Na CLARA MATIMO- MWANZA
MKUU wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Dk. Leonard Masale, amewataka madiwani kusimamia matumizi ya fedha za Serikali kwa kuhakikisha halmashauri zinazingatia sheria, kanuni na taratibu katika masuala ya manunuzi ya umma.
Wito huo ulitolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya, Said Kitinga kwa niaba ya Dk. Masale, wakati akifunga semina ya siku tatu ya kuwajengea uwezo madiwani kuhusu manunuzi ya umma.
Semina hiyo iliandaliwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Ilemela (ILEDICNET), kupitia mradi wake wa kukuza ushiriki wa wananchi katika matumizi ya rasilimali za umma, kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society (FCS).
Dk. Masale aliwataka madiwani hao kutumia elimu waliyoipata kusimamia vyema matumizi ya rasilimali za umma ambazo hufujwa na baadhi ya watendaji wasiokuwa waadilifu kwa kupitia miradi ya manunuzi ya umma, na hivyo kusababisha halmashauri nyingi kupata hati zenye shaka, zisizoridhisha ama mbaya.
Mwezeshaji wa semina hiyo, mkaguzi wa nje wa hesabu za serikali tawi la Mwanza, Cletus Sutta, alisema changamoto kubwa ambayo wanakabiliana nayo ni kumkagua mwajiri.
“Kwa kweli hatufanyi kazi kwa uhuru kwa sababu mkurugenzi ndiye mwajiri wetu na anao uwezo wa kumfukuza kazi mfanyakazi yeyote kutoka katika ofisi yetu, hivyo hata tunapokwenda kumkagua huwa hatufanyi kazi kwa uhuru.
“Lakini naishukuru Serikali kwa sababu ililiona hilo na imeanzisha taasisi huru ya kukagua na kudhibiti fedha za Serikali, ninaamini itakapoanza kazi, tutafanya kazi kwa uhuru zaidi,” alisema Sutta.
Mwenyekiti wa Bodi wa ILEDICNET, Ulinyelusya Tumbo, alisema semina hiyo imewashirikisha madiwani, viongozi wa dini, wakuu wa idara wa Manispaa ya Ilemela, wawakilishi wa vyama vya siasa na waandishi wa habari kwa lengo la kukuza ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa matumizi ya rasilimali za umma.