23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

CCM YATIA MGUU MGOGORO WA MEYA MWANZA

BENJAMIN MASESE NA JUDITH NYANGE -MWANZA

SAKATA la kumng’oa Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire, limechukua sura mpya baada ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza kuwahoji viongozi wa Serikali.

Taarifa zilizolifikia MTANZANIA Jumapili kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CCM Mkoa wa Mwanza, zinadai kwamba Kamati ya Siasa ya Mkoa, juzi iliwahoji Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula.

Wengine waliohojiwa ni Meya Bwire, Naibu wake Bhiku Kotecha, Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Diwani wa Kata ya Mkolani, Dismas Rite, Donatha Gapi (Mkuyuni), John Minja (Igogo), Musa Magabe (Igoma) na Vicent Tegge wa Luchelele.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kukwama kufanyika kwa vikao viwili tofauti ndani ya siku mbili kutokana na madiwani 19 kati ya 21 kutia saini ya mashtaka 23 dhidi ya Meya Bwire.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Mwanza, Simon Mangelepa, amethibitisha kuhojiwa kwa viongozi hao ingawa hakufafanua zaidi.
“Ni kweli Kamati ya Siasa ya Mkoa imekutana leo (juzi) kuujadili mgogoro wa meya, mkurugenzi na madiwani. Kuna baadhi yao watahojiwa, siwezi kuwaambia kwa sasa kwa sababu na mimi sijui ni nani na nani wapo kwenye orodha ya kuhojiwa, ila wakikamilisha na kunielekeza kutoa taarifa yake tutafahamishana,” alisema.

Aidha Mangelepa hakuwa tayari kueleza uwepo wa Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM ngazi ya taifa ambayo inadaiwa kufika Mwanza kushughulikia mgogoro huo, bali alisema anachokitambua ni kuwa mara baada ya Kamati ya Siasa Mkoa kumaliza, ingebainisha mgogoro huo ushughulikiwe na ngazi gani.
MTANZANIA Jumapili lilishuhudia juzi viongozi wakiingia kwa zamu katika Ofisi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo kuhojiwa. Aliyekuwa wa kwanza kuingia ofisini humo ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na kufuatiwa na Mbunge wa Nyamagana na Naibu Meya.

 

MGOGORO ULIVYOANZA KUIBUKA

Mgogoro huo ulibuka katika kikao cha madiwani Agosti 15, mwaka huu baada ya Diwani wa Mkuyuni,  Donatha Gapi, ambaye ni Katibu wa Madiwani wa CCM, kusimama na kuwasilisha hoja  ya kutaka mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni meya, asiwe mwenyekiti badala yake kiti kikaliwe na naibu wake.

Hoja ya Gapi iliwasilishwa kabla ya Meya Bwire kusimama kufungua kikao hicho, kitendo ambacho kilidhihirisha kuwapo kwa mpango wa kumng’oa.
Hata hivyo Meya Bwire alifanikiwa kuipangua hoja ya diwani huyo na kufungua kikao hicho, huku akiwaonya wajumbe kutomjadili yeye kwa vile haikuwa moja ya ajenda zilizopo mezani kwake.

Kutokana na majibu hayo, Mbunge Mabula aliingilia kati na kumshauri meya kuondoka ili naibu wake aendeshe kikao, lakini ushauri huo haukuweza kufua dafu.

Baada ya Mabula kuketi Meya Bwire alisimama kwa mara nyingine kusisitiza kuwa hawezi kuondoka, hivyo akawataka madiwani kujadili kilichowasilishwa mezani hatua ambayo iliwafanya kutoka nje ya  ukumbi na kumwacha yeye na madiwani watatu wanaomuunga mkono.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles