23 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kwaheri wafanyakazi Azam

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

SIMANZI na vilio jana, vilitawala  katika viwanja vya ofisi ya Azam Media, Dar es Salaam, wakati wa kuaga miili ya wafanyakazi watano wa Azam Tv waliofariki dunia kwa ajali mkoani Singida.

Wafanyakazi hao, ni kati ya watu saba waliofariki dunia kwa ajali iliyotokea juzi eneo la Sherui mkoani Singida, wakati wakienda Chato mkoani Geita kwa ajili ya uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi.

Mamia ya wakazi wa Dar es Salaam walianza kufika katika viwanja vya Azam Media, saa 2 asubuhi wakisubiri  kuipokea miili ya wafanyakazi hao.

Ilipofika saa 5:40 asubuhi, msafara wa magari matano yaliyobeba miili hiyo iliwasili katika viwanja hivyo na kupokewa kwa vilio na majonzi.

Gari la kwanza kufika katika eneo hilo, lilikuwa ni la wagonjwa lenye namba za usajili T337 DFV, likiwa limebeba mwili wa aliyekuwa mwongozaji wa matangazo, Salimu Mhando.

Baada ya kushushwa mwili huo,lilifuatia na gari  lenye namba za usajili T 609 DNN, likiwa na mwili wa mhandisi mitambo, Silvanus Kasongo na huku ikifuatiwa na gari jingine lenye namba za usajili T507 DPL lililokuwa na mwili wa mpiga picha, Charles Wandwi.

Gari hilo ilifuatiwa na gari jingine lenye namba za usajili  T452 DLJ lililokuwa limebeba mwili wa aliyekuwa mhandisi sauti, Florence Ndibalema na la mwisho lenye namba T 345 DFV, lilikuwa na mwili wa aliyekuwa mpigapicha, Said Hajj.

Dua ilisomwa na Sheikh Nurdin Kishki kwa upande wa Waislamu na kwa upande wa wakristo maombi yaliongozwa na Padre Steven Siwa.

DEREVA MBARONI

Akitoa salamu za rambirambi kwa familia na wafanyakazi wa Azam Media, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani,Mhandisi Hamad Masauni alisema wamemkamata dereva wa lori aliyesababisha ajali hiyo.

Alisema tayari wameanza uchunguzi wa tukio hilo kwa kuwashirikisha mashuhuda waliopo eneo hilo.

“Tumeanza uchunguzi wa ajali hii na tayari tunamshikilia dereva wa lori na kwa kushirikiana na mashuhuda tutajua sababu za kutokea kwa ajali hiyo,” alisema Masauni.

Aliwataka wananchi kuendelea kutii sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazozuilika.

“Tutaendelea kusimamia sheria za usalama barabarani si kwa kumkomoa mtu, bali kuhakikisha watumiaji wote wanakuwa salama,”alisema Masauni.

ONYO WANAOPIGA PICHA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alitoa onyo kwa wanaopiga picha za watu waliopoteza maisha katika ajali na kuzisambaza mitandaoni.

“Watanzania nawaomba sana tuendekeze tabia yetu ya utu bila hata ya kutumia sheria, ndugu zetu wanapopata ajali pamoja na kwamba kila mtu sasa hivi ana uwezo wa kununua simu nawaombeni sana achene tabia ya kupiga picha na kurusha mitandaoni, hufikirii kuwa hao unaowapiga picha wana ndugu, marafiki na watoto.

“Sheria inazuia na tutakufunga na nafikiri hili ni onyo la mwisho, sheria iko wazi na hatutaongea tena. Tutaanza kuchukua hatua kwa wanaofanya vitendo hivyo,”alisema Dk. Mwakyembe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media, Tido Mhando alisema miili ya marehemu hao itafanyiwa maziko sehemu tofauti kulingana na walikotoka.

“Salimu Mhando anazikwa leo(jana) saa 7 mchana katika makaburi ya Sweetcorner,Dar es Salaam, Charles Wandwi atazikwa kesho(leo) katika makaburi ya Sinza, Dar es Salaam, Said Hajj anasafirishwa kwenda Hale mkoani Tanga,”alisema Mhando.

Alisema upande wa mwili wa Silvanus Kasongo, utasafirishwa kwenda Iringa na mwili wa Florence Ndibalema utasafirishwa kwenda mkoani Kagera kwa maziko.

MAJERUHI

Akizungumzia hali za majeruhi, Tido alisema wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa  Arusha.

“Majeruhiwa  Artus Masawe, Mohammed Mwinshehe na Mohammed Mainde walisafirishwa kwa ndege ya Shirika la  Hifadhi za Taifa(TANAPA) hadi Arusha kwa matibabu,” alisema Mhando.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa zote za msiba wa vijana hao ambao wameondoka wakiwa na umri mdogo.

“Nchi nzima imeingia kwenye majonzi, chama chetu tunaungana na familia za marehemu, wafanyakazi, na menejimenti ya Azam na Watanzania wenzetu kuomboleza na kuwaombea maisha mema na roho zao zikapumzishwe pema peponi,”alisema Mbowe.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema:“Kwa niaba ya uongozi wa chama tunatoa pole kwa tasnia nzima ya habari lakini kwa upekee kwa Azam Media kwa msiba huu mkubwa.

“Tunashiriki misiba lakini pahala pamoja kupotelewa na wafanyakazi watano ni msiba mkubwa, hii ni ajali kwa kweli ni tukio ambalo limetugusa sana, wakuu wa chama walishtushwa na ajali iliyochukua vijana wetu. Chama kinatoa pole nyingi kwa wote walioguswa na msiba huu,”alisema Polepole.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema msiba huo mzito na pigo kubwa kwa chombo cha habari na taasisi moja kuondokewa na watu watano kwa mpigo.

“Ni pengo kubwa kwa sababu utaalamu pia umepotea, hata unaona kitengo cha uzalishaji cha Azam kilikuwa na ubora mkubwa kwa sababu ya utaalamu huu ambao umeondoka lwa pamoja, tunawapa pole,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliwataka wanahabari kufanya kazi kwa utaalam ili kuwaenzi wafanyakazi hao.

“Tunawapa pole familia, Azam Media na Watanzania wote, ni jambo linalouma sana lakini ni uamuzi wa Mungu inabidi tuukubali. Kilichobakia ni kuendelea kuwaombea na kuwaenzi,”alisema Profesa Lipumba.

MARAFIKI

James Ngazi, rafiki wa Mhando alisema alikuwa mtu mwenye nidhamu katika kazi na alikuwa anapenda kujisifia kuwa amefanya kazi nzuri kabla ya kusifiwa.

“Mhando alikuwa mkali katika kazi, mkweli na hamtaelewana kama utaharibu kazi yake, alikuwa kiongozi kwetu na tumejifunza mengi kutoka kwake,”alisema Ngazi.

Hashimu Igwe alimzungumzia Ndibalema, kuwa ilikuwa ni rahisi kwa mtu ambaye hajamzoea kuhisi kuwa ana kiburi, jeuri kutokana na upole na ukimya wake na kuangalia zaidi mambo yake, lakini tangu amfahamu miaka minne iliyopita alikuwa ni zaidi ya rafiki.

“Mara zote alikuwa mtu ambaye ananishauri katika kile ninachofanya, alikuwa mtu wa kubadilika, kuna siku ataniambia sauti yangu inafaa katika Tv kuliko redio na kuna wakati alisema inafaa katika redio kuliko Tv,”alisema Igwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles