NA MWANDISHI WETU, Mtanzania Digital
JUMLA ya mapambano 16 yatarajia kupigwa katika fainali ya kumsaka Champion wa Kitaa wa ngumi za kulipwa, huku mabondia watakaopanda ulingoni na makocha wao kila mmoja akijinadi kuibuka kidedea.
Fainali hiyo ambayo itasindikizwa na mabondia mbalimbali akiwamo Dulla Mbabe atakayezichapa na Amour Sheikh, inatarajia kufanyika Machi 20, 2022 kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa utambulisho, Kocha kutoka kambi ya B. Combination, Mbagala, Babu Ally amesema siku hiyo vipaji vipya alivyotengeneza vitaonesha burudani na kuwataka wadau wa ngumi kujitokeza kwa wingi.
“Watu wamezoea kuwaona na kuwasikia kina Mfaume Mfaume, Mwakinyo na wengine, lakini siku ya fainali ya Champion wa Kitaa nimeandaa kitu cha tofauti na tutaondoka washindi,” ametamba Babu Ally.
Naye kocha Christopher Mzazi wa Mabibo, ametamba kuwa ameandaa mapambano makali hadi kupewa jina jipya la Rais wa Urusi.
“Huwa ninapewa majina mengi kutokana na kazi ninayofanya kuwatengeneza mabondia, sasa hivi naitwa Rais wa Urusi hivyo watu waje tarehe 20, waone kile nilichofanya, nimeandaa mabomu,” amesema Mzazi.
“Keko ndiyo sehemu ngumi zilipozaliwa, mimi nikilala huwa nawaza ngumi tu hadi kuna wakati naweza kuota nampiga kofi mke wangu,” amejinadi kocha Mohamme Mbwana wa Keko.
“Makocha wote wanajua kuwa Fire Stone ni moja ya walioongoza kuingiza mabondia wengi katika fainali hizi, tunahidi kuwa hata mtu akikosa kiingilio siku hiyo ajitokeze tu, sisi tutamlipia.
Kwa upande wa mabondi Dulla Mbabe amesema yeye mchezo huo ni kama anajaribu mitambo yake baada ya kukosekana ulingoni kutokana na kuumwa mguu.
Aidha bondia Kenedy Samweli ambaye litakuwa pambano lake la pili kucheza, amesema amejipanga kuondoka na ushindi dhidi ya mpinzani wake Sebastian Deo.
Kwa upande wake muandaaji wa mapambano hayo, Meja Seleman Semunyu, amesema fainali hiyo ikimalizika wanaelekea Morogoro kwa maandalizi ya pambano la Twaha Kiduku dhidi ya Alex Kambangu Raia wa DR Congo.