26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MAENDELEO YA NCHI HAYAKWAMISHWI NA MITANDAO YA KIJAMII


Na MARKUS MPANGALA    |   

HIVI karibuni umesikika mwangwi wa dhana mbaya juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii hapa nchini. Inadaiwa kuwa watu wanatumia uhuru wao vibaya hasa sakata la Sh trilioni 1.5 ambalo liliibua taharuki mwezi uliopita.

Kauli mbalimbali zilitolewa ikiwamo kuwa hatupaswi kuamini kila kitu kinachoandikwa mitandaoni. Hii ni kweli. Tuliambiwa kuwa mitandao hatuidhibiti sisi wenyewe ndiyo maana inabeba na kupokea taarifa potofu. Tuliambiwa kuwa katika nchi kama China “hakuna” mitandao ya Google na WhatsApp. Hapo ndipo hoja yangu ya leo inapoanzia.

Nianze kueleza hili, mitandao ya kijamii ni wavuti au huduma ambayo watu huongea, kupiga gumzo au hujumuishwa pamoja na watu wengine ndani ya nchi au duniani. Huduma ya mitandao ya kijamii inaweza kuunganisha watu wenye mtazamo mmoja au kupenda jambo fulani mfano mpira wa miguu, shule, ndondi, vyakula aina mbalimbali, filamu, dini na urafiki pamoja na kuwa chanzo cha mapato kwa Serikali, ajira, taasisi na watu binafsi.

Mitandao hiyo ni kama ifuatavyo; Facebook, Twitter, Tagged, Flickr, blogu, Snapchart, Pinterest, Badoo, Vk, WeChat, Telegram, Instagram, YouTube, Linkedin, Myspace, Tumblr, Vimeo, Vevo, Skype, Foursquare, Xing, Hangout, Connect na WhatsApp kwa kutaja chache.

Sehemu kubwa ya mitandao ya kijamii inakupa fursa ya kutengeneza taarifa zako katika ukurasa wako ikiwa ni pamoja na picha na maelezo kiasi kuhusu wewe mwenyewe au taasisi fulani. Hasa yale ya msingi, unaishi wapi, una asili ya wapi, elimu, nini unapenda na kadhalika.

Dhana inayojengwa kwamba mitandao ya kijamii ni kitu kibaya zaidi kuwahi kutokea nchini si sahihi hata kidogo. Hapa sitajadili kwa maana ya kulumbana badala yake natoa picha juu ya mitandao hii kwa mtazamo wa kiuchumi, ajira na mawasiliano ya umma katika taasisi mbalimbali.

Kama mwanahabari siwezi kukubaliana na dhana potofu kama hii kwa sababu inatufikirisha zama za kale za kuandika barua za wasomaji magazetini (ambazo hata wahariri wamezifutilia mbali siku hizi).

Kwamba ili msomaji apate kutoa ujumbe au dukuduku lake alilazimika kuandika barua, kuiweka kwenye bahasha na kwenda kuituma katika sanduku la barua la gazeti husika katika Shirika la Posta nchini, ili imfikie mhariri wa gazeti la kampuni husika. Hii ni njia ya kizamani mno (ilifaa enzi za ukoloni), lakini ndiyo ilikuwa sehemu ya maisha yetu, hatupaswi kurudi huko.

Taasisi za kifedha au tuchukulie mfano benki za biashara na kampuni za mawasiliano ya simu, zinaajiri watu wa kusimamia kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii. Wizara mbalimbali za Serikali zinaendesha kurasa zao katika mitandao ya kijamii kwa nia ya kuwasiliana na Watanzania kupitia habari mbalimbali.

Vyombo vya habari vimeanzisha vitengo ya ‘digital’ ili kuongeza tija kwa wasomaji ambao wanapatiwa bashrafu ya habari mbalimbali zinazotokea duniani. Wapo watu binafsi ambao wanaajiriwa na mashirika fulani kuendesha kurasa za mitandao ili kutoa somo, mfano teknolojia.

Tumeona Serikali imewasilisha sheria ya maudhui na hivyo kuzitaka blogu na televisheni (Online TV) za mitandaoni zote zisajiliwe. Hii ina maana mitandaoni kuna ajira ambayo inatolewa na inayolisaidia taifa kutoa taarifa kwa wananchi pamoja na kukuza uchumi wake kwa sababu inakusanya kodi huko.

Tafsiri ya mitandao ya kijamii ni biashara, masoko, jamii (hukutanisha ndugu na jamaa waliopoteana), kodi, mahusiano, urafiki na kadhalika. Ninapenda kutoa mfano huu wa kushangaza. Kijana mmoja Nuseir Yassin, mwenye asili ya Israel na Palestina, anaendesha ukurasa wake wa Nas Daily kwenye mtandao wa Facebook wenye wafuasi 6,001,084 akiwamo Rais wa Malta, Marie-Louise Coleiro Preca.

Rais huyo alimpatia kazi ya kuwa ‘balozi’ wa Malta kwa kufanya kazi mbalimbali kutangaza mazuri na kuvutia watalii kutembelea nchi hiyo. Hayo ni makubaliano ya haraka tu, hatujajua ya faragha ni yapi.

Kijana huyu ni mhandisi wa takwimu (Data Engineer) ambaye aliacha kazi katika kampuni Venmo nchini Marekani, ili kutengeneza video za dakika moja kila siku kutoka sehemu mbalimbali za dunia anazotembelea. Ameshatembelea Zanzibar na kutengeneza video nzuri kabisa iliyowavutia watu milioni 6.

Katika maeneo yote anayotembelea hujadili mada za aina mbalimbali kupitia video hizo zilizomvutia Rais Marie-Louise Coleiro Preca. Anajadili kuhusu amani na usalama, matatizo ya mipaka, ulinzi viwanja vya ndege, vivutio vya utalii, utamaduni, malezi ya watoto, migogoro, hoteli na teknolojia kwa kuzitaja chache. Ameshatembelea Zanzibar, Morocco, Zimbabwe, Palestina, Israel, Malta, Ufilipino, Australia, Misri, Tunisia, Senegal na nyinginezo.

Miezi miwili iliyopita kijana huyo alialikwa na bilionea na mmiliki wa Facebook, WhatsApp na Instagram, Mark Zuckerberg, ili kuelezea zaidi mbinu, mipango anayofanya na matarajio yake. Bado haijasemwa nini kinachofuata, lakini amepiga hatua kubwa mno kupitia mtandao wa kijamii ndani ya miaka miwili tu.

Mifano mingine. Tunafahamu kuwa mmiliki wa Facebook, alisafiri hadi Kenya kwenda kujifunza namna ya uendeshaji wa huduma za kutuma na kupokea fedha (Mobile Money) akilenga kuja kufanya shughuli hiyo.

Facebook imelifikia soko la Afrika Mashariki kwa kuongeza matumizi ya lugha yetu Kiswahili. Jambo hili lilizua zogo hivi karibuni wakati bilionea huyo alipohojiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge la Marekani, kuhusiana na kuvuja siri za wateja wake.

Mmoja wa wabunge alihoji kwanini anatumia lugha ya Kiswahili. Hii ina maana lugha ya Kiswahili inatuletea fursa nyingine kuhitajika timu ya wataalamu kuungana na mmiliki wa Facebook katika udhibiti wa matumizi ya mtandao huo kwa njia chanya. Hawa watamsaidia kubaini matumizi hasi.

Kampuni ya Google ilianzisha huduma ya lugha ya Kiswahili, Google Tanzania ikilenga kuwapata wateja na watumiaji wa lugha hiyo katika eneo la Afrika Mashariki. Hii ni fursa ambayo inatuletea mahitaji ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili, si jambo la kukwazika nalo hili.

Aidha, Google hao hao tena walianzisha huduma ya Google Wallet ili kuwezesha watumiaji kutuma na kupokea fedha, benki, simu za mikononi au baruapepe.

Vilevile Google wameanzisha huduma ya kutafsiri wakaiita “Google Translate’, ambayo huwawezesha Watanzania na watu mbalimbali duniani kutafsiri maneno ya lugha yao kwenda Kiingereza au Kiingereza kwenda Kiswahili inayozungumzwa zaidi ya watu milioni 20. Tunaofanya kazi kila siku kwenye ofisi tumeyashuhudia hayo.

Wafanyabiashara makini wamejazana kwenye mitandao ya kijamii kuvutia wateja. Bidhaa kemkem zinatangazwa kwa sababu inafahamika kuwa dunia inaelekea kujaa kiganjani. Na wafanyabiashara hao wanalipa kodi. Mauzo ya muda wa maongezi yanayofanywa na kampuni za simu, malipo ya Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT) yako dhahiri. Ikiwa na maana mitandao ya kijamii pia inachangia pato la nchi.

Ukweli mwingine, dunia imebadilika. Zama zimebadilika, hatuwezi kukwepa mitandao ya kijamii na hatupaswi kuhofia nguvu zake iwapo tuna uwezo wa kutunga sheria za kudhibiti hali mbaya ikiwemo “Sheria ya maudhui.”

Ukweli huo unatanabaishwa na tafiti kutoka taasisi tatu tofauti ambao unaonyesha kuwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zinakua kwa kasi katika eneo muhimu la matumizi ya teknolojia. Mapinduzi hayo yana maana na fadia kubwa kwetu kiuchumi, utamaduni, kisiasa, jamii na mengineyo.

Utafiti kutoka taasisi za Next Africa, The Economist na Pew Research Center wa mwaka 2016, zote zinakubaliana kuwa Kusini mwa Jangwa la Sahara ni eneo lenye watumiaji wengi wa simu za mikononi.

Kwamba kwa sasa Afrika ni sehemu bora ya mapinduzi ya teknolojia. Teknolojia inayozungumzwa hapa ni mambo yote yahusuyo utoaji na upokeaji wa huduma zote za kiufundi, elimu au ufahamu na pengine matumizi ya mashine yanahusika pia pamoja na mitandao ya kijamii.

Mitandao ya kijamii imesaidia wagonjwa, wahudumu, wafanyakazi, wataalamu, waandishi wa habari, mashirika ya habari, watendaji wa kila ngazi ambao wanategemea huduma hiyo kuhakikisha shughuli zinakwenda salama.

Ripoti ya utafiti ya ‘Digital in 2018’ ya Taasisi ya We Are Social and Hootsuite, inaonyesha kuwa nusu ya watu duniani (bilioni 4) wapo mitandaoni na robo ya watu katika idadi hiyo wamejiunga mtandaoni kwa mara ya kwanza mwaka 2017. Sababu kubwa inayotajwa ni ongezeko la matumizi ya SimuJanja (Smartphones) na manunuzi ya bando la intaneti.

Nchi zinazokua kwa kasi chini ya asilimia 20 ya watumiaji wa intaneti barani Afrika ni Mali, Benin, Sierra Leone, Niger na Msumbiji. Hadi mwaka 2017 zaidi ya watu milioni 200, wanamiliki simu za mikononi na theluthi mbili ya watu bilioni 7.6 walioko hai (sawa na watu bilioni 5.135) duniani wanamiliki simu za mikononi.

Zaidi ya watu bilioni 3 duniani sasa wanatumia mitandao ya kijamii kila mwezi pamoja na watu 9 kati ya 10 wanatumia kupitia simu za mikononi. Kila baada ya sekunde moja hadi mwaka 2017, watu 11 wanajiunga na mitandao ya kijamii sawa na watu milioni moja ya wanaotumia kwa mara ya kwanza. Takwimu nyingine kutoka taasisi ya GlobalWebIndex, zinaonyesha untaneti inatumiwa kwa muda wa saa 6.

Kimsingi anayekwamisha maendeleo ya nchi yetu si mitandao ya WhatsApp, Twitter, Telegram, Google, Tagged, blogu au neno la jumla mitandao ya kijamii, bali ni matendo yetu katika maisha ya mitaani, hulka zetu, sera zetu, uongozi wetu na taratibu zetu za kuyafikia. Mtu akiniambia anaichukia mitandao hii huwa nabaki kumshangaa, labda ni kizazi kilichozaliwa na kukulia zama za giza za ukoloni. Ila nashangaa, tusitafute visingizio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles