24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO WANAHITAJI MUDA KUCHEZA NA WAZAZI

Na Christian Bwaya


TUNAVYOWALEA watoto wetu siku hizi, wakati mwingine sivyo tulivyolelewa sisi na wazazi wetu. Wakati zamani wazazi hawakuwa na kazi zilizowalazimu kuwa mbali na nyumbani, siku hizi hali hii ni ya kawaida. Imekuwa kawaida kwa wazazi kutoka nyumbani alfajiri na kurudi usiku wakati ambao tayari watoto wameshalala.

Pilika hizi nyingi za kikazi zina lengo jema la kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao ya msingi kama watu wengine yaani kula vizuri, kupata mahali salama pa kulala, kuvaa vizuri, kuwa na afya njema na hata kwenda shule bora.

Lakini pamoja na umuhimu wa mahitaji haya, ni vizuri kutambua kuwa watoto wanahitaji uwepo wetu zaidi. Wanahitaji tupatikane tuweze kuwasikiliza kujua undani wa maisha yao ambao wakati mwingine hawawezi kuwaambia watu wengine.

Kwa kuzingatia umuhimu huo wa kuwa karibu na watoto, ni wazi tuna kazi ya kufanya jitihada za kuhakikisha tunatengeneza muda utakaotuwezesha kupata muda mzuri wa kuwa na familia.

Binafsi nimegundua wakati mwingine ukiwa na tabia ya kutengeneza mipango isiyokutenganisha na familia inasaidia si tu kuwafanya watoto kujua kitu hasa wanachotarajiwa kukitekeleza lakini pia kukulazimu mzazi kuwa karibu nao.

Shughuli zenye malengo ya kifamilia ni mfumo wa uwajibikaji unaosaidia kukukumbusha mzazi kutenga muda kwa ajili ya kukidhi matarajio ya watoto.

Kwa watoto wengi, kwa mfano, kukumbuka sherehe za kuzaliwa, mahafali, siku ya wazazi shuleni na matembelezi ni mambo yanayoweka kumbukumbu ya kudumu katika fahamu zao kwa muda mrefu. Unapokumbuka kuingiza mambo haya ya wanao katika mipango yako, inawasaidia watoto kuona unajali mambo yao.

Lakini kuna suala la kukosa muda hasa kwa wazazi walioajiriwa. Inakuwa vigumu, mathalani, kwa wafanyakazi kumaliza majukumu yao wakiwa kazini. Kutomaliza shughuli zao wakiwa kazini huwalazimisha kuhamishia ofisi nyumbani. Mazoea kama haya yanachangia kwa kiasi kikubwa kuwakosesha watoto muda wa kuwa na wazazi wao. Wakati mtoto anamhitaji baba, ndio kwanza anawasha kompyuta kukamilisha kazi za ofisi.

Wingi wa majukumu unaweza usiwe kisingizio cha kutosha. Kuna mambo mengi yanaweza kuchangia kupoteza muda katika eneo la kazi kwa matarajio kwamba kazi hizo zitahamishiwa nyumbani.

Kwa mfano, wafanyakazi wengi huweza kutumia muda mwingi kwa soga zisizo na tija wawapo kazini. Teknolojia imefanya iwe rahisi ‘kuishi’ kwenye mitandao ya kijamii bila ulazima. Matokeo yake, tunajikuta hatukamilishi majukumu ya kazi kwa muda uliopangwa na hasara ya upotevu huu wa muda hufidiwa kwa kukosekana nyumbani.

Sambamba na kutokuhamishia kazi za ofisi nyumbani, ni muhimu kukumbuka wajibu wetu wazazi tuwapo nyumbani. Watoto wanahitaji kukaa na mzazi na si mzazi anayeendelea kuwa polisi, meneja, mwalimu au injinia awapo nyumbani.

Pengine aina ya kazi unayofanya haikuruhusu kupata muda katika siku za wiki. Ikiwa hivyo, fikiria kutumia siku za mwisho wa wiki kwa familia yako. Kuendelea na ratiba nyingine za kazi siku za mwisho wa wiki ni kuwanyima watoto haki yao ya msingi.

Dhamiria kuwa siku za Jumamosi na Jumapili ni maalumu kwa ajili ya kukaa na familia yako badala ya kutoka na marafiki. Unapokuwa nyumbani unawapa watoto wako muda wa kutosha kukufurahia kwa mazungumzo na michezo ya pamoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles