29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: JK tatizo Z’bar

m1*Adai alibariki kufutwa Uchaguzi Mkuu

*Jaji Mkuu Kenya, LHRC washauri utatuzi

Na Waandishi Wetu, Zanzibar/Dar

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amemvaa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete na kudai kwamba alibariki kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Amesema kiongozi huyo hana nia njema kwa Wazanzibari, huku akiwataka wananchi waliokiunga mkono chama hicho kutembea kifua mbele kwani wao ndio walioshinda uchaguzi huo aliouita halali kwa mujibu wa sheria.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini Unguja, alipokuwa akizungumza na viongozi wa CUF wa ngazi za majimbo na wilaya zote, ambapo alikuwa akifafanua maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho, ambalo liliazimia kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufanyika Machi 20.

Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais kupitia CUF, alisema uchaguzi umeshafanyika na kukamilika tangu Oktoba 25, mwaka jana na kuthibitishwa na waangalizi wote kuwa ulikuwa uchaguzi huru na wa haki.

Aliwataja waangalizi hao ni pamoja na wale wa Jumuiya ya Madola (The Commonwealth), Umoja wa Ulaya (European Union), Umoja wa Afrika (African Union), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na waangalizi kutoka nchi za Marekani na Uingereza.

 

KOMBORA KWA JK

Katibu huyo wa CUF, alidai kuwa kitendo cha kupindua maamuzi ya Wazanzibari kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kilifanywa kwa baraka zote na Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete.

“Kitendo cha kupindua maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya kupitia Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 kilifanywa kwa baraka zote za aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati huo, Jakaya Kikwete. Hakuna mtu mbaya kwa Zanzibar na Wazanzibari kama Jakaya Kikwete.

“Na hapa ninasema wazi msimamo wa CUF hadharani kwamba uchaguzi wa marudio si halali na si ufumbuzi wa mkwamo wa uchaguzi uliopo na uchaguzi ulishafanyika tangu tarehe 25 Oktoba, 2015,” alisema Maalim Seif.

Pamoja na hali hiyo, alidai kushangazwa na baadhi ya watu kusema kwamba Rais Dk. John Magufuli hana mamlaka ya kuingilia Uchaguzi wa Zanzibar.

Msimamo huo wa Maalim Seif unakuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, kusema kuwa Rais Magufuli hana mamlaka ya kikatiba kuingilia suala hilo.

Jaji Lubuva alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli.

Hatua hiyo ilimfanya Maalim Seif kuipinga na kusema wanaodai hilo hawatambui wajibu na mamlaka ya kiongozi wa nchi kwa mujibu wa sheria.

“Kwa hivyo, anasema kudai kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano hana mamlaka kuliingilia kati suala la Zanzibar, ni unafiki wa hali ya juu,” alisema Maalim Seif.

 

VIKAO VYA MWAFAKA

Mwanasiasa huyo alitumia kikao hicho kueleza kwa kina yaliyojiri katika vikao tisa vya mazungumzo kati yake na Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na marais wastaafu na kuweka wazi kwamba mazungumzo hayo hayakufanikiwa na kudai kwamba kiongozi huyo hana nia njema na si mkweli.

“Dk. Shein ni mtu anayeamini kutawala kwa mabavu na matumizi ya nguvu na asiyejali wala kuheshimu Katiba. Kwa hali hii ya sasa wana-CUF tembeeni kifua mbele mkijua kwamba nyie ndiyo washindi halali wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

“Na hapa nasisitiza tena kwamba msimamo wa CUF kama ulivyotangazwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa uko palepale,” alisema Maalim Seif.

 

TAMKO LA MABALOZI

Januari 29, mwaka huu mabalozi wa nchi zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) walieleza kusikitishwa na kitendo cha ZEC kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio visiwani humo,  wakati mazungumzo ya kutatua mgogoro yakiendelea  ambapo walimtaka Rais Magufuli kutumia nafasi yake ya uongozi kutatua sintofahamu hiyo ya kisiasa.

Taarifa ya pamoja iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mabalozi hao, pia inamtaka Rais Magufuli kuendeleza wito wake wa kuzitaka pande zote zitafute suluhu kwa amani.

Kutokana na sakata hilo, mabalozi hao wamelaani kitendo hicho wakisema kurudia uchaguzi kwa kigezo kuwa utaratibu ulikiukwa, kinawatia wasiwasi kwa kuwa ZEC haikutoa ushahidi wa ukiukwaji huo.

Mabalozi hao walisema katika tamko lao kuwa ZEC imerudia kauli yake ya kuwa uchaguzi ulikiuka taratibu licha ya waangalizi kutoka EU, Jumuiya za Afrika Mashariki, SADC, Marekani na Jumuiya ya Madola kufanya tathmini na kujiridhisha kuwa ulikuwa huru na haki.

Taarifa hiyo iliyotumwa kwa ushirikiano wa mabalozi wa Uholanzi, Norway, Hispania, Italia, Ujerumani, Finland, Ufaransa, Sweden, Uswisi, Uingereza, Ireland na Marekani inasisitiza kuwa kitendo cha upande mmoja kuamua kurudia uchaguzi kinaweza kuzidisha hofu na taharuki miongoni mwa Wazanzibari.

Hata hivyo, mabalozi hao wamesema kulingana na mazingira ya Zanzibar kwa sasa, itakuwa vigumu kwa waangalizi wa kimataifa kutegemewa kushiriki kwa namna yoyote katika uchaguzi huo.

 

JAJI MKUU WA KENYA

 

Jaji Mkuu wa Kenya, Dk. Willy Mutunga amesema masuala ya kisiasa Zanzibar yanatakiwa kumalizika kwa mazungumzo ili Muungano usivunjike.

Jaji Mutunga alisema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kuhusu mageuzi ya mahakama nchini Kenya.

Alisema Wakenya wanafahamu msimamo wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na siasa yake nzuri iliyokuwa ikijali masilahi ya wengine.

“Mambo ya Zanzibar yanatakiwa kuingia katika mazungumzo, Muungano hautakiwi kuvunjika kwani ukivunjika tutazungumza vipi Muungano wa Afrika.

“Lazima mjadiliane na mkubaliane kuhusu rasilimali na wananchi watanufaikaje nazo,” alisema.

 

KATIBA

Akizungumzia Katiba mpya, alisema majadiliano yakiendelea Watanzania watapata Katiba waitakayo.

“Katiba si sheria peke yake, inagusa mpaka rasilimali, kodi na masilahi ya Watanzania. Mfano Mtwara kuna gesi wananchi wanataka kujua watanufaika vipi,” alisema.

Alisema nchini Kenya Katiba mpya imewaingiza katika mageuzi ya kuteua majaji ambapo zamani majaji walikuwa wakiteuliwa na rais.

Jaji Mutunga alisema sasa hivi wananchi lazima wahusishwe katika kupatikana kwa majaji, sifa za majaji zifuatiliwe na endapo wananchi wana maoni kuhusu majaji hao, wanafika katika shirika linaloajiri majaji kueleza kuwa hawafai.

Alisema jaji mkuu ili ateuliwe kushika nafasi hiyo, jina lake lazima lifikishwe bungeni kujadiliwa na anatakiwa awe amefanya kazi za kisheria kwa miaka 15 na akiwa na kesi za kuharibu sifa zake hawezi kuteuliwa.

Jaji huyo alishauri wananchi washirikishwe katika mchakato wa kuwapata majaji.

Katika upande wa usikilizwaji wa kesi, alisema mahakama za Tanzania zinafanya vizuri zaidi kuliko Kenya katika kuamua kesi nyingi.

Alitolea mfano Kenya kulikuwa na kesi tatu zilizokaa mahakamani kwa miaka 35, hivyo hata wao itakuwa vizuri kama wakisikiliza na kuamua kesi kwa miaka miwili hadi mitatu.

 

LHRC WAMKOMALIA JECHA

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimemtaka Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kujiuzulu kutokana na kutoa matamko yaliyokiuka haki za binadamu na kuvuruga amani ya Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Imelda Urio, alisema hatua ya Jecha kufuta uchaguzi bila kufuata sheria kunampuguzia sifa ya kuongoza tume na ni kiashiria cha wananchi kukosa imani naye, hivyo ni hekima ajiuzulu mwenyewe.

“Kituo kilisikitishwa sana na utaratibu wa kufutwa na kutangazwa kwa uchaguzi wa marudio kwani unakiuka haki za binadamu na misingi ya demokrasia na utawala bora, hivyo kuwanyima Wazanzibari viongozi wanaowataka,” alisema Urio.

Alisema hatua ya ZEC kufuta na kutangaza tarehe ya kurudia uchaguzi bila maridhiano ya vyama vya siasa na wadau kutaongeza chuki na uhasama, hivyo kuhatarisha amani visiwani humo.

Urio alisema kuwa ukosekanaji wa taarifa ya mchakato wa maridhiano tangu kufutwa kwa uchaguzi kumeondoa imani ya wananchi kwa viongozi wao.

Alishauri kuwa ZEC isipewe nafasi ya kusimamia tena uchaguzi kwani imeonyesha dhahiri kukosa sifa ya kufanya kazi hiyo.

Aidha alishauri kutafutwa kwa mpatanishi huru wa ndani na nje ili kusaidia majadilino na kuweka mikakati ya uchaguzi ulio huru na haki.

Alisema kwa mujibu wa sheria, Rais Magufuli ana mamlaka kamili kuingilia mgogoro huo kwani yeye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles