Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wametaka kuwepo na mpango mahususi wa upimaji afya bure baada ya kubainika kuwa wagonjwa wengi waliojitokeza katika meli ya matibabu ya Wachina wanatoka Ilala.
Akizungumza leo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani, Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Omar Kumbilamoto, amesema kwa hali ilivyo inaonekana kuna tatizo kubwa katika sekta ya afya.
“Hata Mstahiki Meya leo mnaona hatuko naye hapa kwa sababu na yeye anaumwa amekwenda kwenye meli hiyo kupata matibabu,” amesema Kumbilamoto.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Victorina Ludovick, amesema wananchi wengi wanashindwa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwa sababu ya kushindwa kumudu gharama za matibabu katika vituo vya serikali na binafsi.
Kutokana na hali hiyo amesema watatenga fedha zitakazopelekwa katika zahanati 23 za halmashauri hiyo kwa ajili ya kuhamasisha upimaji wa magonjwa ya kisukari, presha na mengine.