BOMBAY, India
JITIHADA za ukoaji bado zinaendelea katika Jimbo la Kerala Kusini Magharibi mwa nchi hii, baada ya kukumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua ya masika inayoendelea kunyesha eneo hilo.
Taarifa zilizopatikana mjini hapa zinaeleza kuwa kwa sasa helikopta za kikosi cha anga na cha wanamaji zinafanya kazi ya kuwakoa wakazi wa eneo hilo ambao wamekwama juu ya mapaa ya nyumba, na zikiwasambazia misaada ya chakula ambao bado hawajaokolewa.
Maofisa wa serikali katika eneo hilo wanaeleza timu za uokoaji zimeelekeza nguvu zaidi katika mji wa Chengannur, ambako inasemekana zaidi ya watu 5,000 wamekwama.
Mmoja wa wanasiasa katika eneo hilo, Saji Cherian, alionekana akikibubujikwa na machozi wakati akiomba msaada wa kupelekewa helikopta.
“Tafadhairi tunaomba msaada wa helikopta, Tafadhari nisaidieni watu watakufa. Tafadhari tusaidfieni hakuna suluhisho jingine zaidi ta watu kuokolewa,”alisikika akisema mwanasiasa huyo.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, Yogita Limaye, aliyepo katika jimbo hilo la Kerala, alisema licha ya serikali kupeleka msaada wa hekopta na boti, pia mitumbwi ya wavuvi inatumika kuwaokoa waliokwama huku mingine ikisaidia kusambaza chakula cha msaada.
Alisema mbali na misaada hiyo ya binadamu, pia wamiliki wa kampuni za mawasiliano wameamua kutoa huduma hiyo bure kuwasaidia waliokwama, kuweza kutuma na kupiga simu kuelezea hali inayowakabili.
Alisema hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na barabara za kuingia katika eneo hilo kujaa matope jambo ambalo limewalazimu wanajeshi kutengeneza njia na madaraja ya dharura kwa ajili ya kurejesha mawasiliano ya barabara.
Maofisa wa Kitengo Cha Dharura katika jimbo hilo walisema zaidi ya familia 200,000 zimekwisha kupewa hifadhi ya muda.