31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Samia aipongeza CRDB ataka taasisi nyingine kuiga mfano

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa mshirika mzuri wa mafanikio ya Serikali na sekta binafsi na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa benki hiyo.

Ametoa pongezi hizo leo Machi 5 wakati akizindua makao makuu ya benki hiyo na kusema kuwepo kwa sekta ya benki iliyo imara huchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira na kuongeza kipato.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, akimuonesha Rais Samia Suluhu ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya CRDB yaliyopo Barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji wa biashara ya kibenki si tu wa kigeni bali hata wa hapa nchini.

“Crdb imekuwa mfano mzuri wa ushirika wa mafanikio kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuwaletea wananchi maendeleo, niwapongeze na kuwatia moyo nendeni maeneo yote mnayohisi mnaweza kufanya kazi kwa sababu benki za nje zinakuja Tanzania kwanini sisi tusiende…nendeni kwa nguvu,” amesema Rais Samia.

Kuhusu jengo hilo lililogharimu zaidi ya Sh bilioni 100 ameipongeza Crdb na kuwataka wafanyakazi kuongeza ufanisi katika utendaji wao ili faida ikue maradufu.

“Nimelitembelea na kulikagua jengo ni la kisasa na limejengwa kwa ubora wa hali ya juu, linafaa kabisa kuwa makao makuu ya benki kubwa. Kuwa na jengo zuri ni jambo moja lakini ufanisi wa kazi ni jambo lingine, hivyo uzuri wa jengo na mazingira yaliyoboreshwa yatawafanya muongeze ufanisi wa kazi tunategemea faida zaidi mwakani,” amesema.

Pia amezitaka taasisi zingine kuiga mfano wa Crdb kwa kuwa waaminifu katika kulipa kodi kwani ndio uzalendo.

Takwimu za benki hiyo zinaonesha kwa miaka miwili imelipa kodi Serikalini ya Sh bilioni 430 huku pia ikitumia zaidi ya bilioni 3.2 kusaidia jamii katika sekta ya elimu, afya na majanga mbalimbali.

Katika hatua nyingine Rais Samia amezitaka benki na taasisi za fedha zitakazokopeshwa fedha kwa ajili ya kufufua uchumi ulioathiriwa na Uviko 19 zizingatie maelekezo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kukopesha kwa riba ndogo isiyozidi asilimia 10.

Julai 2021 BoT ilianzisha mfuko maalumu wenye thamani ya Sh trilioni moja kukopesha benki na taasisi za fedha riba nafuu ya asilimia 3 ili nazo zikakopesha sekta binafsi kwa riba isiyozidi asilimia 10 mwaka.

Tayari Benki ya CRDB imepunguza riba ya mikopo mbalimbali ikiwemo inayotolewa katika sekta ya kilimo hadi asilimia 9.

“Naomba sana isiende kulipa madeni ikatumike kwa kuwapa sekta binafsi ili waifanyie kazi, trilioni moja si fedha ndogo ziende zikafanye kazi kubwa, sina shaka zitaleta matokeo makubwa kwa sekta binafsi na mwananchi mmoja mmoja,” amesema Rais Samia.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Crdb imekuwa ya kwanza kuitikia wito wa kupunguza riba na kuwataka Watanzania kutumia benki na kuepuka kutumia taasisi bubu zenye riba ambazo si rafiki.

“Jengo hili ni la kihistoria siyo tu kwa benki hii bali kwa sekta nzima ya fedha, Crdb ni benki kiongozi hapa nchini na leo wamethibitisha hilo,” amesema Dk. Nchemba.

Kwa upande wake Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga, amesema sekta ya benki imeendelea kuimarisha uchumi wa nchi na kwamba nchi zingine zimeomba Tanzania ikawekeze kwao.

“Tunachokiona na kushuhudia leo ni kuimarika kwa ubora wa huduma za kibenki nchini, hatukutegemea tutafikia wakati tutakuwa na huduma za kibenki zenye ubora ambao leo hii unaonyeshwa na Crdb,” amesema Profesa Luoga.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Crdb, Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo ilyoanzishwa mwaka 1996 ina matawi zaidi ya 265 nchi nzima, mawakala 22,000 na huduma mbalimbali za kidigitali.

Amesema jengo hilo lililojengwa kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa lina vyumba vya mikutano 60, ukumbi mkubwa wenye uwezo wa kuchukua watu 200 na sehemu ya kutoa huduma kwa wateja maalumu.

“Kama mteja amesafiri kutoka Dodoma kuja Dar anataka kukutana na wawekezaji tuko tayari kumpa chumba cha mkutano bure akutane nao,” amesema Nsekela.

Kwa mujibu wa Nsekela, Crdb ndio benki kubwa iliyotoa mikopo mingi yenye thamani ya Sh trilioni 5.1 kwa wateja na sekta mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles