MFUNGAJI wa bao la Simba, Daniel Lyanga, amesema ametoa bao hilo kama zawadi kwa Kocha Mkuu wake, Dylan Kerr, kutokana na kumwamini na kumpa nafasi katika kikosi chake cha kwanza.
Lyanga alisema mbali na kumpa zawadi kocha wake Kerr, lakini pia amefurahishwa na kiwango chake kizuri ambacho kimekuwa kikiongezeka siku hadi siku tangu ajiunge na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu.
Akizungumza na MTANZANIA, Lyanga aliyewahi kuichezea Coastal Union kwa misimu mitatu alisema amejisikia faraja kufunga bao lake la kwanza akiwa kwenye kikosi cha Simba.
“Najisikia faraja nikiwa kama mshambuliaji ninapofunga bao ina maana hapo nimekuwa nimetimiza majukumu yangu vizuri, kikubwa naomba wenzangu tuendelee kushirikiana mambo mazuri zaidi yanakuja tukiwa na umoja,” alisema Lyanga.
Alisema amejipanga kuhakikisha anaisaidia Simba kutwaa ubingwa msimu huu, kutokana na timu hiyo kuwa na kikosi kizuri kinachoundwa na nyota wengi wa kimataifa na wazawa kitu ambacho kitamfanya kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi.
Lyanga alisema katika mchezo wa juzi wangeweza kuibuka na ushindi usiopungua mabao matatu, lakini mvua iliyonyesha jijini humo ilipoteza malengo yao kwani uwanja ulikuwa unateleza.