Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Posta (TPC) limetapanya zaidi ya sh. Milioni 10 na viwanja 198.
Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Kanali mstaafu, Dk. Harun Kondo katika kikao cha viongozi waandamizi wa shirika hilo kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Dk. Kondo alisema utapanywaji wa mali na fedha za shirika hilo uligunduliwa na bodi ambayo baada ya kuteuliwa kazi yake ya kwanza ilikuwa kuhakiki mali za shirika na ukaguzi wa fedha.
Alisema wakati wa ukaguzi huo, bodi ilibaini kuwepo kwa akaunti 120 za shirika katika benki mbalimbali ambazo iliamua kuzifunga wakati ikiendelea na ukaguzi.
Dk. Kondo alisema ukaguzi ulibaini viwanja 198 vya shirika vilikuwa vimeporwa na kumilikishwa kwa watu na binafsi huku kukiwa hakuna maelezo yeyote kuhusu viwanja hivyo kuhamishwa umiliki wake.
“Tulibaini matumizi ya fedha yalikuwa ya ovyo na shirika halikuwa na akiba hata shilingi moja huku likiwa linawadai wateja wake Sh. bilioni 16. Watendaji walikuwa hawazifuatilii.
“Kuna methali inasema anayeficha ugonjwa kifo kitamuumbua. Kwa kuwa shirika hili ni mali ya umma ni vema jamii ikatambua madudu tuliyoyabaini na sisi kama bodi tulisema liwalo na liwe madudu lazima yabainike na watendaji wabovu wawajibishwe,” alisema Dk.Kondo.
Akizungumzia mwenendo wa ukaguzi wa mali za shirika mikoani, alisema bodi ilibaini baadhi ya viwanja vilivyoporwa vilishajengwa nyumba na watu binafsi.
Alisema hivi sasa utaratibu wa kuvirudisha kwenye miliki ya shirika unafanyika.
“Tulipokuwa tukikabidhiwa ripoti ya utendaji kazi na mali za shirika hakukuwa na orodha ya kiwanja hata kimoja kinachomilikiwa na shirika, tuliingiwa na wasiwasi tukaamua kufuatilia.
“Wakati tunaanza kazi hii tulipigwa vita kweli lakini wengi waliotupiga vita ni wale waliokuwa wanafahamu madudu ndani ya shirika hivyo waliona tunaweza kuwaumbua na tunashukuru hadi sasa tumefanikiwa kuvirejesha viwanja 198,” alisema Dk. Kondo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, bodi pia ilibaini shirika lilikuwa halijawahi kufanya hesabu za mwaka ndani ya miaka tisa na deni lililokuwa nje lilikuwa kubwa.
Kwamba iliamua kuwafuatilia wadaiwa sugu ambao walilipa Sh. bilioni 10.
“Ajabu, baada ya kuzikusanya fedha hizo, baadhi ya watendaji walichukua Shilingi Bilioni Nane, wakazitumia bila kuishirikisha bodi. Tulipowabaini tulichukua hatua, baadhi yao tuliwafukuza kazi.
“Wengine tliwashtaki mahakamani na wapo tuliowafikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU),” alisema Dk. Kondo.
Alisema ili kukabiliana ubadhirifu wa mali za shirika bodi iliamua kununua mashine mpya ya kisasa ya ukaguzi.
Aidha, mwenyekiti huyo alisema wakati wa ukaguzi wav yeti vyeki, wafanyakazi 65 waliondolewa kazini.
Naye Mtendaji Mkuu wa TPC alisema shirika hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wapo kwenye mchakato wa kuanzisha anuani za makazi.