28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mtoto wa Wasira anusurika kuchomwa moto Bunda

Mh.StephenWassiraNa Shomari Binda, Bunda

MGOMBEA ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya, amesema amemwokoa mtoto wa Waziri wa Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, aliyetaka kuchomwa moto ndani ya nyumba na wananchi kwa madai ya kugawa rushwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bunda jana, Bulaya alisema mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la  Kambarage, alikumbana na mkasa huo juzi kwenye Kata ya Kunzugu eneo la Bukore.

Alisema Kambarage akiwa na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wengine, wakiwamo watumishi wa Serikali, walifungiwa ndani ya nyumba na wananchi na kutaka kuwachoma moto baada ya kugundua kwamba walitaka kuwapa baadhi ya vijana rushwa ili wafanye fojo kwenye mkutano wake.

Bulaya alisema wananchi wa Bukore baada ya kuwafungia watu hao ndani ya nyumba, kabla ya kuchukua uamuzi wa kuwachoma moto, baadhi yao walimpigia simu ndipo alipochukua askari na kwenda eneo hilo.

“Nimewaita leo ili niwaeleze hali ambayo imetokea hapa jimboni, kuna watu ambao tukikaa kimya wanaweza kusababisha hali ya amani ikapotea hapa.

“Jana (juzi), mtoto wa Wasira na wenzake nimewaokoa wakitaka kuchomewa moto ndani na wananchi ambao walipata taarifa zao za kukutana ili wawape watu rushwa waje kufanya fujo kwenye mkutano wangu ninaopanga kuufanya Bukore.

“Mambo haya lazima yaangaliwe na vyombo vya usalama, wananchi hawataki kuona mambo ya ajabu,” alisema Bulaya mbele ya waandishi wa habari.

Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (Takukuru), Wilaya ya Bunda, Alex Mpenda, alikiri kutokea kwa tukio hilo.

Alisema walipofika eneo walipofungiwa watu hao, walikuta tayari wameshaondolewa na askari polisi waliofika hapo mapema.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Wilaya ya Bunda, Daniel Charles, alisema zipo taarifa za vijana zaidi ya 15 kutoka nchini Kenya, kuingizwa wilayani humo ili kuweza kufanya vurugu kwenye mikutano yao.

Alivitaka vyombo vya dola vifuatilie taarifa hizo na kuzifanyia kazi kwa sababu hadi sasa vijana wanne wanaokiunga mkono chama chao wameshavamiwa kwenye maeneo tofauti ya jimbo hilo na kukatwa mapanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philip Kalangi, alikiri kuwapo kwa tukio hilo ambapo alisema walipigiwa simu na wananchi wakieleza kuwa kuna watu walikuwa wamefungiwa kwenye nyumba.

“Tulikwenda eneo la tukio na kuwachukua watu hao, na tulipowafikisha kituoni mtu mmoja ndiye aliyeripoti kushambuliwa na watu wasiojulikana ni wa chama gani.

“Jeshi la Polisi halina taarifa za rushwa, suala hilo lifuatiliwe na Takukuru wakati polisi wakiendelea na uchunguzi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles