24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maftaha: Sitasahau mizengwe ya Murji Mtwara Mjini

MAFTAH*Asema alivuruga Ukawa Uchaguzi Mkuu

*Adai Bunge la 11 limejaa uvyama kuliko utaifa

NA ELIZABETH HOMBO

PAMOJA na kwamba katika Uchaguzi Mkuu uliopita vyama vikubwa vya upinzani vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, viliungana na kusimamisha mgombea mmoja kwa kila jimbo lakini kwa upande wa Mtwara Mjini hali ilikuwa ni tofauti.

Tofauti hiyo ilitokana na kile kilichodaiwa kuwapo figisufigisu kwa wagombea wa vyama vya Chadema na NCCR-Mageuzi kutumiwa na CCM ili kuvuruga uchaguzi huo.

Vyama hivyo kupitia umoja wao wa Ukawa awali walikubaliana kwa pamoja kumsimamisha mgombea wa CUF, Maftaha Nachuma kugombea Jimbo la Mtwara Mjini, lakini cha kushangaza wagombea wa Chadema na NCCR-Mageuzi waliendelea kufanya kampeni hadi dakika za mwisho.

Lakini pamoja na figisufigisu zote hizo mgombea huyo wa CUF ndiye aliyeshinda na kunyakua jimbo hilo lililokuwa likiongozwa na Hasnen Murji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Gazeti hili limefanya mahojiano na Maftah ambapo pamoja na mambo mengine anasema mchakato wa uchaguzi ulikuwa mgumu kwani mgombea wa CCM aliingilia uchaguzi wao wa ndani ya chama kwa kununua wajumbe huku akivuruga Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jimboni humo. Endelea…

MTANZANIA: Hebu tueleze historia yako kwa ufupi

MAFTAH: Nilihitimu elimu yangu ya msingi mwaka 1999 na baadaye mwaka 2003 nikamaliza kidato cha nne na kidato cha sita nilihitimu mwaka 2006.

Baada ya kuhitimu kidato cha sita nikaenda kusoma course ya ualimu ya mwezi mmoja. Nikapangiwa kufundisha sekondari wakati ule shule za kata ndio zilikuwa zimeanzishwa kwa hiyo hakukuwa na walimu wa kutosha.

Mwaka 2007 nikaenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), nikafanya degree yangu ya kwanza ya Political Science and Public Administration.

Baadaye nilipomaliza nikarudi tena kufundisha, nikateuliwa kuwa Head Master wa Shule ya Sekondari Mchinga kutokana na uwezo wangu na nimekuwa mkuu wa shule mpaka nimeacha kazi mwaka jana.

MTANZANIA: Ni kitu gani kilichokusukuma ukagombea ubunge?

MAFTAH: Kwanza tangu nikiwa shule ya msingi nilikuwa kiongozi wa wanafunzi na hata sekondari hakuna ngazi ya uongozi wa wanafunzi ambayo sijaishika hadi chuo kikuu nilikuwa kiongozi mwandamizi wa serikali ya wanafunzi.

Jambo lingine ambalo lilinisukuma nikagombea ubunge ni kwa vile kusini ni maeneo ambayo yalisahaulika sana katika mambo mengi, mfano ujenzi wa miundombinu na hata zile za huduma za kijamii.

Ukifanya comparison na maeneo mengine utaona Kusini bado tuko nyuma sana hivyo nikasema lazima nije niwakomboe ndugu zangu.

Pia mwaka 2003 kabla sijamaliza kidato cha nne nilikuja bungeni, kulikuwa kuna mashindano ya vijana wanaojua kuongea Kiingereza vizuri katika shule zote za sekondari na yale yalikuwa ya kikanda na nikashinda.

Nikabahatika kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa UN model general assembly hapa bungeni Dodoma na mwaka ule ilifanyika hapa Tanzania katika ule ukumbi wa Msekwa.

Baada ya kupata ushindi huo ndio nikasema kumbe nina uwezo hata wa baadaye kugombea ubunge na nitashinda na nitakuwa na uwezo pia wa kuwatetea watu wangu.

Pia kwa mara ya kwanza mwaka 2005 nikiwa kidato cha sita, kulikuwa kuna uchaguzi nikagombea udiwani na kimsingi nilifanya maajabu sana kata ya pale Mtwara Mjini.

Niliweza kushawishi wananchi wa Mtwara na nilikuwa nikifanya mikutano na watu walikuwa wanajaa kweli kweli.

MTANZANIA: Ilikuwaje ukagombea wakati ukiwa mwanafunzi?

MAFTAH: Kwanza kwenye siasa niliingia nikiwa sekondari kwa sababu nimesoma sheria za uchaguzi na inasema ili ugombee kwanza uwe na akili timamu, ujue kusoma na kuandika zaidi ya hapo hakuna limitation kwamba mwanafunzi asigombee, nikaona hakuna sababu ya mimi kutowakomboa wananchi wa Mtwara.

MTANZANIA: Baadaye ikawaje?

MAFTAH: Ilitokea mizengwe kweli kweli na ukizingatia nilikuwa mdogo wakati ule. Wenzangu walitaka kunikatia rufaa kutokana na umri wangu lakini tuliwashinda.

Nilifanya siasa nikiwa mdogo kabisa na ilikuwa siasa ya Kimapinduzi na isingekuwa chama tawala kunyang’anya ushindi wangu ningepata udiwani.

Mwaka 2010 wakati wa Uchaguzi Mkuu nikagombea ubunge huku nikiwa chuoni na nikashindwa kwenda kwenye kura za maoni kwa sababu nilikuwa kwenye mtihani wa kumaliza chuo, nikatuma fomu zangu kwa fax na ilitembezwa na watu na nikawa wa pili kati ya wagombea watatu. Nikakubaliana na matokeo, nikasema mwaka ujao nitagombea tena ubunge.

Baada ya hapo nikiwa naendelea kufundisha pale Mchinga sekondari nilipoteuliwa kuwa mkuu wa shule, baadaye walimu wakuu wenzangu wakaniteua kuwa mwenyekiti wa wakuu wa shule wilaya.

Pia mbali ya kufundisha nilikuwa najihusisha na michezo nikawa Katibu wa TFF Lindi mpaka sasa. Pia Halmashauri ikanichagua kuwa kama mjumbe wa kamati ya ukaguzi wa shule Wilaya ya Lindi hivyo kutokana na kushika nafasi hizo niliweza kufanya mengi sana.

Mwaka 2014 niliwaeleza pale shuleni kuwa nataka nikagombee ubunge na wakati huo nikashiriki kwenye uchaguzi wa vijiji na tulipata kata nyingi sana.  Badaye nikawapa taarifa mwajiri wangu kuwa naacha kazi. Wakaja watu wengi kunishawishi nisiende kugombea CUF wakaniahidi kunifanyia mambo mengi lakini sikuwakubalia.

Wakanifuata wakurugenzi, maafisa elimu na watu maalumu kwa sababu  walijua nikigombea kupitia CUF nitashinda hivyo wakanishawishi nigombee kupitia CCM, lakini nikawaambia hapana nimeamua kugombea kupitia CUF.

Nilikuwa nimeshaamua hivyo kwa sababu kwa muda mrefu watu ambao tumekuwa tukiwapeleka bungeni hawana uwezo, nikasema lazima niende kuwatetea wanyonge na kuleta ukombozi wa kweli. Nikaamua kuandika barua ya kuacha kazi ndani ya masaa 24.

MTANZANIA: Mchakato wa uchaguzi ulikwendaje kwa upande wako?

MAFTAH: Mchakato ulikuwa mgumu sana aliyekuwa mgombea wa CCM aliingilia sana uchaguzi ndani ya chama chetu, wajumbe wakanunuliwa kweli kweli lakini wote nikawashinda.

Baadaye wakaanza harakati nisishinde na wakawatumia vyama vingine pamoja na kuwepo Ukawa lakini vyama vyote vilisimamisha wagombea, nikasema hata wakiungana wote nitashinda tu.

Mbali na hilo, pia mchakato ulikuwa mgumu kwangu ukizingatia niliacha kazi na fedha zangu za mafao sikulipwa kwa sababu hawakutaka niache kazi kwa hiyo nilikuwa nina hali ngumu kifedha kwenye kampeni lakini namshukuru Mungu, wananchi walichangishana kila siku kwa ajili ya usafiri na mambo mengine ya kampeni.

Baadaye baada ya upigaji kura kumalizika Mkuu wa Mkoa na Wilaya wakawa wanashinikiza Murji (mgombea wa CCM) atangazwe na wakachelewa kweli kutangaza matokeo na pesa ilitembea lengo likiwa ni ili atangazwe mgombea wa CCM.

Bahati nzuri Mtwara nzima walikuja kulinda kura kwenye maeneo ya majumuisho, baadaye baadhi ya vyombo vya usalama wakawa wanasema hapana, hatuwezi kuua watu kwa sababu walishaona dalili na wangegeuza matokeo zile vurugu za gesi ya Mtwara ingekuwa ni mara kumi yake kwa sababu watu walijiandaa.

MTANZANIA: Ni kero gani ambayo ni sugu katika jimbo lako la Mtwara Mjini?

MAFTAH: Kero ni nyingi lakini kubwa ni kuhusu rasilimali gesi kuondoka bila ya kuwanufanisha wananchi wa Mtwara kwa sababu tumenyanyasika na kudhalilika siku nyingi.

Tukidai fursa za ajira kupitia gesi hiyo wanakuja na mabomu wanaua watu eti sisi tunataka tutumie gesi peke yetu jambo ambalo si kweli, tulichotaka ni wananchi wa Mtwara wanufaike kupata ajira.

Kwa mfano kuna mwekezaji anataka ajenge kiwanda cha mbolea kwa kutumia gesi, huu ni mwaka wa kumi Serikali inamnyima gesi bila sababu ya msingi na nimewaeleza wasimpompa huyu mwekezaji sisi tutaandamana.

MTANZANIA: Unauzungumziaje mwenendo wa Bunge la 11?

MAFTAH: Ujue asilimia 64 ni wabunge wapya 40 ni wale wa zamani hivyo waliokuwa wakionekana ni hao wa zamani ambao wakati wao Bunge lilikuwa linarushwa live.

Sasa kwa Bunge hili ambalo matangazo yake yamesitishwa kurushwa live, ukisimama wewe ambaye Spika hakujui jina anaishia kuwachagua wale ambao ni wazoefu na wanaofahamika.

Sisi wageni hata ukisimama mara mia hakuchagui na ukizingatia Naibu Spika naye ni mpya hivyo na yeye anachagua wale ambao walikuwa ni wachangiaji sana katika Bunge lililopita.

Kingine ambacho nilijifunza katika Bunge hili kuna uchama zaidi kuliko utaifa. Mfano pale wabunge wa upinzani hata wanapokuwa na hoja nzito yenye maslahi kwa taifa, wabunge wa CCM wao wanapinga kwa vile tu imetolewa na upinzani hivyo hii ni mbaya sana na ukizingatia upinzani ni wachache kuliko CCM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles