24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

SAKATA LA BOMBARDIER: LISSU, SERIKALI HAPATOSHI

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kusema ndege ya tatu aina ya Bombardier Q400 iliyotarajiwa kuwasili nchini  mwishoni mwa mwezi Julai imekamatwa nchini Canada, Serikali imejitokeza na kukiri jambo hilo.

Kwa mujibu wa Lissu, ndege hiyo imekamatwa kwa  amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, baada Kampuni ya Stirling Civil Engineers Ltd  kuidai  Serikali Dola za Marekani milioni 38.7 (Sh bilioni 87) kutokana na hatua yake ya  kuvunja mkataba wa ujenzi wa barabara kutoka  Wazo Hill, Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani mwaka 2009.

Akizungumza na waandisi wa habari kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Zamaradi Kawawa, alikiri kuwapo kwa mgogoro katika ununuzi wa ndege hiyo, ambao umechangiwa na kesi iliyopo mahakamani iliyosababisha kuzuiwa.

“Mgogoro huo upo, lakini kimsingi umetengenezwa na Watanzania wenzetu baada ya kuweka masilahi ya kisiasa badala ya kuweka mbele ya taifa,” alisema Zamaradi.

Alisema kutokana na mgogoro huo, kampuni husika ambayo hakuitaja kwa jina, imepeleka kesi mahakamani na kuweka zuio lililoelekeza ndege hiyo isiondolewe hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Ingawa pia Zamaradi hakuitaja mahakama ambayo imeweka zuio hilo, licha ya kulazimishwa na waandishi wa habari kufanya hivyo, alisema baadhi ya wanasheria waliokwenda kufungua madai hayo dhidi ya Serikali ya Tanzania na kusababisha ndege hiyo kushikiliwa, hawana uhalali wowote wa kufanya hivyo.

“Wanasheria hao ni matapeli tu ambao wamesukumwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wasioitakia mema nchi yetu,” alisema.

Pasipo kuwataja majina, Zamaradi alisema mgogoro huo umechochewa na wanasiasa wasio wazalendo waliopo nchini, kwa lengo la kukwamisha jitihada za Rais Dk. John Magufuli.

Alisema Serikali ilishapata fununu ya uwapo wa baadhi ya viongozi wa chama cha siasa ambao hata hivyo hakuwataja majina, waliokuwa na mpango wa kuzuia ndege hiyo na kwamba watu hao kwa sasa wameanza kujidhihirisha hadharani.

“Baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaoshabikia migogoro inayolikumba taifa  na kukwamisha  jitihada za rais wetu za kutuletea maendeleo, hawana uzalendo,” alisema Zamaradi.

Alisema Serikali imesikitishwa na hujuma zinazofanywa waziwazi na kwa ushabiki wa hali ya juu na baadhi ya viongozi hao za kupingana na mwelekeo mzuri wa Rais  Magufuli katika kuleta maendeleo.

“Kwa mtu yeyote mwenye uchungu na nchi, angepambana na jambo linalohusu masilahi ya taifa likiwamo la kununua ndege lisikwame, kama kuna mkwamo basi ashiriki kukwamua badala ya kushabikia,” alisema Zamaradi.

Alisema mbali na kuhujumu masuala ya maendeleo, Serikali pia ina fununu kwamba wanasiasa hao wanahujumu hali ya usalama wa raia kwenye baadhi ya maeneo ya nchi.

Zaidi alilishutumu kundi hilo la wanasiasa akisema kuwa waliwahi kuomba wafadhili wasilete misaada nchini.

“Tunachojiuliza kama Serikali, hivi misaada isipoletwa anayekomolewa ni Rais Magufuli au ni Watanzania wanyonge ambao wangekosa madawa, huduma za maji, umeme, n.k?” alihoji Zamaradi.

Alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na wanasiasa hao, lakini kwa sasa washirika wameongezeka.

“Mifano ya wazi ya hivi karibuni ni tamko la Serikali ya Marekani kupitia balozi wake, kwamba itaongeza kiasi cha misaada Tanzania, ziara ya tajiri mashuhuri duniani,  Bill Gates, ujio wa viongozi wakuu wa nchi 15 ndani ya muda ambao Mhe. Magufuli amekuwa madarakani na mambo mengine mengi,” alisema Zamaradi.

 

HATUA ZINAZOCHUKULIWA KUINUSURU NDEGE

Akizungumzia hatua ambazo Serikali imeanza kuchukua ili kunusuru ndege hiyo, Zamaradi alisema ni za kidiplomasia na kisheria na endapo zitakamilika,  itawasili nchini na waliokuwa wakikwamisha watapanda.

Nyingine ni kuendelea na uchunguzi na kutosita kuchukua hatua za kisheria kwa watu wanaoshabikia na kutengeneza migogoro na hujuma mbalimbali dhidi ya maendeleo ya taifa.

Alisema Serikali ya awamu ya tano inawahakikishia Watanzania kwamba ndege hiyo itakuja.

 

AKATAA KUJIBU MASWALI

Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo ya tamko la nakala tatu, Zamaradi alikataa kujibu maswali ya waandishi wa habari, ambayo miongoni mwake ni pamoja na kutaja mahakama na nchi iliyofunguliwa kesi hiyo na kiasi  cha fedha zinazodaiwa Serikali.

“Nimesema sitaki maswali na siwezi kuendelea kufafanua zaidi ya hapo, nendeni huko walikoanza kuwapa taarifa watawaambia.

“Kama mnataka maelezo zaidi ya upande wa Serikali, subirini muda mwafaka utafika, baada ya mchakato kukamilika wanasheria watatoa ufafanuzi na kuja kuelezea suala hilo, pia kuhusu ndege itakuja lini hii itategemea na mwenendo wa kesi,” alisema Zamaradi.

 

LISSU AJIBU HOJA ZA SERIKALI

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema kauli iliyotolewa na Zamaradi kwa niaba ya Serikali haiwezi kujibiwa na Lissu kwa kuwa si ngazi yake.

Alisema hoja za kuhusu kushikiliwa kwa ndege hiyo kwa uzito wake na mtu aliyezitoa, zilipaswa kujibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Seikali (AG), George Masaju.

Makene aliahidi kujibu hoja za Serikali yeye mwenyewe kwa kuwa zimetolewa na mtu anayelingana naye kihadhi.

Hata hivyo, baadae Makene alituma taarifa iliyoandikwa na Lissu, akijibu hoja zilizoibuliwa na upande wa Serikali.

Kupitia andiko hilo, Lissu alielekeza lawama zote kwa Serikali na hususani Rais Magufuli juu ya sakata la ndege ya Tanzania kushikiliwa Canada ikiwa ni pamoja na madeni ambayo inadaiwa.

“Aliyeingia mkataba wa ujenzi wa Wazo Hill-Bagamoyo Road na Kampuni ya SCEL ni Tundu Lissu au aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli?” alihoji Lissu.

Hakuishia hapo, alikwenda mbele na kueleza kwamba yote hayo ni matokeo ya uamuzi wa kuvunjwa kwa mikataba ambako kulifanywa pasipo kujali sheria au madhara yatokanayo na hatua hizo.

 

ZITTO KABWE

Mbali na Lissu, Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT–Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye alikuwa wa kwanza kabla ya Lissu kuhoji kuchelewa kwa ndege hiyo kupitia ukurasa wake wa twitter kwa kumtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa kutoa ufafanuzi, naye alishangazwa na majibu hayo ya Serikali.

“Mimi kama mbunge wa upinzani, nilihoji suala hilo kwa ajili ya kutimiza wajibu, hivyo Serikali inapaswa kujibu hoja zilizopo.

“Wao waliahidi ndege itafika mwezi Julai, lakini Serikali haijawaambia watu kwa nini ndege hiyo haijafika. Nilihoji kwenye mtandao na waziri alinijibu itafika,” alisema Zitto.

Alikwenda mbali zaidi na kudai kwamba alifikia hatua ya kuhoji sababu za ndege hiyo kuchelewa kutokana na kuwa na taarifa kwamba hali ya fedha serikalini haikuwa nzuri.

“Niliuliza kama je, hatujalipa? Kwa sababu nafahamu kama mbunge, serikalini kuna shida ya pesa,” alisema Zitto.

Alisema alipojitokeza Lissu juzi na kufanya mkutano wa kuelezea kwa nini ndege zimechelewa, Serikali ilipaswa kuthibitisha tuhuma hizo.

“Nimekuwa Mwenyekiti wa PAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali) kwa miaka minane, kwa sababu hiyo najua Serikali inadaiwa sana nje ya nchi na sio hao tu waliokamata Bombardier, wapo wengi,” aliongeza Zitto.

Alisema Serikali kwa kulitambua suala hilo, ilianzisha Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) ili wadeni hao wasishikilie ndege hizo.

“Sio tu kampuni hiyo, Wallif wanaidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 60, jambo hilo wamelifanyia kazi PAC, kuna tetesi madeni ya namna hiyo yapo mengi sana. Tusishangae hata ubalozi wetu wa Ujerumani au Uingereza au popote kule ukashikwa kwa sababu ya madeni,” alisema Zitto.

Akijibu swali ni kwa nini basi wadeni hawa wameanza kushika mali za Serikali wakati huu pamoja na kwamba madeni haya yalikuwapo tangu siku za nyuma, Zitto alisema: “Jambo hili linafikirisha.

“Lakini Tanzania haiwezi kufanya mambo yake kama kisiwa na maamuzi tunayoyafanya pia  yazingatie maarifa.”

Akizungumzia kuhusu hatua ya Serikali kuwahusisha wapinzani na vitendo vya kula njama kwa ushirikiano na wageni hata kukamata ndege hizo, Zitto aliitaka Serikali kuchunguza madai hayo na kuchukua hatua kama itapata ushahidi.

“Serikali kama ina ushahidi wa tuhuma itukamate na kutushtaki, vinginevyo zitakuwa ni porojo za siasa za mtaani,” alisema Zitto.

 

JULIUS MTATIRO

Aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Segerea kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, katika andiko lake linalosambaa mitandaoni, alieleza kushangazwa na hatua ya  Serikali ambayo pamoja na kukiri tukio hilo, inalazimisha watu waamini kuwa kinachokwamisha maendeleo ya taifa ni wapinzani waliofichua ukamatwaji wa ndege hiyo.

Rais Magufuli alipoingia madarakani aliahidi kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kununua ndege mpya  nne  zitakazosimamiwa na shirika hilo.

Mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka jana, ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q400 zilizonunuliwa na Serikali, zilizwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), huku ndege nyingine kubwa ikitarajiwa kuingia mwezi uliopita.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kama tuhuma zinazoenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa Lisu ndiye aliyefanikisha mpango wa kuizuia ndege isiingie nchini kwa wakati uliopangwa, basi kitendo hiki kinapaswa kulaniwa na wanchi wale wote tunaopenda maendeleo ya nchi yetu. Kwani hii inaonesha kuwa mhe. Tundu Lisu amekosa uzalendo kwa nchi yake na zaidi ameweka mbele maslahi yake binafsi ya kisiasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles