WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa onyesho la sanaa la Historia na chimbuko la mwanadamu litakalofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni, jijini Dar es Salaam.
Onyesho hilo limeandaliwa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania, ikishirikiana na Makumbusho ya Akiolojia ya Madrid, nchini Hispania (Regional Archaeological Museum of Madrid) na limetokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika katika maeneo ya Akiolojia na Palentolojia hapa Tanzania.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabula, onyesho hilo litazinduliwa saa tisa mchana na vitu vitakavyoonyeshwa katika onesho hilo vimepatikana nchini.
“Onyesho limegawanyika katika sehemu kuu nne, ikiwemo sehemu ya kwanza inayohusu ushahidi wa nyayo za zamadamu zilizongunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dk. Mary D. Leakey, sehemu ya pili inahusu hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus Homo) ambapo kutakuwa na masalia ya zamadamu wanaoitwa Zinjanthropus au Paranthropus boisei na Homo habilis, sehemu ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus na sehemu ya nne inaonesha kipindi cha mwanzo cha binadamu wa sasa,” alisema Profesa Mabula.