32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, February 2, 2023

Contact us: [email protected]

Jaji Ramadhani apasua jipu urais CCM

jaji agustino ramadhani*Asema haki haikutendeka katika mchakato wa kupata mgombea 2015

*Akerwa polisi kuingia bungeni,amkwepa Dk.Magufuli

Na Elizabeth Hombo, aliyekuwa Arusha

JAJI Mkuu mstaafu  wa Tanzania, Augustino Ramadhani amesema utaratibu uliotumiwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) wa kukata majina yao katika uteuzi wa urais haukuwa wa haki.

Amesema hakupata nafasi ya jina lake kuchekechwa katika uteuzi huo, bali kalamu ilipita na majina yao yakakatwa.

Amesema amepanga kwenda kuonana na uongozi wa juu hivi karibuni, kutokana na kile alichosema hakubaliani na baadhi mambo ndani ya chama hicho tawala,

Jaji Ramadhani ambaye alikuwa miongoni mwa wagombea waliosaka tiketi ya urais kupitia CCM, sasa anaungana na waliokuwa wagombea wenzake kukosoa mchakato huo wa ndani ya chama.

Jaji Ramadhani anaungana na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa  Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye na Profesa Mark Mwandosya ambao walitoka hadharani na kueleza kutoridhishwa na mchakato huo.

Jaji Ramadhani ambaye hivi sasa ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na MTANZANIA yaliyofanyika ofisini kwake jijini Arusha juzi.

“Sikupata hata nafasi ya jina langu kuchekechwa kwenye mchakato wa uteuzi wa urais ndani ya CCM… kalamu ilipitia tu majina yetu yakaondolewa na tulitumia busara mno kukaa kimya,”alisema Jaji Ramadhani.

Sababu za kuchukua fomu

Akizungumzia sababu zilizomsukuma achukue fomu ya kugombea urais, Jaji Ramadhan alisema alitegemea  rais wa awamu tano angetoka Zanzibar, baada ya Bara kuongoza kwa awamu mbili mfululizo.

Alisema sababu nyingine ni kutokana na dhuluma nyingi na haki za binadamu kuvunjwa, hivyo aliamini angeleta mabadiliko.

“Niliamini sasa ni zamu ya Zanzibar baada ya Bara kuongoza kwa awamu mbili. Kuna siku nilikutana na Kingunge Ngombale Mwiru kwenye mkutano fulani, nikamwambia kuhusu idadi ya Serikali, yeye anasema kuwa na serikali tatu inavunja Muungano, nikamwambia je kuwa na marais mara tatu mfululizo kutoka upande mmoja haina athari…akanijibu ‘you have a point’ kwa hiyo ndiyo hivyo.

Alipoulizwa kuhusiana na namna alivyoshtua watu wengi pale alipochukua fomu, Jaji Ramadhan alisema hakushtua bali baadhi ya wanasiasa walikuwa wakieneza propaganda chafu, baada ya kuona rekodi yake haina shaka katika uongozi.

“Watanzania hawakushtushwa, wengi walifurahi wakaona sasa wamepata mtu kwa sababu wanajua rekodi yangu katika uongozi, wachache wa kisiasa ndio walikuwa wanaeneza propaganda chafu kwa sababu wananiogopa.

“Miongoni mwao ni mwanahabari mmoja (anamtaja jina)naye alikuwa akiandika habari za kunichafua kuwa inakuwaje jaji awe ndani ya chama cha siasa na agombee urais, lakini nilimpigia nikamwonya,”alisema Jaji Ramadhani.

Kada CCM

Jaji Ramadhan ambaye pia ni askari mstaafu wa  Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye cheo cha  Brigedia Jenerali, alisema tangu alipostaafu ujaji alikuwa mwanachama wa CCM hadi sasa.

“Mimi ni mwanachama wa CCM,  kuna mambo ambayo sikubaliani nayo na hayako sawasawa ndani ya chama, nimepanga kwenda kuonana na uongozi wa chama kuwashauri,”alisema.

Amkwepa Rais Magufuli

Alipotakiwa na gazeti hili kutoa maoni yake kuhusiana na kasi ya Rais Dk. John Magufuli, Jaji Ramadhan alisema anamtakia kila heri.

BUNGE LA 11

Akizungumzia kuhusu mwenendo wa Bunge la 11, Jaji Ramadhani alieleza kusikitishwa kwake kwa kitendo cha polisi kuingia ndani ya Bunge na kuwatoa nje wabunge.

“Kwanza sijafuatilia sana… kitendo cha polisi kuingia ndani ya Bunge si sawa kabisa. Mimi pamoja na ujaji wangu kuna mipaka ya kuingia bungeni, hatuingii ovyo ovyo.

“Kuna askari wa Bunge pale, kwanini polisi waingie bungeni…huku ni kuvunja heshima za taasisi zetu si sawa kabisa,”alisema.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles