Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi nchini pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali wametoa onyo kali dhidi ya watu wanaopanga kuandamana.
Onyo hilo limetolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Nsato Marijani, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni.
Kwa nyakati tofauti, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, pia wamewahi kutoa onyo la maandamano hayo yanayoratibiwa kwenye mitandao.
Jana viongozi hao wenye dhamana na jeshi la polisi, walitoa kauli hizo hizo jijini Dar es Salaam wakati wakizindua vituo vya polisi vinavyohamishika.
Kwa upande wake  Mhandisi Masauni, alisema kuna watu nchini na wengine wako nje ya nchi wanachochea kufanyika kwa maandamano hayo kinyume cha sheria.
“Kuna watu ambao wako ndani ya nchi wengine kwa bahati wako nje ya nchi, hawa wanataka kukwamisha ajenda ya maendeleo, watupeleke kwenye ajenda zisizo za msingi za kufanya tofauti na ajenda tulizonazo.
“Utasikia mwingine anasingizia polisi kuwa katekwa kumbe kajiteka mwenyewe, mwingine anataka watu waandamane, yani watu waache kutumia fursa zilizopo kwa mfano jana Rais alizindua reli ya umeme ambayo mimi nilikuwa naiona Ulaya leo inajengwa Tanzania.
“Waache  kutumia fursa za viwanda vinavyoibuka kwa wingi kama uyoga eti wakaandamane. Ninachoweza kuwahahikikishia ni kwamba vyombo vyetu viko imara” alisema Masauni.
Alisema Jeshi la Polisi limejitahidi kukabiliana na vitendo mbalimbali vya uhalifu nchini licha ya kuwapo kwa changamoto mbalimbali ikiwamo kukosekana kwa vituo vya polisi vya kutosha na makazi bora ya askari.
Alisema matukio ya uhalifu nchini yamepungua kutokana na juhudi za vyombo mbalimbali vya usalama na wadau ambao wamekuwa wakisaidia kutoa visa kama sehemu ya ushikiri wao katika ulinzi wa raia na mali zao.
Kuhusu vituo hivyo sita vilivyokabidhiwa Mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Masauni alisema vitasaidia kukabiliana na matukio ya uhalifu katika mkoa huo ambao umekuwa ukiongoza kwa matukio ya uhalifu.
Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.