina wangu John alikuwa hajitumi vizuri,” alisema Rais Magufuli.

UPEKEE HIFADHI YA BURIGI

Hifadhi ya Taifa Burigi – Chato ambayo imetokana na kuunganishwa kwa mapori ya akiba ya Kimisi, Burigi na Biharamulo ni maarufu nchini kutokana na maliasili za wanyama, mimea na mandhari nzuri ambazo ni kivutio muhimu kwa utalii.

Rais Magufuli, alisema hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 4,702 na kuifanya ishike nafasi ya tatu kwa ukubwa nchini. Hifadhi inayoshika nafasi ya kwanza ni Ruhaha yenye kilomita za mraba 20,300 ikifuatiwa na Serengeti yenye kilomita za mraba 14,763 iliyoanzishwa mwaka 1959.

Hifadhi nyingine mpya ni Ibanda – Kyerwa na Rumanyika – Karagwe ambazo zinafanya idadi ya hifadhi zote nchini kufikia 19, mapori ya akiba 23, mapori tengefu 44, hifadhi za misitu 463, misitu asilia 17 na mashamba ya miti 23.

Alisema nchi sasa ina eneo la hifadhi lenye kilomita za mraba 361,594 ambalo ni zaidi ya theluthi moja ya nchi kulinganisha na nchi zingine.

Alitaja baadhi ya nchi na maeneo yao ya hifadhi kwenye mabano kuwa ni Burundi (2,066), Kenya (72,544), Malawi (32,242), Msumbiji (170,662), Rwanda (2,320), Uganda (39,059), Zambia (286,161), Algeria (174,219), Angola (87,507), DRC (324,290), Misri (129,390), Ethiopia (274), Nigeria (127,359) na Afrika Kusini (101,336).

“Ndio maana wakati mwingine huwa tunashangaa watu wanaotutuhumu kwamba hatupendi mazingira, tusingetenga eneo kubwa kiasi hiki au kuanzisha hifadhi tatu kwa mpigo,” alisema Rais Magufuli.

Kuanzishwa kwa Hifadhi za Burigi – Chato, Ibamba – Kyerwa na Rumanyika – Karagwe kutasaidia kuendeleza na kupanua mtandao wa hifadhi nchini na kuongeza wigo na manufaa ya utalii katika Ukanda wa Kaskazini Magharibi na mapato ya utalii nchini.

Tayari wawekezaji sita wameonyesha nia ya uwekezaji wa kitalii katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato.

WAZIRI MALIASILI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, alisema Tanzania inatarajiwa kupokea faru 10 kutoka nje ya nchi ili kuongeza idadi ya faru waliopo nchini.

Alisema mpaka sasa wameanza kuhamishia wanyamapori katika hifadhi hiyo ili kuiongezea wanyama kutokana na eneo hilo awali kuwa na historia ya uwindaji.

“Kuhamisha wanyama ni kawaida kwa uhifadhi, kuna watu walipiga kelele bila kujua historia kwani tumekuwa tukisafirisha wanyama pia kutoka nje kuja nchini.

“Mwaka huu tutapokea faru 10 kutoka nje ya nchi kuja kuongeza faru wetu waliopo nchini, hata eneo hili (Burigi) nalo lilikuwa na faru ila walitoweka,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema chini ya mfumo mpya wa Jeshi Usu, linalosimamia uhifadhi na misitu watahakikisha unakuwa chachu ya utendaji kazi, ujasiri, nidhamu na ukakamavu wa hali ya juu.

Alisema TANAPA pia wameanza kujenga hoteli za nyota tatu ambapo itakayojengwa katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi itakuwa na uwezo wa kulaza wageni 60, Hifadhi ya Taifa Rubondo (wageni 24) na eneo la mji wa Chato itakayolaza wageni 100.

Pia kutajengwa hosteli zitakazochukua wageni 80 kwa wakati mmoja katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi.

“Tunajenga kilomita 600 za barabara katika Hifadhi ya Burigi zitakazotumika kutazama wanyama na mizunguko katika hifadhi hiyo, pia kilomita 150 za barabara zitajengwa katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo,” alisema.

Waziri Kigwangalla alisema pia tayari wameanzisha utalii wa fukwe Ziwa Victoria na kunajengwa kivuko kitakachokuwa na uwezo wa kupakia magari kati ya manne hadi sita na abiria 100.

Kupitia sherehe hizo Dk. Kigwangalla alimkabidhi Rais Magufuli tuzo ya hifadhi bora ya Serengeti na tuzo ya kivutio bora ya Mlima Kilimanjaro.

RC GEITA, DK. KALEMANI

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel, alisema Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato ni mgodi mwingine katika mkoa huo baada ya kuwa na migodi ya dhahabu.

“Kuanzisha hifadhi hii ni jitihada kubwa za kimapinduzi zilizofanywa na serikali, tutahakikisha tunatunza na kuendeleza ili uchumi wa wananchi na maisha yao yabadilike.

“Mkoa tuna deni kubwa Serikali Kuu imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya utalii hivyo ni wajibu wetu kutumia fursa hizi kuinua uchumi wa taifa,” alisema.

Alisema mkoa huo, unaendelea kuwa na deni la kukaribisha wawekezaji wote katika sekta mbalimbali ambapo aliahidi kuondoa urasimu.

“Ofisi yangu ipo tayari,Geita imeiva kwa utalii ipo tayari kwa mapinduzi, tunawaomba wawekezaji wasiangukie kwenye mikono ya matapeli,”alisema RC Gabriel.

Naye Waziri wa Nishati na Mbunge wa Chato, Dk. Medard Kalemani, alisema wananchi wamejipanga kutumia fursa hiyo katika biashara ili kukuza uchumi wao na wa nchi.

“Tungewaomba sasa msaidie kutoa elimu ya wanyamapori kwa wananchi, lakini nanyi TANAPA tunawaomba muwe makini dhidi ya wanyamapori na wananchi,” alisema Dk. Kalemani.

MWENYEKITI BODI YA TANAPA

Akizungumza katika sherehe hizo Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA Jeneral Mstaafu George Waitara alisema Hifadhi hiyo na nyingine zitaongeza idadi ya watalii, mapato na kuchangia ukukuaji wa uchumi.

“TANAPA tutahakikisha tunasimamia kikamilifu na kuendeleza maeneo tuliyokabidhiwa,”alisema Jeneral Mstaafu Waitara.

JENERALI WAITARA

Mwenyekiti wa Bodi ya Tanapa, Jeneral mstaafu Mwita Waitara alimshukuru Rais Dk.Magufuli kwa kukubali kutoa idhini kwa Waziri wa Maliasili na Utalii kuwavisha nishani makamishna wa uhifadhi.

Makamishna waliovishwa nishani, ni Kamishna wa Uhifadhi TANAPA,Dk.Allan Kijazi, Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk.Fredy Manongi.

Wengine ni Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Dk.James Wakibara na Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Dos Santos Silayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles