KADIRI miaka inavyosonga mbele, ndivyo ambavyo pia maradhi mapya huibuka, kama yalikuwapo tangu zamani, basi wakati huo hayakuwa yakifahamika au hayakuwa tishio kwa afya ya jamii.
Magonjwa haya miongoni mwao ni yale yanayoambukizwa kutokana na kujamiiana, au kwa maneno mengine kushiriki ngono.
Zamani, nchini Tanzania magonjwa hayo yalikuwa yakiitwa ya zinaa, lakini siku hizi yanaitwa ya ngono.
Jina limebadilika ili kuondoa hali ya kuhukumu wagonjwa kuwa wamezini na kuambukizwa maradhi ilhali kuna wengine hawakuhusika.
Mabadiliko yamekubalika kutokana na baadhi ya waathirika kupata maradhi bila kushiriki tendo la kujamiiana bali kuambukizwa pengine kutokana na mchakato wa uzazi, kuongezewa damu na hata kubakwa.
Maradhi haya, ambayo yana neno la kitaalamu lenye ufupisho wa STI, yakimaanisha ugonjwa unaoambukizwa kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya kujamiiana.
Njia hizo ni pamoja na kufanya ngono na wenza wa jinsi moja na wengine kwa njia ya mdomo. Kuna aina zaidi ya 20 ya magonjwa haya, ambayo yana au hayana dalili zinazoonekana iwe kwa macho au kuhisi maumivu.
Ukiondoa maradhi haya yanayofahamika zaidi katika jamii kama vile kisonono, kaswende, Ukimwi, vipele (HSV), Chlamydia, papiloma, gonorrhea na mengineyo, kumeibuka mengine manne, yanayowaumiza kichwa wataalamu na hivyo kuwa tishio jipya la afya ya jamii.
Neisseria meningitides
Neisseria meningitidis, pia hufahamika kwa jina la kitaalamu meningococcus, ambayo husababisha uvimbe hatari wa tando za uti wa mgongo na ubongo.
Lakini, bakteria huyo sasa anapata umaarufu zaidi kwa kusababisha maambukizi kwenye maungo ya uzazi.
Utafiti mmoja uliofanywa katika miaka ya 1970 ulibainisha ni kwa namna gani dume moja la sokwe alihamisha bakteria hao hatari kutoka mdomoni na puani kwenda kwenye uume wake baada ya kujilamba sehemu zake nyeti.
“Mnyama huyu, yaani sokwe mara kwa mara hujilamba uume wake,” waandishi wa utafiti huo wanabaini.
Kwa mujibu wa utafiti, takribani asilimia 10 ya watu wazima wana bakteria aina ya Neisseria katika makoo na pua zao. Tafiti zinabainisha kuwa wanaweza kuhamisha bakteria hao kupitia mabusu makali yanayohusisha ndimi, ama kunyonya sehemu za siri za watu ambao hawana bakteria hao.
Hata hivyo, watafiti hao hawana uhakika ni kwanini bakteria hao wamesambaa kwa kasi na kuzua ugonjwa hatari kwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsi moja barani Ulaya, nchini Marekani na Canada.
Utafiti mmoja uliofanywa juu ya uwasho mkali wa mrija wa kupitisha mkojo kutoka kwenye kibofu unaosababishwa na bakteria huyo, ulibaini kuwa wanaume walipata maambukizi hayo kupitia ngono iliyohusisha mdomo.
Wanasayansi wanaamini kuwa, maambukizi makali ya bakteria huyo yaliyokumba kwa nguvu miji kadhaa ya Marekani mwaka 2015 yalichochewa na vinasaba vya karibu vya bakteria wa familia moja, Neisseria gonorrhoeae, ambaye husababisha ugonjwa mwingine wa zinaa wa kisonono.
Ukaribu wa bakteria hawa ulisababisha kusambaa kwa haraka kwa maambukizi hayo hatari.
Kuna aina tano ya bakteria hatari wa Neisseria Meningitidis duniani, lakini kwa bahati nzuri kuna chanjo za aina mbili zinazopatikana na zinakinga dhidi ya aina zote za bakteria wa aina hiyo.
Mycoplasma genitalium
Mycoplasma genitalium, moja ya bakteria wadogo zaidi wanaofahamika, wanapata umaarufu mkubwa zaidi ya maumbo yao kwa kusababisha maambukizi hatari ya ugonjwa unaotokana na zinaa.
Bakteria huyo aligunduliwa miaka ya 1980, na leo hii anaambukiza asilimia moja hadi mbili ya watu hususani vijana.
Maambukizi ya Mycoplasma genitalium ambayo kwa kawaida hayana dalili, wakati mwingine hufanana na dalili za kisonono na kaswende kwa kuwashwa mfululizo kwa mrija wa mkojo kwa wanaume na mlango wa kizazi kwa wanawake.
Kutokana na kuweza kusababisha maumivu makali ya nyonga kwa wanawake, bakteria huyo anahusishwa pia na kusababisha ugumba, kuharibika kwa mimba, kuzaliwa watoto njiti na hata watoto kufia tumboni mwa mama zao.
Licha ya kwamba kondomu inaweza kuzuia maambukizi haya, watafiti wanatoa tahadhari juu ya usugu wa bakteria huyo kutibika na dawa za antibaotiki za azithromycin na doxycycline.
Shigella flexneri
Ni maradhi mengine ya zinaa, ambayo husababisha maumivu makali ya tumbo na kuhara damu, ambapo hustawisha kusambaa kwa bakteria hao.
Shigellosis huambukiza kwa kugusa moja kwa moja au kwa njia moja au nyingine kinyesi cha binadamu.
Ijapokuwa ugonjwa huo umekuwa ukionekana zaidi kwa watoto na wasafiri kwenye nchi zenye uchumi mdogo na wa kati, watafiti walianza kupokea kesi za ugonjwa huo kwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja tangu miaka ya 1970.
Ugonjwa huo, wanasayansi wanaamini, umechukua njia mpya ya maambukizi kwa kutumia ngono ya kinyume cha maumbile na ngono kwa njia ya midomo na hivyo kusabisha maambukizi kadhaa ya ugonjwa huo wa ngono kwa miongo minne sasa.
Lymphogranuloma venereum (LGV)
LGV mwanzo hutokea kama kipele ama lengelenge na kisha kushambulia mfumo wa kinga ya mwili na hivyo kusababisha uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Ugonjwa huu pia husababisha maambukizi katika njia ya haja kubwa na kuleta maumivu makali ya tumbo.
Katika miaka 10 iliyopita, kumekuwa na maambukizi makubwa ya LGV barani Ulaya na Amerika ya Kaskazini hususani kwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Kutumia kondomu kunaweza kupunguza uwezekano wa maambukizi, na kutibu ugonjwa huu kunahitaji walau matibabu ya wiki tatu na kunywa antibaotiki kama doxycycline.