25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mafuriko yahamisha vijiji viwili Sumbawanga

Gurian Adolf -Sumbawanga

WAKAZI 540 wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, wamezikimbia nyumba zao baada ya Ziwa Tanganyika kujaa maji na kusababisha mafuriko katika vijiji viwili vilivyopo katika wilaya za Nkasi na Kalambo.

Walikuwa wakiishi katika nyumba 108 zilizojengwa maeneo ambayo awali maji ya Ziwa Tanganyika yalikuwa yakifika kwenye vijiji vya Kipwa wilayani Kalambo na Kirando wilayani Nkasi ambapo kwa zaidi ya miaka 30 yalikauka na watu hao wakajenga makazi.

Miundombinu mingine iliyofurika maji ni pamoja na mwalo wa samaki na gati katika Kijiji cha Kirando na gati jingine lililopo katika Kijiji cha Kipili wilayani Nkasi.

Soko la kisasa la samaki lililopo katika Kata ya Kasanga wilayani Kalambo nalo limefurika maji na shughuli za kibiashara zimesimama.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura, alisema mafuriko hayo yalikikumba Kijiji cha Kipwa miaka 23 iliyopita wakati wa mvua za El-nino za 2017/18.

“Nyumba zote 90 za Kijiji cha Kipwa zimefurika maji baada ya Ziwa Tanganyika kujaa na kufika yalipokuwa awali, familia za watu 400 hazina makazi, wamepoteza kila kitu walichokuwa wakimiliki, taasisi mbili za umma ambazo majengo yake hayakuathirika ni shule ya msingi na zahanati tu,” alisema Julieth.

Akifafanua zaidi aliongeza kuwa baadhi ya watu wamehifadhiwa katika vyumba vya madarasa ya shule ya msingi huku wengine wakiwa wamekimbilia kwenye maeneo ya miinuko pamoja na milimani.

Hata hivyo amethibitisha kuwa hakuna kifo chochote kilichoripotiwa na bado hasara halisi iliyosababishwa na mafuriko hayo haijafahamika hadi sasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya waathirika wa tukio hilo waliiomba Serikali kuwapatia msaada wa hali na mali ikiwemo makazi ya muda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles