25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

MAANDAMANO YAKIRUHUSIWA YANAWEZA KUUA UPINZANI


Na. M. M. Mwanakijiji

HAKUNA sababu ya msingi ya kuzuia maandamano ya kisiasa Tanzania. Mikusanyiko ya mikutano ya kisiasa haihitaji kufanywa iwe migumu kiasi kwamba ionekane Serikali haina uwezo wa kusimamia ulinzi wa wananchi katika mikutano hiyo.

Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vinalipwa fedha nyingi kwa kodi za Watanzania kwa ajili ya kuhakikisha usalama wao na sehemu mojawapo ya usalama huo ni kuhakikisha shughuli za kisiasa zinafanyika kwa njia ya amani.

Mikusanyiko ya kisiasa hata kama ni maandamano. Kwamba, watu wanaogopa maandamano au mikutano mikubwa ya kisiasa eti kwa sababu inatishia amani ni sababu dhaifu kabisa ya kusitisha maandamano Tanzania. Ni sawa na kuamua kutompeleka mtoto shule kwa sababu hesabu ngumu!

Ni sawa na kuamua kujenga seng’enge kwenye nyumba yako na kuhakikisha kuwa watoto hawatoki nje kwa sababu nje kuna matatizo mengi kwenye jamii. Mzazi yeyote anajua kwa hakika kabisa sehemu ya kukomaa kwa mtoto ni pamoja na kukutana na mambo mbalimbali ya maisha.

Kama kila mtu angekuwa anaogopa yale yatakayomkuta, basi watu wasingekuwa wanapanda magari kwa kuogopa ajali, au kwenda mahali kwa kuogopa jambo lisilojulikana. Hata hivyo, watu pamoja na kujua jambo lolote linaweza kutokea wanaamua bado kupanda magari na kwenda mahali na safari.

Sasa kwanini watu waogope maandamano na mikusanyiko ya kisiasa kama watoto waliodekezwa? Kwanini Jeshi la Polisi, lenye maofisa waliosomea kazi ya kulinda amani, na kipo kabisa kikosi chenye vifaa mbalimbali kinachojulikana kama kikosi cha kutuliza ghasia na bado watu wanaogopa mikusanyiko. Sasa hiki kikosi jukumu lake ni kuzuia nini; kimekuwa ni kikosi cha kuzuia hisia?

Maandamano ya kisiasa, mikusanyiko ya kisiasa ni haki ya msingi ya raia. Lakini vyama vya siasa na wanasiasa wana jukumu la kuhakikisha mikutano yao wanayoipanga na maandamano yoyote wanayoyapanga yanafanyika kwa njia ya amani na pale ambapo hilo linashindikana, Jeshi la Polisi lina wajibu na ulazima wa kuingilia kati.

Sasa, kila siku tunasikia jeshi linapiga marufuku maandamano, mara liingilie kati na kukamata watu eti kwa vile wamekutana kisiasa (wengine hata misibani) ni kwa woga gani huu? Ni nani mwoga wa watu kukutana kiasi kwamba wanapiga mkwara hata watu kuandamana ndani ya vyumba vyao?

Tatizo ninaloliona ni kuwa, kuna imani iliyokosewa kuwa maandamano ni haki ya upinzani peke yake. Kwamba, wanaotakiwa kuandamana au wenye uwezo na nia ya kuandamana ni wapinzani peke yao. Hili si kweli. Wenye kuunga mkono Serikali au chama tawala nao wana haki ile ile ya kuonyesha hisia zao kwa njia ya maandamano ikibidi.

Ni kwa sababu hiyo, naamini kabisa kuwa kama Rais John Magufuli na serikali yake wakiamua kuruhusu maandamano hata mara moja hivi kwa vyama vya upinzani, wana uwezo wa kuua kabisa upinzani. Hii ni kwa sababu, tumejifunza kwenye nchi nyingine hili.

Baada ya jaribio la kumpindua Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki kulikuwa na maelfu ya watu waliojitokeza kuunga mkono jambo lile. Hata hivyo, baada ya jaribio lile kushindwa maelfu zaidi ya watu walijitokeza kusimama na Rais wao ambaye kwa kiasi kikubwa kimtazamo na mwelekeo anashabihiana na Rais Magufuli.

Chini ya Rais Erdogan, Uturuki imepiga hatua za haraka za maendeleo katika nyanja mbalimbali. Imefanya hivi hata hivyo kwa gharama kubwa ya demokrasia na upinzani na uminyaji wa uhuru wa habari na maoni. Hili nitalielezea wakati mwingine kuhusiana na chaguo la Rais Magufuli.

Kwa nchi yetu hata hivyo, naamini kabisa kuwa endapo Rais Magufuli na serikali wataamua na wenyewe kushindanisha maandamano kati ya wale wanaompinga na wanaomuunga mkono, kuna uwezekano mkubwa wanaomuunga mkono wakawa wengi kiasi kwamba anaweza kupata nguvu nyingine kabisa ya mabadiliko anayoyataka.

Rais Erdogan yeye alikwenda mbali zaidi na kuitisha kura ya maoni ili kuhalalisha mabadiliko makali ya Kikatiba aliyoyataka nchini mwake. Je, upinzani utakuwa tayari kama Rais Magufuli ataamua kuitisha kura ya maoni kuhusiana ama na mabadiliko ya Katiba ambayo yatampa nguvu zaidi ya alizonazo sasa?

Ni kweli maandamano ni haki ya kidemokrasia, lakini kama wingi wa watu na kura peke yake ndiyo sababu ya wanasiasa kufuata mwelekeo fulani, upinzani Tanzania usije ukajikuta unatengeneza mtego wake wenyewe, mtego ambao wakinasa itakuwa vigumu sana kujitegua.

Jambo la msingi sasa hivi kwa upinzani ni kukaa chini na kujiuliza wafanye nini na Rais ambaye ana mwelekeo mkali wa maendeleo? Wafanye nini na Rais ambaye yuko tayari kutoa kafara demokrasia ili Tanzania iendelee?

Swali jingine nalo bado linasimama; hivi ni kweli kabisa vyombo vyetu vya usalama havina uwezo, nyenzo, utaalamu, weledi na ujasiri wa kusimamia maandamano ya kisiasa nchini kiasi kwamba yanapigwa marufuku hewani?

Hapa patakuwa patamu.

Niandikie: [email protected]

www.zamampya.com

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles