NA EMMANUEL IBRAHIM
WANANCHI wa Geita Mjini wamesema wamefurahia kurudishwa jina la mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema, Rogers Luhega, kwa vile amekuwa mtetezi wa masuala ya maji na wachimbaji wadogo migodini.
Wlikuwa wakizungumza juzi wakati wanatoka kumsindikiza mgombea huyo kurudisha fomu ya kuwania jimbo hilo ambalo kwa muda mrefu linashikiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa wananchi hao, mbali na changamoto zinazowakabili, wilaya na Mkoa wa Geita ni miongoni mwa maeneo yenye raslimali nyingi ikiwamo dhahabu, hifadhi na ziwa Victoria lakini hakuna manufaa yoyote yalitopatikana kwa wananchi .
“Uchaguzi huu tunataka mabadiliko hatutakosea kuchagua kwa vile tumejipanga, tunashukuru jina la mgombea tunayemtaka limerudi sasa kazi imebaki kwetu kuhakikisha tunampa ridhaa ya kutuletea maendeleo yaliyokosekana kutoka kwa viongozi waliopita kupitia CCM,’’alisema Juma Salumu mkazi wa mjini Geita.
Wananchi hao walisema wanakabiliwa na kero ya maji kwa muda mrefu lakini wamekuwa wakiahidiwa na viongozi wa CCM bila mafanikio, hivyo wamejipanga kumchagua.
Akiwapongeza wananchi waliojitokeza kumsindikiza wakati wa kurudisha fomu, Luhega alisema wakati wa mapambano umewadia na aliwaomba wananchi kumuunga mkono awatumikie na hatimaye kutatua kero zilizopo.
“Sina mengi ya kuzungumza mimi nitakuwa na nyinyi bega kwa bega kikubwa naombeni ridhaa yenu nifufue maendeleo kwa kasi. Wwezo huo ninao, nina mambo mengi ya kuwaeleza na tutaelezana katika kampeni,” alisema.