24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAFUNZO UFUNDI STADI NJIA PEKEE KUWAKWAMUA VIJANA

Na FERDNANDA MBAMILA


MAKUNDI maalumu kwenye jamii yetu kama ya watu wenye ulemavu, yatima na waliokosa fursa mbalimbali yana watu muhimu ambao wameendelea kudhihirisha vipaji na uwezo mkubwa wa kutoa mchango katika kujenga uchumi wa Taifa na wa kwao binafsi.

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kama taasisi ya umma yenye dhamana ya uendelezaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini, inaamini kuwa ujuzi kama nyenzo ya msingi kabisa ya kumwezesha mtu kwenda sambamba na wengine katika harakati za kiuchumi ni haki ya kila mtu.

Ujuzi umekuwa ukiwawezesha watu kujiajiri au kuajiriwa mahali popote. Ili kuhakikisha suala hilo linatekelezeka, VETA imekuwa na mikakati mbalimbali yenye lengo la kupanua wigo wa fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa makundi maalumu katika jamii yetu kama anavyofafanua Dk. Bwire Ndazi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA.

“Serikali imekuwa ikiendelea kuhimiza kila mwananchi kushiriki katika shughuli za kujikwamua kiuchumi. Hivyo, tunatambua kuwa ufundi stadi unaweza kuyasaidia makundi maalumu pia katika jamii kama vile wenye ulemavu, walio katika mazingira hatarishi na watu waliokosa fursa wakiwamo wale wanaotoka kaya masikini. Hivyo, katika kutimiza dhamana yake iliyopewa na Serikali, VETA pia imekuwa ikitoa mafunzo maalumu kwa makundi hayo katika vyuo vyake na kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali,” anafafanua.

Dk. Ndazi anafafanua kuwa ili kulitekeleza hilo Serikali kupitia VETA na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikiwajengea uwezo wakufunzi wake na kuboresha miundombinu yake ili kuwezesha utoaji wa mafunzo jumuishi kwa watu wenye ulemavu katika vyuo mbalimbali inavyovimiliki. Pia VETA imekuwa ikiratibu na kusimamia viwango vya utoaji mafunzo katika vyuo binafsi vinavyotoa mafunzo mahsusi kwa watu wenye ulemavu. Miongoni mwa mafunzo ambayo yamegusa hisia za watu wengi ni ya watu wenye ulemavu wa akili katika chuo cha VETA Dar es Salaam, ambapo vijana walioonekana kwamba hawana uwezo kabisa wa kufanya chochote katika jamii, wamedhihirsha kwamba wanaweza kufundishika na kufanya shughuli za kiufundi. Pia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, VETA imeweza kubuni na kutekeleza mipango kadhaa ya mafunzo inayogusa na kuyanufaisha makundi maalumu.

Anaeleza kuwa kutokana na juhudi za kutoa fursa za mafunzo kwa vijana wenye ulemavu, VETA imeweza kuongeza udahili wa vijana wenye ulemavu kwenye mfumo wa mafunzo ya ufundi stadi katika kozi za muda mrefu kutoka 700 mwaka 2010 hadi 1053 mwaka 2015.

“Mafunzo mengine ambayo huwanufaisha vijana wenye mahitaji maalum yamekuwa yakitolewa kwa kozi za muda mfupi mfupi kuanzia wiki chache hadi miezi sita,” anasema.

Anataja baadhi ya miradi iliyolenga makundi hayo kuwa ni: Mpango wa Kuwezesha Vijana Kiuchumi (YEE) kwa kushirikiana na Plan International na mashirika mengine, unaotekelezwa katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Lindi na Mtwara; Mpango wa Kuwafadhili Vijana Kupata Mafunzo ya Ufundi Stadi, Ujasiriamali na Stadi za Maisha kwa kushirikiana na International Youth Foundation (IYF) kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Kigoma, Ruvuma, Mbeya na Mtwara.

Mpango mwingine ni wa Via-Jitengenezee Ajira ulioanzishwa kati ya Shirika la Kimataifa la Vijana (IYF) kwa kushirikiana na VETA na kufadhiliwa na MasterCard Foundation. Mpango huo unalenga kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana walio katika mazingira magumu nchini kwa kuwapatia mafunzo ya stadi za kazi, ujasiriamali na stadi za maisha.

Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2016, mpango huo unatarajia kuwanufaisha vijana waishio katika mazingira magumu 22,550 katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, Dar es Salaam na Morogoro. Hilo litatekelezwa kwa kuwapatia mafunzo na uwezeshaji mwingine ili kuwaweka katika nafasi ya kupata ajira kwa urahisi ama kwa njia ya kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa IYF wa Ukanda wa Afrika, Matthew Breman mafunzo katika fani mahsusi za ufundi stadi yanafanyika kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mtwara, huku Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kikiwajengea wanafunzi wake, ambao ni walimu wa baadaye wa ufundi stadi kuwawezesha kuimarika kitaaluma, kupata mbinu za kutafuta ajira, kujiamini na kuweza kupata mafanikio katika ajira na maisha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Shindani cha Ujasiriamali Tanzania (TECC), Beng’i Mazana Issa anaeleza kuwa vijana watakaonufaika na mpango huo katika mikoa husika watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali ili kuimarisha uendeshaji wa miradi yao ya kiuchumi.

VETA pia imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na IYF katika kutoa mafunzo ya ufundi stadi yanayolenga makundi maalumu. Miongoni mwa programu nyingine zilizotekelezwa kwa ushirikiano ni ule uliojulikana kwa jina la Vijana Wasomi (Youth Scholars)  ambao ulitekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Iringa, Kigoma, Mwanza, Mtwara, Ruvuma, Tanga na Mbeya mwaka 2011 hadi 2015 ambapo uliwanufaisha vijana zaidi ya 300.

Kuhusu mpango wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi – YEE, Dk. Ndazi anaeleza kuwa mradi huo uliotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2017, pia ulilenga kuwawezesha vijana wenye miaka ya kuanzia 15 hadi 35 kutoka katika makundi maalumu kupata ujuzi, hususani mafunzo katika stadi mbalimbali wanazopendelea.

Mradi huo ulitekelezwa katika wilaya tisa za mikoa mitano ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Pwani na Morogoro.

 

“Programu hizo zitasaidia kuchangia juhudi za Serikali kupunguza umaskini na kutowaacha nyuma vijana wengi walio katika maisha duni, wenye ulemavu na makundi mengine yenye changamoto katika jamii,” anasema.

Anafafanua kuwa mafunzo kwa vijana hao wa makundi maalumu yalifanyika kwa namna tatu zikiwamo mafunzo vyuoni, mafunzo kwenye jamii na mafunzo kwa njia ya uanagenzi. Mafunzo ya vyuoni na kwenye jamii yalikuwa ya muda mfupi kuanzia miezi mitatu hadi sita. Wakati wa mafunzo ya uanagenzi vijana waliunganishwa na mafundi wakuu katika jamii zao hivyo kujifunza kwa vitendo katika sehemu za kazi. Mpango huo umewanufaisha moja  kwa moja vijana wapatao 9100 ambao wamejifunza fani mbalimbali zikiwamo ufundi magari, uungaji na uundaji vyuma, ushonaji, useremala, ufundi umeme wa majumbani, upishi na mapambo, uashi, ufundi pikipiki, na udereva.

Dk. Ndazi anaeleza kuwa licha ya mafanikio ya kupata ujuzi wa ufundi stadi, vijana 455 waliweza pia kuunda vikundi vya kuweka na kukopa hivyo kuwa katika fursa nzuri zaidi ya kupata mikopo kwa ajiri ya kuendesha miradi yao ya kiufundi.

Anahitimisha kwa kusema kuwa wakati ambapo VETA inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha makundi yote, hususani yale maalum, yanapata fursa za kutosha za mafunzo ya ufundi stadi, ni vyema wadau mbalimbali nao wakaunga mkono jitihada za Serikali kwa kusaidia makundi maalumu kupata mafunzo ya kuwawezesha kupata ujuzi wa kuajirika na hivyo kuondokana na utegemezi katika jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles