25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mkulo:Tuliomba mkopo wa awamu mbili

Na KULWA MZEE- DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo amedai akiwa madarakani hadi anaondoka mkopo walioomba ulikuwa Dola za Marekani milioni 550 na ada ya uwezeshaji ilikuwa asilimia 1.4 na si asilimia 2.4 kama inavyodaiwa.

Mkulo alidai hayo, Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam jana, wakati akitoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Harry Kitilya na wenzake.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hillah mbele ya Jaji Immaculata Banzi, shahidi alidai mkopo walioomba ulikuwa wapewe kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ni Dola za Marekani 250 na awamu ya pili Dola milioni 300.

Alidai mkopo ulikuwa unatoka  benki ya Standard  kwa riba ya asilimia 6.5 na ada ya uwezeshaji ilikuwa asilimia 1.4 ya mkopo huo na ulitakiwa kupatikana mwaka 2012.

“Mchakato ulikuwa haukukamilika,mkopo haukuweza kupatikana, wataalamu walipopitia mapendekezo walishauri mkopo usubiri hadi mwaka mwingine 2012/13.

“Mei 2012 nilistaafu, mwaka 2016 nilikuwa nimeshaondoka Wizara ya Fedha, niliitwa Takukuru wakataka nieleze kuhusiana na mchakato wa mikopo, nikawaeleza.

“Nikiwa PCCB niliulizwa maswali kama nafahamu mchakato wa kuomba mkopo, waliniambia mkopo ulitolewa wa Dola za Marekani milioni 600 kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4.

“Mpaka naondoka wizarani, mchakato wa mkopo ulikuwa haujakamilika sijajua chochote kilichoendelea, niliacha ada ya uwezeshaji ikiwa asilimia 1.4 ya mkopo wote wa Dola za Marekani milioni 550,”alidai.

Mkulo anadai tofauti na washauri wa Serikali katika mchakato wa mkopo, hakukuwa na mshauri mwingine kutoka nje.

Shahidi huyo alimaliza kutoa ushahidi wake na mahakama hiyo awali ilikubali kupokea kielelezo cha barua ya mapendekezo ya mkopo  kutoka Standard Benki ambayo aliweka maelekezo ndani yake akiwa waziri.

Mawakili wengine wa Jamhuri ni Wakili Serikali Mkuu, Osward Tibabyekomya, Hashim Ngole huku upande wa utetezi, Wakili Do Masumbuko Lamwai, Majura Magafu, Jeremiah Mtobesya, Zahra Sanare, Mwanaidi Maajaa, Godwin Nyaisa na Charles Alex.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba nne ya mwaka 2019 ni mshindi wa Mashindano ya Urembo (Miss Tanzania), mwaka 1996, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon, ambao walikuwa maafisa wa Benki ya Stanbic.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles