27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

NYAKATI NGUMU ZISIKUFANYE UKATENGANA NA WATU

Na CHRISTIAN BWAYA


IRENE alikuwa na ndoto za kuwa mama wa familia bora. Tangu akiwa binti mdogo, alipenda watoto. Kila alipowaona wakicheza, moyo wake ulisisimka kwa furaha. Hata pale alipokuwa katika mazingira yanayomweka karibu na mama mwenye mtoto, ilikuwa kawaida kwake kuwasiliana na mtoto kwa ishara ya tabasamu.

Baada ya kumaliza masomo yake kwa mafanikio, alikutana na Stephen, aliyekuja kuwa mume wake. Stephen alikuwa kijana mtaratibu, mcha Mungu, mwelewa na mwenye upendo kwa mke wake.

Hata hivyo, miaka saba baada ya ndoa yao, Irene na Stephen bado hawajabahatika kupata mtoto. Pamoja na jitihada za kila namna walizojaribu kufanya, ndoto zao hazijatimia. Mwanzoni waliichukulia hali hiyo kuwa ya kawaida wakiamini muujiza ungetokea. Lakini kadiri miaka ilivyozidi kusonga, ndivyo jambo hili lilivyozidi kuwa changamoto katika ndoa yao.

Ndugu wa mume wanamnyooshea kidole Irene kwamba ndiye mwenye tatizo. Maneno ya jamaa na marafiki nayo kwa upande mwingine, yanawakosesha amani. Irene anajisikia kama mtu mwenye bahati mbaya na maisha.

Akiwa katika hali hiyo ya kukata tamaa, majuzi Irene alipata taarifa kutoka kwa ndugu wa mumewe kwamba Stephen ana mtoto nje ya ndoa na yuko mbioni kuoa mke mwingine. Moyo wake ulizizima kwa hasira na masikitiko makubwa. Pengine kwa kujisikia fedheha na kudhalilishwa, Irene hana ujasiri wa kukutana na marafiki. Muda mwingi anautumia ndani akilia na kuomboleza.

Hakuna mtu asiyepitia katika kipindi kigumu. Ingawa tunaweza kutofautiana kiwango cha changamoto tunazokuwa nazo, lakini ni ukweli kuwa kila mtu, kwa wakati fulani hukutana na mambo magumu. Inawezekana si kukosa mtoto kama ilivyokuwa kwa Irene bali ni kutokufikiwa kwa malengo uliyojiwekea. Pengine ni kupatwa na mambo mabaya usiyotarajia. Hizi zote ni nyakati ngumu zinazoweza kukukosesha usingizi.

Katika nyakati ngumu kama hizi, wakati mwingine, mtu hutamani kukaa mbali na watu. Irene alijitenga na watu anaowafahamu kama njia ya kujihurumia na kutafuta kujiliwaza.

Ni kweli, wakati mwingine kujitenga kunaweza kukusaidia kuwaepuka watu wanaoweza kuwa sababu ya huzuni kwako. Fikiria ndugu, jamaa na marafiki ambao Irene anajua fika wanamsema vibaya. Wengine ndio hao wanaomletea maneno kwa lengo la kumkatisha tamaa. Kujitenga na watu wa namna hii inaweza kuwa muhimu.

Hata hivyo, ukaribu na watu wanaoaminika ni hatua muhimu kuchukua unapopita katika kipindi kigumu. Watu wenye mtazamo chanya, kwa mfano, ndio watakaokusaidia kukutia moyo, kukufariji na kukufanya uyatazame mambo kwa namna itakayochangamsha tena moyo wako.

Kwa vyovyote vile, unawafahamu watu katika maisha yako unaoweza kusema unawaamini. Hawa ni watu mnaoaminiana na kuheshimiana. Hawa si watu wepesi kukushambulia, kukuhukumu na kukuonyesha namna gani hali uliyonayo hukupaswa kuwa nayo. Ambatana na watu wa namna hii.

 

Vile vile, jifungamanishe na vikundi vya kijamii ulivyonavyo tayari. Inawezekana ni waumini wenzako kanisani au msikitini. Hata kama hauwafahamu watu hawa kiundani, bado kwa kule kuwa nao karibu itakusaidia kuyatazama maisha kwa sura ya matumaini.

Nyakati ngumu, mara nyingi hukufanya uone upande mbaya wa maisha. Unapokuwa unatafuta mtoto na hujampata, kwa mfano, unaweza kuanza kujihesabu kama mtu asiye na thamani. Unapoona wenzako wakipata mtoto muda mfupi baada ya ndoa, ni rahisi kuanza kuwa  mtazamo hasi na maisha. Unaanza kujihurumia, kulaumu na wakati mwingine kujihukumu kwa makosa ambayo wakati mwingine si ya kwako.

Lakini unapokwenda kwenye vikundi vya kiimani,  mbali na kukutana na watu wanaoweza kukubadilishia mtazamo wako kwa hicho kigumu kilichokutokea, vikundi hivi vitakusaidia kuyatazama maisha kwa mtazamo mpana.

Kwa mfano, badala ya kuchukulia kukosa mtoto wa kumzaa kama janga kubwa linalokukosesha amani na maisha, ukijengwa kiimani na wenzako mtazamo wako unaweza kubadilika. Watu wengi waliochelewa kupata mtoto kwenye Biblia, kwa mfano, walikuja kuzaa watu wakubwa. Manabii maarufu tunaowasoma kwenye Biblia, wengine walizaliwa na akina mama walioitwa tasa lakini walipojifungua, walizaa watu walioeleta mabadiliko makubwa. Pengine wewe ni mmoja wao.

 

Pia ni vizuri wakati mwingine kukutana na watu wenye uzoefu wanaoweza kukupa mawazo chanya ya namna ya kukabiliana na changamoto yako. Irene, kwa mfano, anaweza asipate muujiza wa mtoto tena. Ili kukidhi shauku aliyonayo, Irene anaweza kukutana na watu wanaoweza kumwelekeza namna ya kuasili mtoto kwa mujibu wa sheria. Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba kukutana na watu wenye uzoefu  kwa gumu unalopitia, inaweza kuwa na faida nyingi kuliko kukata mawasiliano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles