22 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

MAJANGILI 4,000, BUNDUKI 100 MBARONI


Na Ramadhan Libenanga - Morogoro

JUMLA ya majangili 4,294 wamekamatwa pamoja na bunduki 101, zikiwamo tisa za kivita katika kipindi cha mwaka 2016/2017.

Taarifa hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, wakati akifungua kikao cha pamoja kati ya maofisa upelelezi mkoa na wahifadhi kutoka hifadhi za taifa nchini kilichoandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Nsato alisema bado kuna changamoto ya matukio ya ujangili katika hifadhi za taifa, na kikao hicho kitakuwa chachu katika kupanga mikakati ya kukomesha ujangili.

“Kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 walikamatwa majangili 4,294, silaha za kivita (SMG) tisa, bunduki za kiraia (rifle) 19, magobore 55, shotgun 18 na mitego ya waya 84,817,” alisema.

Pia alisema jumla ya tembo 15 na wanyama wengine aina tofauti 2,647 waliuawa, huku kesi 5,588 za matukio ya ujangili zimefikishwa mahakamani.

Alisema kati ya kesi hizo, mpya ni 959 na 1,637 zimekwisha baada ya kusikilizwa na 2,992 zinaendelea katika mahakama mbalimbali zilizopo hapa nchini.

“Bado kuna changamoto ya ucheleweshwaji wa kesi za ujangili, hivyo kikao iki kiwe chachu ya kumaliza kasoro zilizopo, tukiwa na lengo moja la kukomesha matukio ya ujangili,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, alisema kikao hicho kitaweka mikakati ya kukomesha kabisa mitandao ya majangili sugu nchini.

Alisema lengo la kikao hicho pia ni kujadili masuala ya utendaji kazi kwa makundi yote mawili katika kudhibiti matukio ya ujangili.

“Ni vyema kujadili mbinu bora ya kuzuia ujangili,” alisema.

Pia alisema kuweka mikakati ya pamoja kati ya polisi na Tanapa kutaleta tija kubwa katika kukabiliana na majangili hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,284FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles