24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

MACHINGA DAR WACHOMA MATAIRI BARABARANI

Vibanda vya wamachinga vilivyokuwa vimejegwa jirani na jengo la Machinga Complex
liliopo Ilala, Dar es Salaam vikiwa vimebomolewa na Halmashauri ya jiji hilo jana.

MAULI MUYENJWA Na JOHANES RESPICHIUS -DAR ES SALAAM

TAFRANI imezuka baada ya wafanyabiashara ndogondogo nje ya Jengo la Machinga Complex kuanzisha vurugu kwa kuchoma matairi barabarani wakipinga Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kubomoa mabanda yao usiku wa manane.

Vurugu hizo ambazo zilitokea alfajiri jana zilisababisha usafiri wa magari katika eneo hilo kusimama kwa muda hadi askari wa Kikosi cha zima moto walifika na kuuzima moto huo pamoja na wale wa Kutuliza ghasia (FFU) ambao waliwasili na kudhibiti hali hiyo.

MTANZANIA lilizungumza na baadhi ya Wamachina ambao walieleza kuwa kilichofanywa na halmashauri ya jiji hilo ni uvamizi na uonevu wa wazi.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara hao, Abubakar Rakesh alisema kuwa halmashauri hiyo imekiuka agizo la Rais Dk. John Magufuli ambaye aliagiza wasibughudhiwe wala kuhamishwa katika maeneo yao bila kupatiwa sehemu nyingine nzuri.

Alisema hata Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) waliwaruhusu kuendelea kuwepo katika eneo hilo kutokana na changamoto ya biashara katika jengo hilo.

“Tulishakaa tukaongea na liliamuliwa na kamati hiyo ya Bunge kuwa kutokana na changamoto za biashara katika eneo hili wateja hawapandi kwenye jengo hilo basi tushuke chini tufanye biashara na tukaacha vibanda vyetu juu na tulikuwa tunavilipia kwa maana ndio vilikuwa vinatupa uhalali wa kufanya biashara hapa chini.

“Kilichotokea ni uvamizi, vibanda vimevunjwa usiku wa manane na kusababisha upotevu wa mali za wafanyabiashara hawa kama walitaka kufanya kihalali wangekuja muda ambao ni asubuhi ili tuhamishe vitu vyetu,”alisema Rakesh.

Mfanyabishara mwingine, Pili Hassan aliyekuwa akifanya biashara ya viatu na mabegi na mali yake iliyopotea ilikuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 1.2.

 Mfanyabiashara mwingine, Yohana William alisema kuwa vizimba ambavyo walipewa vimeuziwa watu wengine ambao sio wafanyabiashara na wamefungua ofisi zao ambazo hazihusiani na lengo la jengo hilo.

“Tunajua wanachokitaka ni kutuondoa ili eneo hili waligeuze maegesho ya magari kwa maana wanajua ndio itakayowalipa lakini sisi tuko ndani ya soko na tunafanyiwa hivi tunauliza wale wanaofanyabiashara hizi barabarani wapo kisheria? alihoji William.

Meneja wa soko hilo hakupatikana kuzungumzia suala hilo. Hata hivyo Mhasibu Mkuu wa soko hilo, Betha Mariki alisema kilichotokea ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene ambaye aliagiza kuondolewa kwa wafanyabiashara wasiofuata taratibu katika soko hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles