27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: Sawasawa

IMG_0906[1]Na Waandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimezindua  kampeni za Urais Zanzibar  kwa kishindo huku mgombea wake, Maalimu Seif Sharif Hamad, akiahidi ajira kwa Wanzibari wote ndani ya miaka mitano na kubadilisha uchumi wa nchi hiyo kuwa imara kama ule wa Singapore.

Akizungumza na maelfu ya wananchi wa visiwa hivyo waliojitokeza jana kwenye uwanja wa Kibanda Maiti Unguja, Maalim Seif alisema endapo atapatiwa ridhaa ya kuongeza nchi, atapigania pia mamlaka kamili ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kupata katiba inayotambua Muungano wenye usawa.

Ndoto yangu ya kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki ipo palepale, nitahakikisha tunakuwa na uchumi imara ambao utakuwa unakua kwa haraka,”alisema Maalim Seif.

Alisema   katika uongozi wake atahakikisha nchi hiyo inajenga bandari  ya kisasa  kwa vitendo na si maneno kama wanavyofanya wengine.

Alisema pia kuwa serikali inayomaliza muda wake ilikuwa na mipango ya kujenga Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na kuahidi kuuzindua Oktoba mwaka huu lakini dalili zinaonyesha suala hilo halitawezekana.

“Airport (uwanja wa ndege) ilisemwa itazinduliwa Oktoba lakini juzi nilitembelea ujenzi wa uwanja huo inaonekana haiwezekani,”alisema Maalim Seif.

Alisema uboreshaji wa miundombinu ya Zanzibar   ikiwa ni pamoja na bandari, kutafanya watu wawe wanafika visiwani hivyo kununua bidhaa kama ambavyo sasa wanapoenda Dubai.

Alisema serikali yake pia itafungua Benki ya Uwekezaji ya Zanzibar(ZIB) ambayo itakuwa inatoa mikopo  kwa watu mbalimbali wakiwamo vijana lengo likiwa ni kuwapa mitaji watu wote.

“Benki itakuwa inatoa mikopo ya masharti nafuu, lengo ni kuwasaidia vijana wasiokuwa na mitaji kujiendesha katika maisha,”alisema Maalim Seif na kuongeza:

“Hakuna jambo linaloniuma kama kuona vijana wakiwa wanarandaranda (kutembea)barabarani, matumaini yangu nikimaliza miaka mitano kutakuwa hakuna mtu asiyekuwa na ajira,”alisema Maalim Seif.

Akizungumzia    mafuta na gesi, alisema ataanzisha wizara maalumu ya kushughulika na nishati hiyo na kwamba ndani ya siku 100 atakuwa ametengeza sheria na sera yake  wananchi waweze kuonja matunda yake.

 

Muungano

kuhusu muungano alisema ahatakikisha visiwa hivyo vinapata  mamlaka kamili  viweze kufanya uamuzi kwa masuala yanayowahusu.

“Wazanzibari wanataka kuona nchi yao imepata mamlaka kamili, walio madarakani  hivi sasa wameshindwa, zimefanyika  juhudi za kuleta Tume ya Jaji Joseph Warioba  kwa kukusanya maoni.

“Mlio wengi mlitaka muungano wa mkataba lakini tume wakasema tupate serikali tatu  kwa bahati mbaya CCM waliikataa na kuweka vitu vyao.

“Hata waliokuwa mbele katika mambo hayo walishindwa kuitetea Zanzibar na badala yake walipofika huko waliufyata wakaandaa rasimu yao wakakubali Zanzibar iendelee kudhalilishwa”.

Alisema endapo atachaguliwa yeye pamoja na mgombea urais wa Muungano, Edward Lowassa, watashirikiana na kuhakikisha wanaitisha upya bunge la katiba  na kurudisha maoni ya wananchi ambayo yataelekeza kuwapo   serikali tatu ambazo zina mamlaka.

 

Misingi ya utawala bora

Maalim Seif alisema atahakikisha  anaimarisha  misingi ya utawala bora ambayo itazuia Wazanzibari kunyanyaswa na kuteswa ndani ya nchi yao.

“Mambo  ya watu kuvaa soksi usoni wanapiga watu mwisho Oktoba 25, siwezi kukubali Wazanzibari wanadhalilishwa ndani ya nchi yao,”alisema Maalim Seif.

Alisema pia hataruhusu Mzanzibari aliyefanya kosa visiwani humo  kwenda kusomewa mashtaka Tanzania Bara.

“Mahakama ya Dar es Salaam na Zanzibar ni sawa ila leo wameamua kuwatoa watu huku kuwapeleka huko, nasema watarudi kama wana makosa watahukumiwa huku kwa mahakama ya Zanzibar,”alisema Maalim Seif.

 

Lowassa alaani uchanaji mabango yake

Naye Mgombea urais wa   Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),  Edward Lowassa, amekemea vikali tabia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuchana mabango yake akisema ni kinyume na sheria.

Alisema katika kipindi hiki cha kampeni, mambo mengi yanaweza kujitokeza hivyo wanachama hao wanapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu   kuepusha matatizo.

Alisisitiza kauli yake kuwa Ukawa wataendelea kufanya kampeni za ustaarabu  kuhakikisha wanapata ushindi kwa sababu uwezo huo wanao huku akiwataka CCM kuacha tabia ya kufikiria kuiba kura.

“Siku hizi wameanza tabia ya kuchukua mabango yetu na kuyaangusha, wakimaliza wanayatupa porini, nawaambia waache kabisa mchezo huo, sisi tutandelea kufanya kampeni za ustaarabu  kuhakikisha tunapata ushindi kwa sababu uwezo tunao.

“Mtanipa kura…? Wangapi watamchagua Lowassa…wanyooshe mikono juu, uwezo wa kushinda tunao, ninawaambia CCM waache kuiba kura,”alisema Lowassa.

Lowassa pia alimzungumzia mgombea urais wa Zanzibar  wa Chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ni kiongozi aliyepigania ukombozi wa taifa hilo hivyo anapaswa kuungwa mkono   aweze kupata ushindi.

Naye Mwasisi wa CCM, Mzee Nassoro Moyo alisema Wazanzibari wanaopenda amani na utulivu hawana budi  kuwachagua wagombea wa CUF waweze kupata ushindi na kuwaletea wananchi maendeleo.

“Kama kuna Mzanzibari anapenda amani na utulivu, anapaswa kuwapigia kura ya ndiyo viongozi wa CUF  waweze kuendeleza amani,”alisema Mzee Moyo.

 

NCCR-MAGEUZI

Katibu Mkuu wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema   CCM kimekuwa kikikataa kutoa ushindi kwa CUF lakini mwaka huu kitautoa kulingana na wanavyotaka wenyewe.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu aliwataka Wazanzibari wasijisahau kwa madhira na kero zilizofanywa na CCM, hivyo wafanye uamuzi mgumu  kuhakikisha wanapata ushindi.

“Wazanzibari tusijisahau kwa matatizo yetu yaliyotukuta, tunapaswa kuwa bega kwa bega   kuhakikisha tunapata ushindi,”alisema Mwalimu.

Naibu Katibu Mkuu  wa CUF Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu alisema leo ni siku ya kumbukumbu kwa wananchi waliofariki dunia kwenye meli ya MV Spice Islanders ambayo imetimiza miaka minne tangu ilipozama katika Bahari ya Hindi.

Ilivyokuwa

VIWANJA vya Kibanda Maiti jana vilifurika umati wa watu waliokuja kushuhudia uzinduzi wa kampeni za mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Maalif Seif Sharif Hamad.

Mkutano huo uliopangwa kuanza saa 9:00 alasiri, lakini kuanzia saa 4:00 asabuhi tayari baadhi ya wanachama wa chama hicho walianza kuwasili uwanjani hapo.

Ilipotimu saa 7 mchana uwanja huo ulikuwa umefurika umati wa watu huku wengine wakigombea mahali pa kukaa.

Makundi mbalimbali ya vijana walikusanyika uwanjani hapo huku wakiimba nyimbo mbalimbali, huku baadhi yao walikuwa wakipeperusha bendera za CUF na zile za chama cha zamani cha Afro Shirazi (ASP).

Hata hivyo vikundi mbalimbali vya ngoma navyo havikuwa nyuma, ambapo wasanii walijipanga wakituimbuiza nyimbo mbalimbali za kuisifia CUF na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Vikundi hivyo vya ngoma vilikuwa vikiimba “Mwaka huu tumeamua, CCM hata wafanye nini sisi tumeamua kuwapa kura zetu Seif na Lowassa, tuna imani mabadiliko yataletwa na ninyi, kura zetu tutawapa…CCM waone kinguzungu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles