33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli atibua nyongo Z’bar

MAGUFULI1*CUF  wadai kauli yake imedhihirisha Z’bar ni koloni

*Ulimi wamponza Jaji Makungu,Zitto apinga uchaguzi

Na Waandishi Wetu, Zanzibar/Dar

SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kusema hana mamlaka ya kuingilia Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF), kimeibuka na kusema  kiongozi huyo amedhihirisha kuwa visiwa hivyo ni koloni la Tanganyika.

Chama hicho kimesema Rais Dk. Magufuli, ameshindwa kusimamia kauli yake aliyoitoa Novemba 20, mwaka jana wakati akituhubia Bunge la 11 mjini Dodoma, juu ya nia yake ya kuupatia ufumbuzi mgogoro  wa kisiasa wa Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari  mjini Unguja jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF- Zanzibar, Nassoro Mazrui, alisema wakati wote wa mgogoro huo walimwomba Rais Dk. Magufuli kutekeleza kauli yake kwa vitendo  na si vinginevyo.

Alisema kitendo cha Rais kusema hana mamlaka ya kuingilia suala la Zanzibar, ni wazi sasa kiongozi huyo amekuwa mtu wa kugeuka na aliyeshindwa kusimamia kauli zake.

“CUF tumeshangazwa mno                                                                                              na kauli ya Rais Magufuli ambaye badala ya kuzungumzia tatizo anasema hana mamlaka ya kuingilia ZEC, huku akitambia vyombo vya dola kwa watakaovuruga amani ya nchi.

“…ni wazi ameonekana na hata kudhihirisha kwamba kauli yake bwana mkubwa, Zanzibar ni koloni la Tanganyika. Matatizo ya Zanzibar hayawezi kumalizika kinyume cha matakwa ya mtawala,” alisema Mazrui.

Alisema kutokana na kauli hiyo ya Rais Magufuli ni vema wananchi wakatafakari, huku akishangazwa na uamuzi wake wa kumwagiza Waziri wa Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Kikanda, Balozi Dk. Augustino Maiga kwenda kusuluhisha mgogoro wa Burundi, wakati Zanzibar ikimshinda.

“Inashangaza sana eti Jakaya Kikwete (Rais mstaafu) anakwenda Libya mara Comoro kusuluhisha huku Zanzibar ikiwashinda ni jambo la kusikitisha sana,” alisema

Kutorudia uchaguzi

Alisema pamoja na mambo yanayoendelea sasa, bado CUF inaendelea kusimamia msimamo wake wa kutorudi kwenye uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.

“Tunasisitiza CUF tutaendelea kupigania haki yetu hadi dakika ya mwisho nasi tunawaambia wananchi ambao ndio waamuzi waelewe hivyo, tunawaomba watulie  tayari walishafanya uamuzi Oktoba 25, mwaka jana kupitia sanduku la kura na matokeo kutangazwa.

“Na tunasema haya hatutanii hata kidogo CUF tumeandika barua kwa ZEC ya kujitoa na Maalim Seif ambaye ndiyo alikuwa mgombea wetu naye ameandika barua pia ya kuondolewa kwa jina lake kwenye karatasi ya ZEC.

“ZEC wamegoma kutoa jina lakini tunasema hapa hata Maalim achaguliwe kwa asilimia 99 hatokwenda kuapa ila ataendelea kusimamia uamuzi wa chama wa kutoutambua uchaguzi huo wa marudio,” alisema.

Jaji Makungu ashukiwa

Kutokana na kauli ya Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, aliyoitoa wiki iliyopita katika kilele cha siku ya sheria ikiwemo kushangazwa na madai ya CUF na uwezo wa ZEC kutoingiliwa na chombo chochote, alisema kiongozi huyo wa mhimili wa haki ana nia ovu na maamuzi ya Wazanzibari.

Alisema pamoja na hali hiyo, amekubali kuingia kichwa kichwa kwa ajili ya kutumika kisiasa pamoja na kikundi anachokitumikia.

“Mheshimiwa Jaji Mkuu Makungu, alishajipanga kuikwamisha CUF na wananchi wa Zanzibar katika kudai haki yao kwa njia za amani na za kisheria kwa kutumia sababu za kitaalamu jambo ambalo linakwenda kinyume na misingi ya haki.

“Kwa sababu zote hizo zilizoelezwa CUF kinatamka wazi rasmi kwamba kinapinga na kulaani kitendo cha fedheha na cha kukiuka maadili alichofanya Jaji Makungu. Tunawaomba wale wanaoheshimu utawala wa sheria na misingi ya haki walaani kitendo hicho.

“… tunamwomba Jaji Makungu awaombe radhi hadharani wananchi wa Zanzibar kwa kukhalifu imani yao juu yake binafsi na mhimili wa mahakama,” alisema Mazrui.

Alisema kutokana na kitendo hicho, CUF haioni sababu na imeishiwa na imani na mahakama na itawashauri wanawake wake na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wateule waliokuwa na nia ya kupeleka shauri mahakamani kuacha kufanya hivyo, kwani tayari Jaji Makungu ameshaandaa hukumu na kuisoma hadharani.

“…hata kabla ya shauri kufunguliwa, kusikiliza hoja ya kisheria na ushahidi,” alisema.

ACT-Wazalendo

Akisoma uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho ilikutana jijini Dar es Salaam juzi, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema chama hicho kimepokea na kujadili hali ya kisiasa katika Visiwa vya Zanzibar

“Kamati Kuu imeendelea kusisitiza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, hakuwa na uhalali wa kisiasa, kikatiba na kisheria kufuta uchaguzi huo.

“Dalili zote za kisiasa zinaonyesha Jecha alichukua hatua alizochukua kwa shinikizo au mapenzi ya kisiasa kwa lengo la kuzuia ushindi wa chama kimojawapo ulioelekea kuwa dhahiri,” alisem Zitto

Alisema pamoja na hali hiyo, CC imezingatia mbali na CCM waangalizi wote wa uchaguzi wa ndani na nje, pamoja na  jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki, wametamka bayana  uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika katika mazingira ya haki, huru na demokrasia na matokeo ya uchaguzi huo yalizingatia utashi na matakwa ya wapiga kura wa Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles