Msalaba Mwekundu wazidi kushikana ‘uchawi’

ambulance_k

NA CHRISTINA GAULUHANGA,DAR ES SALAAM

BAADHI ya wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu wameazimia kuandamana wakitaka  viongozi wao wajiuzulu kwa kile walichodai kuchoshwa na  ufisadi wa mali za chama unaofanywa na bodi ya chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho Tawi la Mzizima, Dk.Suphian Khamis alisema wanachama  hao wamechoshwa na ufisadi wa mali za chama hivyo wameazimia kutangaza maandamano nchi nzima kupinga ubadhirifu huo.

“ Katika hili hatukubaliani nalo tulikuwa kimya kwa muda mrefu lakini ili tukinusuru chama kisifilisike ni lazima tupaze sauti zetu tumechoka na ubadhirifu unaofanywa na viongozi hawa…tunajiandaa kufanya maandamano na tarehe tutaitangaza baada ya kukubaliana na wenzetu,”alisema Dk.Suphian.

Alisema chama hicho kina zaidi ya miaka 50 baada ya kuanzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 71 ya mwaka 1962 kwa lengo la kuisaidia serikali katika utoaji wa huduma za binadamu.

Hata hivyo alisema  uendeshwaji wa chama hicho umekuwa na matatizo makubwa ambayo yanaweza kusababisha chama kufa.

“Viongozi wetu wamekuwa wakijipangia mambo bila kushirikisha wanachama kinyume na katiba yetu hivyo ifike wakati viongozi hawa wakae pembeni  chama kisonge mbele,”alisema Dk.Suphian.

Alisema wanamuomba Rais Dk. John Magufuli aiingilie kati suala la ubadhirifu ndani ya chama hicho kwa maslahi ya chama na taifa kwa ujumla.

Dk. Suphian alisema viongozi hao wamethubutu kuuza jengo la chama lililopo barabara ya Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi ‘Viva Tower’  bila idhini ya Baraza la Wadhamini au Halmashauri Kuu ya Chama.

“ Zipo tuhuma nyingi ikiwamo ukwepaji kodi, matumizi mabaya ya rasilimali  na miradi ya chama … wapo viongozi wastaafu wa muda mrefu ambao wamejilipa fedha za mafao na bado wanaendelea kung’ang’ania ofisini kwa visingizio mbalimbali,”alisema Dk.Suphian.

Alisema kuna kila sababu ya Rais Dk.Magufuli kuingilia kati suala hilo na   kuchunguza malalamiko yetu pamoja na kuwachukulia hatua wahusika wa ubadhirifu ili chama kirejee kwenye misingi yake ya awali.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu kujibu tuhuma hizo, Kaimu Rais wa chama hicho, Zainab Gama ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya chama hicho, alisema  bodi ya chama iliamua kuchukua uamuzi wa kuuza baadhi ya ghorofa za jengo la chama hicho  kuepuka kisifilisiwe kwa sababu ya kukithiri madeni ya chama hicho.

Alisema mchakato wa uuzaji wa jengo hilo ulifanywa kwa dharura na liliuzwa kwa zaidi ya Sh bilioni tatu ambazo zimetumika kulipa madeni mbalimbali ikiwamo wataalamu washauri, mishahara na mtaalamu aliyewaandikia ripoti ya chama hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here