NA ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM
KOCHA mpya wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, George Lwandamina, ameweka wazi mikakati yake ya kazi, huku akiwaahidi Wanajangwani hao soka safi kama la klabu ya Barcelona ya nchini Hispania.
Mzambia huyo aliyazungumza hayo jana, wakati akitambulishwa rasmi mbele ya waandishi wa habari na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, Makoa Makuu ya klabu hiyo, jijini Dar es Salaam.
Kocha huyo wa zamani wa timu ya Zesco ya Zambia, amechukua mikoba ya Mholanzi Hans van der Pluijm, aliyepewa majukumu mapya ya ukurugenzi wa benchi la ufundi la timu ya Yanga.
Baada ya utambulisho huo, Lwandamina alisema ana mpango wa kukibadili kikosi cha Wanajangwani hao kwa kucheza soka la pasi fupi fupi, kushambulia na kukaba kwa pamoja, kama ilivyofanya klabu ya Barcelona.
“Najua kuna changamoto kubwa katika kuanza maisha mapya hadi nije kuzoea mazingira ya ligi ya ndani, wachezaji, wafanyakazi wenzangu kwenye penchi la ufundi pamoja na uongozi kwa ujumla katika kufanya kazi pamoja, lakini nitapambana kwa kufanya kila kilicho ndani ya uwezo wangu,” alisema Lwandamina.
Kocha huyo aliyeipa mafanikio ya kuifikisha Zesco hatua ya nusu fainali ya Klabu Bingwa mwaka huu, alisema aliiona Yanga katika mechi yake ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ikishinda 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting na amegundua ni timu nzuri ambayo haihitaji mabadiliko makubwa.
“Niliiona Yanga kwenye mechi yake ya mwisho ya ligi mzunguko wa kwanza pamoja na kwenye CD nilizoletewa na kugundua kila mchezaji ana uwezo gani, kwa kuangalia hakuna mapungufu makubwa ya kufanyiwa marekebisho, lakini kama kutakuwa na jambo la ulazima kufanyika nafikiri litajulikana baada ya kukutana na wachezaji na kukaa nao kwa muda,” alisema Lwandamina.
Hata hivyo, Lwandamina alimsifu pia mtangulizi wake, Pluijm kwa kufanya kazi nzuri, huku akimuahidi kufuata nyayo zake pamoja na kushirikiana naye bega kwa bega kuhakikisha Yanga inapata mafanikio zaidi katika ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa.
Kwa upande wa Pluijm, alisema ameushukuru uongozi wa Yanga kwa kuendelea kuona umuhimu wake kwa kumpa majukumu mapya, huku akiahidi kutoa sapoti kubwa kwa Lwandamina.
“Sina tatizo na Yanga, nimeridhia majukumu mapya waliyonipa na ninaahidi kushirikiana na Lwandamina hatua kwa hatua ili kuipa mafanikio timu,” alisema Pluijm.
Pluijm anaachia nafasi ya ukocha Yanga, ikiwa ni baada ya kuiongoza katika mechi 128 kwenye awamu mbili, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23, lakini pia akiwawezesha Wanajangwani kutwaa mataji matatu msimu uliopita ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ‘FA’, pamoja na kuifikisha hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 ilipofika hatua ya makundi.
Akizungumzia kambi ya wachezaji, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Sanga, alisema kuwa, kikosi kinataraji kuanza mazoezi Jumatatu jijini Dar es Salaam, kabla ya kuamua sehemu ya kwenda kuweka kambi itakayopendekezwa na benchi la ufundi.
“Wachezaji wataanza mazoezi rasmi Jumatatu hapa hapa jijini Dar es Salaam, kipindi ambacho tunasubiri mapendekezo ya benchi la ufundi kama watahitaji kwenda kuweka kambi nje ya Tanzania.
“Kuhusu kocha msaidzi kwa sasa ataendelea kuwa Juma Mwambusi, Meneja akiwa Hafidhi Saleh, Kocha wa Makipa Juma Pondamali na kama kutakuwa na mabadiliko kwenye sehemu hiyo taarifa itatolewa na uongozi,” alisema Sanga.
Yanga wamemtambulisha Lwandamina baada ya kuficha kwa muda mrefu kabla ya kuja kutangaza Jumatatu iliyopita kuingia naye mkataba wa miaka miwili kukinoa kikosi chao.
Mbali na Ligi Kuu, Lwandamina pia ana jukumu zito la kuifikisha Yanga katika fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika au Kombe la Shirikisho, hatua ambayo Pluijm hajaweza kufika.