25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

UNYAMA MWINGINE

Na FREDRICK KATULANDA-MWANZA


MWILI wa mfanyabiashara na mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Josiah Mzuri, maarufu kama Super Sami, mkazi wa   Mwanza, umepatikana wilayani Bunda, Mkoa wa Mara.

Mwili huo ulipatikana juzi katika Mto Rubana, ukiwa umefungwa katika viroba na ukiwa umeharibika vibaya.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Mara, Jafari Mohamed, alisema mwili huo ulipatikana juzi jioni  katika mto huo ulioko mpakani mwa Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara na Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.

Kamanda alisema hadi jana walikuwa wakishikiliwa watu watano kutokana na upelelezi uliofanyika.

Kwa mujibu wa Kamanda,  baadhi ya wananchi waliokuwa mtoni hapo ndiyo waliuona mwili huo   ukiwa umefungwa kwenye kiroba ambao walitoa taarifa polisi waliofika na kuutoa ndani ya maji.

“Jana (juzi) jioni, wananchi waliona kiroba ndani ya Mto Rubana kikiwa kimefungwa na baada ya kukitilia shaka, walitoa taarifa polisi ambao walifika na kukivuta kutoka mtoni.

“Baada ya kubaini ni mwili na kwa kuwa kulikuwa na taarifa za ndugu wa Josiah kutafuta ndugu yao, tuliwasiliana nao kuja kuutambua na waliweza kuutambua kwamba ni wa ndugu yao ambaye ni mmiliki wa mabasi ya Super Sami,” alisema Kamanda Mohamed.

Mohamed aliwataka wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi  liweze  kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.

“Nichukue nafasi hii kuwaomba wananchi kwamba kama kuna mtu mwenye taarifa zinazohusiana na kifo cha ndugu Josiah, basi awasiliane nami moja kwa moja anieleze na ninawahakikishia tutakuwa na usiri wa hali ya juu kwa watoa taarifa wote,” alisema.

Kaka wa mfanyabishara huyo, Amini Mzuri, alikiri kuutambua mwili wa ndugu yake na kusema ulikutwa ukiwa katika hali mbaya kwa kuwa ulikuwa umeshaanza kuharibika.

“Tumeutambua ni mwili wa ndugu yetu, umepatikana Mto Rubana, lakini kwa sasa tunangojea uchunguzi wa kina wa mwili huo… nadhani baada ya hapo tunaweza kuongea lolote,” alisema.

Mfanyabishara huyo anadaiwa kutoweka Februari 27, mwaka huu nyumbani kwake eneo la Mwananchi, Buzuruga, Kata ya Mahina, Wilaya ya Nyamagana,   Mwanza.

Wakati anaondoka nyumbani kwake  alikuwa na gari lake   Nissan Patrol  namba   T 323 BSF ambalo lilipatikana Machi 9, mwaka huu  likiwa limeteketea kwa moto katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Pembeni mwa gari hilo, kulikuwa na panga na kiberiti ambavyo inasemakana viliwekwa na waliohusika na uhalifu huo.

Taarifa zilizopatikana zinasema wakati Josiah anaondoka Mwanza, alielekea katika mji mdogo wa Ramadi wilayani Busega, Mkoa wa Simiyu  kwa ajili ya shughuri ambazo hazijawekwa wazi.

Kaka wa marehemu alikaririwa akieleza kuwa siku hiyo ya Februari 27, mwaka huu, ndugu yake huyo baada ya kuondoka nyumbani asubuhi, usiku   saa 3.00 alimpigia simu mkewe akimweleza kuwa alikuwa njiani kurudi lakini alikuwa na mgeni.

Hata hivyo, ndugu huyo alisema   hakurudi nyumbani hadi Machi 9, mwaka huu, gari lake lilipopatikana likiwa limeteketea kwa moto.

“Tumefanikiwa kuuona mwili huo, nathibitisha ni wa ndugu yetu na hivi hapa tunavyoongea tunangoja uchunguziu zaidi wa utalaam, tupo Hospitali ya Mkoa wa Mara ambako mwili wake utafanyiwa uchunguzi.

Wakati hayo yakiendelea, Machi 9, mwaka huu, Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mara, Juma Ndaki, alieleza kwamba  baada ya gari la marehemu kupatikana walifanya uchunguzi wa awali na kujiridhisha kuwa ni mali ya mmiliki wa mabasi hayo ingawa miezi mitatu iliyopita, lilikuwa likimilikiwa na John Zephania.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles