22.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

JPM: WATU WENGINE WAMEANZA KULEWA AMANI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli amewatahadharisha baadhi ya watu walioanza kulewa amani wasiichezee kwa sababu ni kitu muhimu lakini chepesi kukiharibu.

Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza Sigara cha Philips Morris International kilichopo mkoani Morogoro.

“Amani huwa inalevya, kila kitu huwa kinalenya, ukila ugali sana au wali utalewa. Chochote ukila sana utalewa na amani ukikaa nayo sana kwa miaka 51…watu wengine wameanza kulewa,” alisema Rais Magufuli.

Alitoa mfano wa nchi za Iraq na Libya zilizokumbwa na machafuko yaliyosababisha kutoweka kwa amani na watu wake kukimbilia mataifa mengine.

“Wanashindwa kuelewa kwenye nchi kama Iraq unamuona mtoto amepigwa risasi amekufa, mtu alikuwa na nyumba yake amewekeza kwa mabilioni imebomolewa.

“Wanashindwa kuelewa wale walichezea amani, hata katika nchi za jirani zetu wanawaona watu wanakimbia wanavuka kwenye maji wako tayari wazame, hata Libya iliyokuwa nchi nzuri wanakimbilia Ulaya, wako radhi wakafie kwenye maji.

“Wanafikiri walihitaji hicho, kimewapata kwa sababu wamechezea amani, ukichezea amani umechezea maisha yako, unaweza ukafiriki wewe uko mbali lakini itakupata tu, isipokupata wewe itampata hata ndugu yako, shangazi au mjukuu wako,” alisema.

Aliwataka Watanzania kutunza amani kwa manufaa ya sasa na yajayo huku wakijifunza kutoka katika mataifa mengine.

“Amani yetu ndiyo italeta wawekezaji, hata mitume na bwana Yesu walihubiri amani, amani ni kitu muhimu sana lakini ni chepesi sana kukiharibu.

“Tufikirie tulikotoka, tulipo na tunakoelekea, tujitambue sisi na tutambue thamani ya taifa letu. Tumesimama kwa miaka 51 tukiwa na amani msifikiiri watu wanaweza kufurahi.

“Tumekaa kwa amani hakuna kelele, watu wengine wanajiuliza kwa nini Tanzania iwe hivyo, angalieni majirani zetu yanayowapata liwe funzo tusijaribu ku – test chakula ambacho hakiliki, tusikiharibu tunachokiunda tukiendeleze kwa faida ya watoto, wajukuu na taifa letu,’ alisema Rais Magufuli.

KIWANDA CHA SIGARA

Awali akizindua kiwanda hicho alisema sigara ambazo zilikuwa zinatengenewa nje sasa zitatengenezwa Morogoro na kwamba kitaisaidia kuondoa kero mbalimbali.

“Tunapokuwa na kiwanda kama hiki maeneo yote yanayolima tumbaku watakuwa na soko zuri la kuuza tumbaku zao,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Pia alielezea masikitiko yake kutokana na viwanda vingi vilivyoachwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kubinafsishwa, kutelekezwa na kufa.

“Mkoa wa Morogoro baada ya Uhuru ndiyo ulikuwa unaongoza kwa kuwa na viwanda vingi lakini ilifika mahali tulivisahau viwanda vyetu. Vingine tukaviua sisi wenyewe kwa kuweka kodi ambazo hazifai.

“Tumejifunza makosa haya tusiyarudie tena, unapokuwa na kiwanda kama kilikuwa kinatengeneza sigara baadaye kikafa maana yake umeua zao la tumbaku.

“Ukiwa na kiwanda ambacho kilikuwa kinatengeneza bidhaa za pamba halafu kikafa maana yake hutakuwa unalima pamba.

“Kama ulikuwa na kiwanda kama Moproco (cha kutengeneza mafuta ya kula) na baadaye ukakiua maana yake umeua ajira za Watanzania,” alisema.

Alisema viwanda ni suala mtambuka kwani vinasaidia kuimarisha uchumi wa nchi kwa kutoa ajira, kusaidia Serikali kukusanya kodi na kuboresha maisha ya wananchi wengi.

“Nakupongeza sana Mansoor kwa kuamua kuwekeza, tunahitaji wawekezaji wa namna hii katika nchi yetu.

“Ulipokuwa Mwanza nilibomoa eneo lako lililokuwa kwenye hifadhi ya barabara lakini leo nakupongeza kwa dhati…yaliyopita si ndwele tunaganga yaliyopo na yajayo,” alisema.

Pia aliwataka watendaji kuanzia mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kutengeneza mazingira mazuri ya kusaidia wawekezaji kuwekeza.

“Nimekwishatoa maelekezo kwa Waziri wa Viwanda na Waziri wa Fedha waangalie kodi zinazoleta kero kwa ajili ya viwanda vyetu.

“Mheshimiwa Mwijage nakupongeza kweli unafanya kazi, siku za nyuma kidogo nilikasirika lakini sasa unafanya kazi, naviona viwanda vinavyofunguliwa, viongozi sasa wananielewa akiwemo Mwijage,” alisema.

KERO

Mmoja wa wakazi wa Morogoro aliyekuwepo katika uzinduzi huo aliyejitambulisha kama Avintishi alilalamikia kamata kamata inayofanywa na mgambo wa Manispaa na kuwatoza faini alizodai ni kubwa bila kurudishiwa bidhaa zao.

Mama huyo alisema hufanya biashara zake katika kituo cha daladala Morogoro Mjini.

“Wakubwa zetu hawatuthamini, tunafanya biashara zinachukuliwa tunakwenda kulipa faini halafu biashara hupewi,” alisema Avintishi.

Mkurugenzi wa Manispaa alipotakiwa kutoa ufafanuzi alisema wameweka mpango wa kuwasaidia wafanyabiashara ndogondogo na kwamba tayari wametengeneza minada minne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,305FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles