NA SAMWEL MWANGA
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Mwamishali wilayani Meatu wameanza kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo huku wakipongeza uamuzi wa Rais Kikwete wa kuagiza ujenzi wa maabara kwa shule zote za kata.
Pongezi hiyo zilitolewa jana ba Mariamu Mwirabi, mbele ya Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Khatib Chum alipofungua
vyumba vitatu vya maabara katika shule hiyo.
Mwirabi alisema kabla ya agizo hilo walikuwa wakisoma masomo ya sayansi kwa kutumia picha na michoro hali ambayo iliwafanya wanafunzi wengi kuyakimbia masomo hayo.
“Kwanza tunapenda kumshukuru rais wetu kwa kuona umuhimu wa kutoa agizo hili kwa sasa imetusaidia kwa vile awali baadhi yetu walikuwa wakikimbia masomo ya sayansi lakini baada ya kuanza kusoma kwa vitendo masomo yanaonekana rahisi,” alisema .
Walisema awali shule za kata zilikuwa zikidharauliwa na baadhi ya watu kwa kukosa ubora lakini baada ya kujengwa maabara shule hizo zimeanza kuonyesha ubora wake kwa kufaulu wanafunzi wengi.
Naye Chum alisema dhamira ya serikali kusisitiza ujenzi huo ni kuongeza wataalamu wakiwamo wahandisi na madaktari.
“Dhamira ya serikali kujenga vyumba vitatu vya maabara kwa ajili ya kemia, bailojia na hisabati tuweze kupata wataalamu wa kutosha katika fani mbalimbali za sayansi zikiwamo za kupata madaktari na wahandisi hivyo ni vizuri tukaitumia fursa hii kutoa elimu bora,” alisema.