25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MAALIM SEIF AANDIKA WARAKA MZITO

Na MWANDISHI WETU – dar es salaam

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amemtuhumu Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuwa ana ajenda yake ya kukisambaratisha chama hicho.

Maalim Seif ametoa tuhuma hizo kupitia waraka wake alioutuma kwa msajili huyo, Agosti 16, mwaka huu.

Pamoja na kuzungumzia mambo mbalimbali yanayosababisha mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho, Maalim Seif amemtuhumu msajili kwamba amenuia kukivuruga chama hicho kwa sababu kinaihangaisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Inasemekana kuwa unazungumza kwamba yanayotokea katika Chama cha CUF eti ni kumuhangaisha Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF, kwa sababu eti bwana huyo anaihangaisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kiasi kuwa serikali hiyo haiwezi kufanya shughuli zake.

“Kama hilo ndilo lengo, la kujiuliza inakuwaje msajili, tena akiwa Jaji wa Mahakama Kuu, anajiingiza katika mambo ya siasa? Naomba ujue kuwa fanyeni mnayoyafanya, kabisa hamtaweza kuwatoa Wazanzibari katika kudai haki yao ya ushindi mnono walioupata katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa 25 Oktoba, 2015,” ameeleza katika waraka huo.

Maalim Seif alisema kuwa Wazanzibar wataendelea kuidai haki yao hadi waitie mikononi, hivyo njama za Profesa Lipumba na genge lake la kutaka kumfukuza hazitazuia haki kupatikana.

“Mnajiadhirisha tu mbele ya macho ya Watanzania na dunia kwa ujumla,” alisema.

Katika hatua nyingine, ameeleza kushangazwa na uamuzi wa msajili huyo, kukubali Magdalena Sakaya kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu wa CUF.

“Nashangaa, tena nashangaa sana, kwa maelezo yako hayo. Mimi ninavyojua ni kuwa kiongozi anakaimiwa ikiwa hayupo nchini au hawezi kutekeleza majukumu yake. Hivyo ndivyo Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014) kifungu cha 105 (1) kinavyoeleza.

“Hapo ulipopokea barua ya Profesa Lipumba ya Machi 16, mwaka huu nilikuwepo nchini nikiwa nafanya kazi za chama makao makuu ya chama, tena nikiwa mzima wa afya na akili timamu.  Wewe umetoa uamuzi kutokana na hiyo barua ya Profesa Lipumba kwa madai kuwa eti siendi Ofisi Kuu Buguruni.
“Tafadhali angalia Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014) kifungu Na. 1 (2) ambacho kinaeleza ifuatavyo: (2) Makao Makuu ya chama yatakuwa katika mji mkuu wa Zanzibar na anuani yake itakuwa kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa. Kifungu cha 1 (3) kinaeleza ifuatavyo: Kutakuwa na Ofisi Kuu ya Makao Makuu ya chama mjini Dar es Salaam na anuani yake itakuwa kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa,” alieleza Maalim Seif.

Alifafanua kuwa hakumbuki kama mkutano mkuu ambao ndio wenye madaraka ya kufanya maamuzi yoyote yanayohusu chama, umewahi kubadilisha kifungu hicho cha Katiba ya CUF.

Hivyo anaamini kwamba Makao Makuu ya chama yako katika mji mkuu wa Zanzibar katika Mtaa wa Mtendeni.

“Je, ulijiridhisha kuwa sifanyi kazi katika Makao Makuu ya Chama? Mimi nikiwa Katibu Mkuu wa chama, nimeendelea kufanya kazi zangu za kichama sio tu katika Zanzibar, lakini pia hata katika Tanzania Bara, ingawa ni wazi kuwa juhudi zimefanywa na Profesa Lipumba na genge lake, wakiungwa mkono na ofisi yako na Jeshi la Polisi kunizuia nisifanye kazi kwa uhuru katika enea la Tanzania Bara.

“Vyombo vya habari nchini vimekuwa vikitoa taarifa juu ya shughuli za kichama ninazoendelea kuzifanya Zanzibar na Bara, lakini pia na mazuio ninayowekewa na Jeshi la Polisi kunizuia nisifanye shughuli Tanzania Bara,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles