23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Machinga kushiriki maonesho Sabasaba

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Umoja wa Wafanyabiashara ndogondogo Mkoa wa Dar es Salaam maarufu kama machinga umesema utashiriki Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) yanayotarajiwa kuanza Juni 28.

Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Namoto, akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ushiriki wao katika maonesho ya Sabasaba.

Hivi karibuni kulikuwa na taarifa zilizosambaa zikisema kuwa wamachinga hawatashiriki maonesho hayo hatua iliyolazimu umoja huo kutoa ufafanuzi na kuwatoa hofu wanachama wao.

Akizungumza na Waandishi wa habari Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Namoto, amesema maonesho hayo yana manufaa kwao na mwaka jana zaidi ya machinga 260 walishiriki.

“Taarifa kwamba kuna tozo ya Sh milioni moja si kweli, bado Tantrade hawajatangaza viwango, hizi taarifa zinalenga kuleta uchonganishi. Siku zote kunapotokea tukio lolote katika mkoa fulani uongozi wa machinga wa mkoa husika ndio huratibu hivyo wanachama wetu watulie,” amesema Namoto.

Amesema katika maonesho ya mwaka jana walipewa banda maalumu ambapo ada ya ushiriki ilikuwa Sh 150,000 na kila machinga alikuwa na meza na sehemu ya kuhifadhia mizigo wake huku akiruhusiwa kuingia na msaidizi mmoja wakati wote wa maonesho.

Naye Katibu wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Masoud Chauka, amesema mfumo unaotumiwa na Shirikisho la Wamachinga Tanzania si rafiki na kudai kuwa unalenga kuwanufaisha wachache.

“Shirikisho kama wanataka kufanya kazi na sisi tukutane tuzungumze vinginevyo kama hawataki tutajitenga nao tujisimamie wenyewe, haiwezekani unaingia kwenye mikataba ndani ya mkoa wetu bila kutuarifu,” amesema Chauka.

Kwa mujibu wa Chauka, umoja huo una mfumo wa kanzidata ya wamachinga wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba Saccos yao tayari ina wanachama zaidi ya 2,0000.

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) inaendelea na maandalizi ya maonyesho ya 46 ambayo yanatarajia kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles