24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli asaka vinara ufisadi wa mabilioni

0D6A2900*Awataka waliohusika na kashfa ya Sh trilioni 1.3 watoe ushirikiano

* aliyekuwa bosi TRA, Harry Kitilya, mtoto wa Waziri wahusushwa

 

Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

SIKU moja baada ya Mahakama ya London, Uingereza kubaini ufisadi wa Sh trilioni 1.3, zilizotokana na mkopo uliotolewa na benki ya Standard ya Uingereza kwa Serikali ya Tanzania, Ikulu imeanza kusaka watu waliosababisha hasara hiyo.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema licha ya mahakama hiyo kuamuru Serikali ya Tanzania ilipwe dola za Marekani milioni saba (Sh bilioni 15) baada ya kubainika kuwapo kwa udanganyifu, vyombo vya uchunguzi nchini vitafuatilia suala hilo na kuwafikisha wahusika mahakamani wakibainika na makosa.

Alisema fedha hizo zinazotakiwa kurudishwa nchini ni asilimia moja ya mkopo huo ambao ulikuwa ni dola za Marekani milioni 600 (Sh bilioni 947.67) zilizokopwa na Serikali kwenye bajeti ya mwaka 2012/13 ambazo zilikuwa zilipwe hadi mwaka 2019.

Balozi Sefue alisema baada ya kesi kufunguliwa kwenye mahakama hiyo na Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO), ilibainika kwamba asilimia moja ya mkopo huo ambayo ni dola milioni 6, zililipwa kwa kampuni ya Kitanzania ya EGMA ambayo inamilikiwa na Harry Kitilya, ambaye wakati huo alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Alisema mmiliki mwingine wa kampuni hiyo ni Gasper Njuu na aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Soko la Mitaji ya Umma Tanzania, Dk. Fratern Mboya ambaye sasa ni marehemu.

“Baada ya uchunguzi kufanyika, ikabainika kwamba ile benki ya Uingereza ilitaka tulipe mkopo ule na riba ya asilimia 1.4, lakini ilivyokuja kwa Stanbic Tanzania wao wakasema tulipe asilimia 2.4 na hii asilimia moja akalipwa EGMA.

“Benki ya Uingereza haikusema kwamba inataka mtu wa kati (EGMA), wala Serikali ya Tanzania haikusema kwamba inataka mtu wa kati, lakini pia hizi fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya hii kampuni ziliingia na ndani ya siku chache zikatolewa zote.

“Sasa inatakiwa Standard Bank wailipe Tanzania dola milioni sita iliyolipwa kimakosa kutokana na ongezeko la hiyo asilimia moja na riba ya milioni moja, jumla inakuwa dola milioni saba ambayo ni sawa na Sh bilioni 15,” alisema balozi Sefue.

 

UINGEREZA IMEONYESHA NJIA

Balozi Sefue alisema Serikali ya Uingereza na SFO, zimeonyesha njia katika kusaidia nchi masikini zinazodhulumiwa na wapokea rushwa na watoa rushwa.

“Zipo nchi nyingine tajiri ambazo wanapigia kelele rushwa kwa kuangalia upande wa mpokeaji tu, na kusahau makampuni makubwa kutoka kwao yanayopenda kuhonga watu wetu,” alisema.

Alisema pia kuwa Rais Dk. John Magufuli, ametoa wito kwa wamiliki wa Kampuni ya EGMA kutoa ushirikiano kwa vyombo vya uchunguzi ili kubaini nani aliyelipwa dola milioni sita na kwa ajili ya nini.

Balozi Sefue pia alisema wachunguzi hao wataangalia suala la utakatishaji fedha chafu kutokana na fedha hizo kuingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo na siku chache baadaye kutolewa.

Alisema suala la kodi za Serikali kama zipo ambazo hazikulipwa pia litaangaliwa.

 

MWANZO WA KUBAINIKA

Balozi Sefue alisema mwaka 2013, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) walikagua benki ya Stanbic Tanzania na kubaini  malipo yasiyokuwa ya kawaida kwa kampuni ya EGMA.

“Malipo hayo yalikuwa kinyume na taratibu za kibenki, na baadhi ya watumishi wa Stanbic Bank (T) walishindwa kuvumilia hali hiyo. Wakaguzi wa Benki Kuu walifuatilia malalamiko hayo na kujiridhisha kuwa uongozi wa Stanbic ulifanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu zinazokubalika kibenki.

“Fedha kiasi cha dola milioni 6 ziliingizwa kwenye akaunti ya EGMA na siku chache baadaye zilitolewa zote kwa fedha taslimu na wala benki haikukusanya kodi ya zuio (withholding tax) kwa mujibu wa sheria ya mapato ya kodi ya mwaka 2004 kutokana na mapato ya Standard Bank kwa kazi ya ushauri iliyoifanya.

“Kama ulivyo utaratibu, Benki Kuu ilitoa taarifa ya ukaguzi kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Stanbic Tanzania na kuitaka kuchukua hatua za kurekebisha kasoro ndani ya benki, pamoja na kutoa taarifa kwa Financial Intelligence Unit kuhusu miamala yenye mashaka kwenye akaunti ya EGMA kwa mujibu wa Sheria ya Anti-Money Laundering Act 2006,” alisema Balozi Sefue.

Alisema bodi ya Standard Bank iliona makosa yaliyobainishwa na wakaguzi wa BoT yalistahili kutolewa taarifa kwa SFO nchini Uingereza, ambao walianzisha uchunguzi ambao hatimaye ulisababisha kesi kufunguliwa.

 

UDANGANYIFU ULIVYOFANYIKA

Balozi Sefue alisema kwa taarifa zilizopo, inaelekea kuwa Standard Bank ilipanga kutoza ada ya asilimia 1.4 tu, yaani dola za Marekani 8,400,000 kwenye mkopo huo.

“Lakini ukafanyika ujanja wa kudai kuwa ati anahitajika local agent (mtu wa kati kutoka nchini) wa benki hiyo, ambaye naye alipwe asilimia 1 nyingine, na kufikisha ada yote kuwa asilimia 2.4, dola za Marekani 14,400,000.

Local agent huyo alikuwa Kampuni ya EGMA, ambayo miamala yao kuhusu dola za Marekani 6,000,000 walizochukua, ndiyo ilishtua wakaguzi wa BoT na taarifa kutolewa kwa Bodi ya Stanbic Tanzania na hatimaye Standard Bank, SFO na Mahakama Uingereza,” alisema.

 

Hukumu

“Novemba 30, mahakama jijini London iliitoza benki ya Standard dola za Marekani milioni 32.2. Kati ya fedha hizo, dola milioni 16.8 ni faini inayolipwa kwa SFO, dola milioni 8.4 ni “disgorgement of profits”; na dola milioni saba ndizo inazolipwa Serikali ya Tanzania,” alisema Sefue.

 

UTATA

Baada ya Balozi Sefue kuzungumza na waandishi wa habari, MTANZANIA ilitaka kujua ni hatua gani zitakazochukuliwa kwa watumishi wa Wizara ya Fedha, BoT, TRA na wengine wa umma waliohusika kutafuta mkopo huo uliobainika kuwa na kosoro.

Balozi Sefue alisema mchakato wa kupata mkopo huo haukuwa na makosa, lakini tatizo lilikuja kuibuka kwenye riba na kutafuta kampuni ya kati.

“Suala hili linaibua maswali kadhaa, ambayo bado Watanzania wengi hawajapata majibu yake,” alisema.

Pia gazeti hili lilitaka kujua kama Serikali ipo tayari kuiweka benki ya Stanbic Tanzania kwenye taasisi zinazotakatisha fedha kutokana na kashfa hii na ile ya Escrow.

Bunge la 10 lilipendekeza benki hiyo ijumuishwe kwenye taasisi zinazotakatisha fedha haramu baada ya kubainika kuwa watu walichukua mabilioni ya fedha za Escrow kwa tasilimu kwenye benki hio kinyume cha sheria.

Kuhusu hilo, Sefue alisema kuwa uchunguzi utakaofanywa utaonyesha kama kuna haja ya kuijumuisha benki hiyo kwenye taasisi zinazotumika kutakatisha fedha chafu.

 

MTOTO WA WAZIRI

Mwenendo wa kesi hiyo iliyotolewa hukumu juzi, unaonyesha kuwa benki ya

Stanbic Tanzania ilitumia muda mrefu kuhakikisha inapata tenda ya kutafuta mkopo huo, na wakati mchakato huo ukiendelea yalitokea mabadiliko ya waziri kwenye Wizara ya Fedha.

Kwamba Julai 2012, Stanbic Tanzania ilimwajiri mtoto wa waziri mpya wa fedha ambaye hakutajwa, na ilipofika Agosti 29 mwaka huo, benki hiyo iliandika barua pepe kwenda Standard Bank ikisema kuwa imefanya mazungumzo mazuri sana na waziri wa fedha pamoja na timu yake ya ufundi.

Mwenendo wa kesi hiyo unasema kuwa Septemba 4, mwaka huo, Stanbic ilimtuma mtoto huyo wa waziri kwenda Wizara ya Fedha kupeleka nyaraka za dokezo la mkopo huo lililoonyesha riba yote ya asilimia 2.4 jambo ambalo mtoto huyo alilifanya siku iliyofuata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles