24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Madaktari, wauguzi waambukizwa TB wakihudumia wagonjwa

image

Na Upendo Mosha, Moshi 

MADAKTARI, wauguzi na wataalamu wa vipimo vya maabara 13, wanadaiwa kuambukizwa    Kifua Kikuu (TB) wakati wakitoa huduma za afya kwa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.

Hali hiyo inatokana na upungufu wa wodi za kulaza wagonjwa na hivyo kulazimika kuwachanganya wagonjwa wa TB na wagonjwa wengine katika wodi moja.

Mratibu wa magonjwa ya kifua kikuu na ukoma mkoani hapa, Dk. Manase Chelangwa alibainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari mjini Moshi.

Alisema madaktari na wauguzi hao waligundulika kuambukizwa ugonjwa huo kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu.

Dk. Chelangwa alisema hospitali hiyo haina wodi maalumu ya kulaza wagonjwa wa TB na hivyo kulazimika kuwalaza katika wodi mbalimbali na wagonjwa wengine.

Alisema  hulazimika kuwatengea eneo dogo wakati wakiendelea kupata matibabu jambo ambalo linadaiwa kuleta athari kubwa ya maambukizi ya ugonjwa huo kwa wataalamu wa afya na watu wengine.

“Hospitali yetu haina wodi ya kuwalaza wagonjwa wa TB pekee isipokuwa huwa tunawalaza na wagonjwa wengine kwa kuwatenganisha umbali wa mita mbili hadi tatu kutoka kwa mgonjwa mmoja hadi mwingine.

“Hatua hiyo inayokwenda pamoja na kutoa elimu na vifaa kwa madaktari na wauguzi ya jinsi ya kujikinga na maambukizi ya TB lakini bado ni changamoto kwa vile  tayari wataalamu wetu wa afya 13 wamepata maambukizi,” alisema.

Dk. Chelangwa alisema Mkoa wa Kilimanjaro upo katika orodha ya mikoa 10 nchini inayoongoza kwa maambukizi ya TB na kwamba kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo imekuwa ikiongezeka na kupungua kidogo  kila mwaka jambo ambalo bado ni tishio.

“Maambukizi ya TB yamekuwa  yakiongezeka na hayajawahi kupungua kwa sababu  mwaka 2011 kulikuwa na wagonjwa 2,548, 2012 wagonjwa wawili, 287, 2013 wagonjwa 2,519, mwaka 2014 maambukizi yalifikia watu 2,444 wakati mwaka 2015 kulikuwa na wagonjwa 2,414,” alisema.

Alisema hali maambukizi  ya ugonjwa  huo yamekuwa yakionekana  bado yapo juu kutokana na baadhi ya wagonjwa kuchelewa kufika hospitali na kwenye vituo vya afya kwa ajili ya  kupata matibabu mapema jambo ambalo limekuwa likisababisha  ugonjwa huo kuwa sugu na kusababisha vifo ambavyo vingeweza kuepukika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles