Na Upendo Mosha, Moshi
MADAKTARI, wauguzi na wataalamu wa vipimo vya maabara 13, wanadaiwa kuambukizwa Kifua Kikuu (TB) wakati wakitoa huduma za afya kwa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.
Hali hiyo inatokana na upungufu wa wodi za kulaza wagonjwa na hivyo kulazimika kuwachanganya wagonjwa wa TB na wagonjwa wengine katika wodi moja.
Mratibu wa magonjwa ya kifua kikuu na ukoma mkoani hapa, Dk. Manase Chelangwa alibainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari mjini Moshi.
Alisema madaktari na wauguzi hao waligundulika kuambukizwa ugonjwa huo kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu.
Dk. Chelangwa alisema hospitali hiyo haina wodi maalumu ya kulaza wagonjwa wa TB na hivyo kulazimika kuwalaza katika wodi mbalimbali na wagonjwa wengine.
Alisema hulazimika kuwatengea eneo dogo wakati wakiendelea kupata matibabu jambo ambalo linadaiwa kuleta athari kubwa ya maambukizi ya ugonjwa huo kwa wataalamu wa afya na watu wengine.
“Hospitali yetu haina wodi ya kuwalaza wagonjwa wa TB pekee isipokuwa huwa tunawalaza na wagonjwa wengine kwa kuwatenganisha umbali wa mita mbili hadi tatu kutoka kwa mgonjwa mmoja hadi mwingine.
“Hatua hiyo inayokwenda pamoja na kutoa elimu na vifaa kwa madaktari na wauguzi ya jinsi ya kujikinga na maambukizi ya TB lakini bado ni changamoto kwa vile tayari wataalamu wetu wa afya 13 wamepata maambukizi,” alisema.
Dk. Chelangwa alisema Mkoa wa Kilimanjaro upo katika orodha ya mikoa 10 nchini inayoongoza kwa maambukizi ya TB na kwamba kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo imekuwa ikiongezeka na kupungua kidogo kila mwaka jambo ambalo bado ni tishio.
“Maambukizi ya TB yamekuwa yakiongezeka na hayajawahi kupungua kwa sababu mwaka 2011 kulikuwa na wagonjwa 2,548, 2012 wagonjwa wawili, 287, 2013 wagonjwa 2,519, mwaka 2014 maambukizi yalifikia watu 2,444 wakati mwaka 2015 kulikuwa na wagonjwa 2,414,” alisema.
Alisema hali maambukizi ya ugonjwa huo yamekuwa yakionekana bado yapo juu kutokana na baadhi ya wagonjwa kuchelewa kufika hospitali na kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupata matibabu mapema jambo ambalo limekuwa likisababisha ugonjwa huo kuwa sugu na kusababisha vifo ambavyo vingeweza kuepukika.