27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mgogoro Zanzibar waitisha CCM

Pg 2 DEC 2*Yaunga mkono juhudi za Dk. Magufuli

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar unaitia doa Tanzania kwenye uso wa kimataifa, licha ya kwamba Serikali ya awamu ya tano imeanza kutekeleza vizuri majukumu yake.

Nape ambaye jana alitembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd zilizopo Sinza Kijiweni jijini Dar es Salaam, alisema kinachofanywa na Rais Dk. John Magufuli kwa sasa ni utekelezaji wa ilani ya CCM na chama hicho kinamuunga mkono kwa asilimia 100.

 

ZANZIBAR

Alipoulizwa mtazamo wake juu ya hali ya kisiasa ya Zanzibar, Nape alisema: “Zanzibar ni kati ya mambo yanayotia doa mwanzo mzuri wa awamu ya tano kwa sababu ni jambo linalosemwa nje na ndani ya nchi.”

Alisema wanaoweza kubadilisha hali ya mambo visiwani humo ni Wazanzibari wenyewe kwa kushirikiana na Rais Magufuli pamoja na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete.

Nape alisema watu kutoka nje ambao aliwaita ‘upande wa tatu’ hawataweza kusaidia kumalizika kwa mgogoro huo, licha ya kwamba wangetaka kuwa sehemu ya ushiriki wa usuluhishi wake.

Alisema hadi sasa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, wameshakutana mara kadhaa kujadili jambo hilo, hivyo anadhani ni vyema wakamaliza mapema.

“CCM kama CCM hatuamini kwamba ‘third party’ (upande wa tatu) inahitajika, kulikuwa na mgogoro mwaka 2001 wakaingia, lakini wakashindwa. Wazanzibari wenyewe watalimaliza hili, na mimi nadhani linataka limalizike mapema sana tena kwa amani,” alisema Nape.

Akizungumzia uhalali wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo wa Zanzibar, Nape alisema kisheria suala hilo halina tatizo isipokuwa mjadala huo unaweza kuwa na utata kwenye uhalali wa kisiasa.

Alisema kama suala hilo lisingekuwa na uhalali kisheria, kwa sasa kungekuwa na watu wapo mahakamani kupinga mchakato huo, na wangeweka wazi sheria iliyovunjwa kwa hatua iliyofikiwa hadi uchaguzi huo kufutwa.

“Kwakuwa hakuna sheria iliyovunjwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), mpaka sasa hakuna mtu aliyesema waziwazi ni sheria ipi iliyovunjwa na tume hiyo.

“Sasa hapa labda tuseme suala la uhalali wa kisiasa na huko sitaki kwenda kwa sababu itaonekana nakitetea chama changu, naomba tubaki hapa kwamba suala hilo lina uhalali wa kisheria,” alisema Nape.

 

KASI YA MAGUFULI

Kuhusu kasi aliyoanza nayo Dk. Magufuli, Nape alisema huo ni utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo waliinadi kwa wananchi.

Akitolea mfano, alisema maadhimisho mbalimbali ambayo huchukua fedha nyingi za Serikali bila sababu yalikuwa yakisemwa hata na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

“Kinana alisema sana mambo haya, kwahiyo kinachofanyika ni utekelezaji wa ilani ya CCM, ilani hii ni mwongozo na anachofanya mkuu huyo wa nchi ni kufikia lengo la mwongozo huo,” alisema Nape.

Nape aliongeza kuwa suala hilo linajaribu kukuzwa na wapinzani wao ili kumtenga rais na chama chake.

“Wasiofahamu wanatafsiri kwamba huenda imewatisha baadhi ya vigogo wa CCM, na kwamba huenda hatumuungi mkono Rais Magufuli, hili si kweli.

“Kuna watu wanajaribu kutenganisha CCM na rais kwa sababu wanataka kukizamisha chama, ukiangalia suala la kuimairisha ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi ambayo ndiyo yanayofanyika sasa, yote yapo kwenye ilani.

“Ilani iliweka lengo yeye ndiye anatafuta njia za kulikifia na chama kinamuunga mkono kabisa, kwa sababu tunataka tuitekeleze ilani kwa kiasi kikubwa tofauti na miaka ya nyuma,” alisema Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles